May 25, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Rais Samia aagiza kesi za ‘kubambikiza’ zifutwe

Rais Samia Suluhu Hassan

Spread the love

 

RAIS wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ameiagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini humo (TAKUKURU), kuzifuta kesi zote zisizokidhi misingi ya kisheria na za kubambikiza, zilizoko mahakamani. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma…(endelea).

Agizo hilo amelitoa hilo leo Jumapili tarehe 28 Machi 2021, Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma, baada ya kupokea taarifa ya utendaji kazi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (TAKUKURU) , kwa mwaka 2019/2020.

Rais Samia amemuagiza Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Brigedia Jenerali John Mbungo, kuzipitia upya kesi zote zilizoko mahakamani na majalada ya uchunguzi yanayotarajiwa kufunguliwa mahakamani, ili kufuta zisizokuwa na misingi ya kisheria.

“Kuna kesi tunashindwa labda hazikuwa na misingi mizuri au zilikuwa za kubambikiza, yote yapo hayo. Kwa hiyo mkurugenzi naomba uzitazame vizuri. Zile ambazo una hisi huna misingi mizito ya kwenda kushinda zifute kabla hujazipeleka huko,” ameagiza Rais Samia.

Rais Samia amesema “Kwa sababu kila siku kusema tumelepeka kesi 300 halafu 130 tumeshindwa , haileti taswria nzuri kwa Serikali.”

Kiongozi huyo wa Tanzania amesema, hatua hiyo itaipunguzia TAKUKURU mrundikano wa kesi zisizokuwa na mashiko.

“Nikiangalia idadi ya kesi mlizonazo na zile ambazo mlizofanyia kazi ziko mahakani, ziko nusu kwa nusu.
Kwa hiyo mimi naomba kuliko kujirundikia makesi angalieni zile ambazo hazina misingi, hazikupeni uhalali kwenda mahakamani mzifute ili muondoe huo mzigo kwenye faili zenu,” ameshauri Rais Samia.

Wakati huo huo, Rais Samia ameiagiza TAKUKURU iharakishe mchakato wa rasimu ya mapendekezo ya uboreshaji Sheria ya Kupambana na Rushwa, ili sheria hiyo iendane na wakati.

“Nimefurahi namna mlivyo andaa rasimu ya mapendekezo ya kuboresha Sheria ya Kupambana na Rushwa, ni kweli kwa wakati tulionao nadhani sheria yetu inahitaji mapitio. Naomba mshirikiane zifikishwe bungeni kwa haraka,” ameagiza Rais Samia.

error: Content is protected !!