May 25, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Rais Ramaphosa ataja siri Magufuli kutosafiri nje

Cyril Ramaphosa, Rais wa Afrika Kusini

Spread the love

 

RAIS wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa amesema, aliyekuwa Rais wa Tanzania, Hayati John Pombe Magufuli, alimwambia hapendi kusafiri nje ya nchi, kwa kuwa alitaka kupata muda wa kutosha kuwatumikia Watanzania. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma…(endelea).

Kiongozi huyo wa Afrika Kusini, ametoa kauli hiyo leo Jumatatu tarehe 22 Machi 2021, katika mazishi ya kitaifa ya Hayati Magufuli, iliyofanyika makao makuu ya nchi, jijini Dodoma.

Akielezea historia ya Hayati Magufuli, Rais Ramaphosa amesema, awali alidhani mawanasiasa huyo anaogopa kupanda ndege, lakini baadaye alifahamu kwamba alibaki Tanzania kuwatumikia wananchi wake.

“Magufuli alikuwa sio msafiri mkubwa, alikuwa hapendi kusafiri. Alipenda kubaki nyumbani, nilidhani alikuwa anaogopa kusafiri kwenye ndege, lakini aliniambia alibaki hapa kuendelea kuwatumikia Watanzania badala ya kutembelea nchi za nje,” amesema Rais Ramaphosa.

Rais Ramaphosa amesema Hayati Rais Magufuli alimueleza siri hiyo alipokwenda Afrika Kusini, kushuhudia sherehe yake ya kuapishwa kuwa Rais wa taifa hilo kusini mwa Afrika.

Mwanasiasa huyo aliyeapishwa Februari 2018 kuwa Rais wa Afrika Kusini, amesema ujio wa Hayati Rais Magufuli nchini humo, ulimfanya ajisikie anaheshimiwa.

Hayati Rais Magufuli alifariki dunia tarehe 17 Machi 2021, katika Hospitali ya Mzena, Makumbusho mkoani Dar es Salaam, alikokuwa anapatiwa matibabu ya matatizo ya mfumo wa umeme wa moyo.

Mwili wake unatarajiwa kuzikwa kijijini kwao Chato mkoani Geita, Ijumaa tarehe 26 Machi 2021.

Hadi umauti unamkuta, Hayati Magufuli hakuwa na desturi ya kusafiri nje ya nchi na hakuwahi kusafiri kwenda nje ya Afrika.

error: Content is protected !!