RAIS wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Dk. Hussein Ally Mwinyi, amezindua Kamati ya Maridhiano Visiwani, yenye lengo la kuendeleza dhamira ya kushirikiana na kuimarisha Umoja wa Kitaifa Zanzibar. Anaripoti Mwandishi Wetu, Zanzibar … (endelea).
Halfa ya uzinduzi huo, imefanyika leo, Ikulu mjini Unguja, ambapo Rais Mwinyi, alitumia fursa hiyo, kumshukuru Rais wa Jamhuri na mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan, kwa kumridhia kukutana na kufanya mazungumzo na viongozi wakuu wa chama cha ACT- Wazalendo.
Katika hafla hiyo, iliyohudhuriwa na viongozi mbalimbali, wakiwamo Juma Duni Haji, Mwenyekiti wa taifa wa ACT – Wazalendo; Zitto Zuberi Kabwe, Kiongozi Mkuu wa chama hicho na Othman Masoud Othman, makamu mwenyekiti wake Zanzibar na Makamu wa Kwanza wa Rais Visiwani.
Wengine, ni Mjumbe wa Kamati Kuu (CC) ya CCM na Makamu wa Pili wa Rais, Hemed Suleiman Abdullah, pamoja na viongozi wengine mbalimbali wa chama hicho Visiwani.

Dk. Mwinyi alimshukuru Rais wa Samia kwa uamuzi wake wa kufanya vikao na viongozi mbalimbali wa vyama vya siasa na kusikiliza maoni yao, ambayo amesema “yameendelea kuyafanyiwa kazi na kutekeleza kwa vitendo azma ya kuleta maridhiano ya kisiasa ikiwemo kuunda Kikosi Kazi, kilichopitia ripoti ya Baraza la Vyama vya Siasa nchini.
Aidha, Dk. Mwinyi alisema, rais Samia ameimarisha uhuru wa kisiasa na kidemokrasia kwa kuruhusu tena kufanyika kwa mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa, na kuanzisha mchakato wa Katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano.
Amesema, hotuba yake aliyoitoa Novemba 2020 wakati anazindua Baraza la Wawakilishi, kwamba dhamira yake ni kuwaunganisha wananchi wote wa Zanzibar kuwa wamoja, bila kujali rangi, asili, imani za dini au itikadi za kisiasa, yaweza kuthibitishwa na kitendo chake hicho.
Dk. Mwinyi alisema, “dhamira ya kuiendeleza Zanzibar, ni jukumu la kila mmoja.”
Hata hivyo, taarifa iliyotolewa na Ikulu ya Zanzibar, leo Jumatano, tarehe 31 Mei 2023, haikutaja majina ya wajumbe wa Kamati ya Maridhiano ambayo rais Mwinyi ameripotiwa kuizundua.
Leave a comment