Thursday , 2 February 2023
Home Gazeti Habari Mchanganyiko Rais Samia aagana na Balozi wa China, asema…
Habari Mchanganyiko

Rais Samia aagana na Balozi wa China, asema…

Spread the love

 

RAIS wa Tanzani, Samia Suluhu Hassan, ameagana na aliyekuwa Balozi wa China nchini humo, Wang Ke, ambaye amemaliza kipindi chake cha uwakilishi. Anaripoti Jemima Samwel, DMC … (endelea).

Mazungumzo baina ya viongozi hao wawili, yamefanyika leo Ijumaa, tarehe 4 Juni 2021, Ikulu ya Chamwino, mkoani Dodoma.

Rais Samia amemshukuru, Balozi Wang Ke kwa jitihada zake za kuendeleza na kukuza uhusiano wa Tanzania na China ambao umewezesha kutekelezwa kwa miradi mbalimbali iliyofadhiliwa na China.

Baadhi ya miradi hiyo, Rais Samia ameitaja kuwa ni; maktaba ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, jengo la Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki lililopo jijini Dar es Salaam na msaada wa Sh.35 Bilioni zilizoelekezwa katika miradi ya maendeleo.

Rais Samia pia, amemshukuru kwa ufadhili wa China katika miradi mbalimbali ya ujenzi wa miundombinu na uboreshaji wa huduma za kijamii pamoja na ushirikiano wa kibiashara na uwekezaji ambao pamoja na kukuza pato la nchi umesaidia Watanzania wengi kupata ajira.

 

Amepokea salamu za Rais wa China, Xi Jinping na amemtakia yeye na Wachina wote maadhimisho mema ya miaka 100 ya Chama cha Kikomunisti cha China (CPC) itakayotimia tarehe 01 Julai, 2021.

Rais Samia, ameshukuru kwa uhusiano na ushirikiano mzuri kati ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na CPC na uhusiano na ushirikiano kati ya Tanzania na China uliodumu kwa miaka 56.

Amesema anatambua kazi kubwa iliyofanywa na CPC katika kuijenga China, kujenga na kuimarisha uhusiano wake na Mataifa mbalimbali ikiwemo Tanzania na amemhakikishia kuwa Tanzania itaendeleza na kukuza zaidi uhusiano na ushirikiano huo.

Kwa upande wake, Balozi Wang Ke, amemshukuru Rais Samia kwa ushirikiano mkubwa alioupata kutoka serikalini wakati wote wa kipindi chake cha Ubalozi na amempongeza kwa kupokea kijiti cha Urais kutoka kwa aliyekuwa Rais wa Tanzania, Hayati John Pombe Magufuli.

Amewasilisha salamu za Rais wa China, Xi Jinping ambaye amesema ana imani kubwa kuwa Rais Samia atafanya mazuri na makubwa kwa Tanzania kutokana na dhamira yake ya kuendeleza kazi nzuri iliyofanywa na mtangulizi wake, Hayati Magufuli, hususani uendelezaji wa miradi ya kimkakati, kuchukua hatua madhubuti za kuboresha mazingira ya kufanya biashara na kuchukua hatua za kisayansi za kukabiliana na janga la ugonjwa wa Korona (Covid-19).

Amesema China itaunga mkono juhudi zinazofanywa na Rais Samia na ameshukuru kwa salamu za heri na pongezi kwa chama cha CPC kutimiza miaka 100 ambapo pamoja na kufanya mageuzi na kuleta maendeleo makubwa kwa China.

Chama hicho, kimekuwa kutoka wanachama 50 hadi wanachama milioni 92 na kwa sasa kipo katika mchakato wa mageuzi mengine ya mfumo wake wa ujamaa wenye misingi ya Kichina utakaojenga nchi ya kisasa zaidi na kutoa elimu ya historia ya China kwa vijana wake.

Aidha, Balozi Wang Ke amesema, China ipo tayari kushirikiana na Tanzania katika kukabiliana na ugonjwa wa Korona.

Mazungumzo hayo yamehudhuriwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Masharik, Mbarouk Nassor Mbarouk.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari Mchanganyiko

GGML kuwapatia mafunzo kazi wahitimu 50 wa vyuo vikuu nchini

Spread the loveJUMLA ya wahitimu 50 wa vyuo vikuu nchini wamepata fursa...

Habari Mchanganyiko

NHC yaongeza mapato kufikia kufikia Sh bilioni 257

Spread the loveSHIRIKA la Nyumba la Taifa (NHC) limeongeza mapato hadi kufikia...

Habari MchanganyikoTangulizi

Mo Dewji achomoza bilionea pekee Afrika Mashariki

Spread the loveMAZINGIRA mazuri ya uwekezaji nchini Tanzania yamezidi kuleta matunda baada...

Habari Mchanganyiko

Rais Samia: Panapotokea uvunjifu wa amani panakuwa haki imepotezwa

Spread the love  RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu...

error: Content is protected !!