Spread the love

RAIS wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi ameshauri matumizi ya rasilimali za bahari katika utekelezaji wa sera ya uchumi wa buluu, yawe endelevu. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam…(endelea).

Rais Mwinyi ametoa wito huo leo Jumatano, tarehe 9 Machi 2022, akizungumza katika mkutano wa mwaka wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF).

“Mtu akiniuliza uchumi wa buluu ni kitu gani, kwa lugha nyepesi ninasema kwamba ni matumizi endelevu ya rasilimali za bahari kukuza uchumi wa Serikali na uchumi wa mtu mmoja mmoja. Ndani ya tafsiri hii kuna maneno mazito mawili, matumizi endelevu,” amesema Rais Mwinyi.

Rais Mwinyi amesema “hili neno endelevu lisipuuzwe hata kidogo, sababu tukiwa na matumizi tu ya rasilimali bahari tutaharibu mapema. Lazima yawe matumizi endelevu. Kwa maana kila tunachofanya katika kuvuna rasilimali za bahari basi tuzingatie hatuvuni kupita kiasi.”

Mwenyekiti huyo wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar, amesema matumizi endelevu ya rasilimali za bahari yatakuza uchumi wa visiwa hivyo.

Rais Mwinyi amesema, lengo la Serikali yake ni kuweka mikakati ya kuongez amchango wa sekta ya utalii na uvuvi kwenye pato la taifa (GDP).

“Utalii unachangia GDP ya Zanzibar kwa asilimia 30 kwa hiyo ni sekta muhimu sana, sekta ya pili ni uvuvi na ufugaji, nayo inachangia GDP kwa asilimia 30. Sekta hizi tayari zinachangia asilimia 60. Asilimia 30 ya uvuvi inachangiwa na wavuvi wadogo wanaovua samaki wastani wa Kg. 2 hadi 3,” amesema Rais Mwinyi na kuongeza:

“Watu wengi wako katika sekta hiyo, tunataka kuwaondoa kutoka hapo kuwapeleka kwenye tani moja. Ndiyo maana sasa hivi kuna mpango mkakati wa kuwawezesha wavuvi waende masafa marefu baharini warudi na tani badala ya Kg. 2.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *