WAZIRI wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, amesema Rais Samia Suluhu Hassan ameagiza mikataba ya ujenzi wa miundombinu ya barabara iasainiwe hadahrani ili wananchi waweze kushuhudia na kufuatilia utekelezaji wake. Anaripoti Mwandishi Wetu, Mbeya … (endelea).
Mbarawa amebainisha hayo leo Jumanne tarehe 27 Desemba, 2022, wakati wa utiliaji saini mkataba wa ujenzi wa barabara tatu zenye jumla ya kilomita 32 zilizopo Kyela Mkoani Mbeya.
Mbarawa amesema Rais alimhoji sababu ya Wakala wa Barabara Tanzania TANROADS, kusaini mikataba ya ujenzi wa miundombinu ndani na kuagiza kuanzia sasa mikataba hiyo isainiwe hadharani
“Mheshimiwa Rais aliniuliza kwanini TANROADS wanakuwa na utaratibu wa kujifungia kwenye chumba wanasaini miradi, akasema kwaajili ya mradi huu nendeni Kyela mkasaini mradi huu mbele ya wananchi wote washuhudie,” amesema Mbarawa.
Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Juma Homera amempongeza Rais Samia kwa kutoa maagizo hayo.
“Watanzania lazima wajue, hii mikataba siku zote huwa inasainiwa makao makuu ya TANROADS, leo hii kwa mara ya kwanza toka nchi hii izaliwe tunasaini mikataba hadharani ili wananchi waweze kujua mikataba hii imesainiwa…ili muone Mheshimiwa Rais barabara hii anakuja kuijenga,” amesema Homera.
Ujenzi wa kilomita 32 utahusisha Barabara ya Ibanda-Kajunjumele kilomita 22, Kajunjumele-Kiwara Port kilomita 6, Kajunjumele-Itungi Port kilomita 4 kwa kiwango cha lami. Barabara hizio zitaunganisha mkoa wa Mbeya na mikoa ya Ruvuma na Njombe kupitia ziwa Nyasa.
Leave a comment