Monday , 11 December 2023
Home Gazeti Habari za Siasa Rais Mwinyi aanza kujisafishia njia Pemba
Habari za Siasa

Rais Mwinyi aanza kujisafishia njia Pemba

Spread the love

RAIS wa Zanzibar, Dk. Hussein Mwinyi  amesema Serikali yake haijakitenga Kisiwa cha Pemba na kwamba inachukua hatua kuhakikisha maendeleo kati yake na Unguja yanalingana. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam…(endelea).

Mwenyekiti huyo wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar, ametoa kauli hiyo leo tarehe 3 Novemba 2023, katika mahojiano yake na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), kuhusu miaka mitatu ya uongozi wake tangu alivyoingia madarakani 2020, baada ya kuulizwa kama madai ya Pemba kutengwa kimaendeleo ni ya kweli.

Rais Mwinyi amesema kwa sasa Serikali yake inatengeneza miradi mbalimbali ya miundombinu, ikiwemo ya barabara, kiwanja cha ndege na usafiri wa majini, ili kukifungua kisiwa hicho, huku akisema sera maalum ya uwekezaji imewekwa ili kuvutia wawekezaji.

“Tulifanya maamuzi ya makusudi ya kufanya maendeleo yapatikane katika pande zote mbili, Unguja na Pemba, kwa kiwango kinachofanana. La kwanza tuliweka sera inayotoa vivutio vya uwekezaji vikubwa zaidi ukiwekeza Pemba kuliko Unguja kwa upande wa kodi. Kwa sasa ukitaka kupunguziwa kodi ukawekeze Pemba, lengo ni kuvutia watu waende Pemba,” amesema Rais Mwinyi.

Amesema vivutio vya kodi vimepelekea wawekezaji kuanza kuwekeza Pemba  na kwamba kwa sasa kuna ongezeko la ujenzi wa viwanda.

Mbali na kuboresha sera za kikodi, Rais Mwinyi amesema Serikali yake imetenga eneo maalum kwa ajili ya viwanda lililoko Chamanangwe. Imeanza kujenga barabara za kuunganisha wilaya za Pemba, pia imepata fedha kwa ajili ya uboreshaji Kiwanja cha Ndege cha Pemba ili kiwe cha kimataifa.

“Tunataka kiwanja cha ndege kukifanya kuwa cha kimataifa, ndege zinazotoka nje ya nchi ziende moja kwa moja Pemba badala ya kufikia Unguja kisha baadae kwenda pemba. Pia tunataka meli za nje ziende Pemba,” amesema Rais Mwinyi.

Madai Pemba kutengwa kimaendeleo, yametolewa mara kadhaa na wapinzani visiswani humo, kutokana na wananchi wake wengi kuunga mkono vyama vya siasa vya upinzani wakati wa uchaguzi mkuu.

Kuhusu uchumi wa Zanzibar, Rais Mwinyi amesema Serikali yake inaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo, ili kuongeza ukuaji uchumi kwa ajili ya kufikia asilimia 7.1 kila mwaka.

“Baada ya janga la UVIKO-19 tumeona kuna umuhimu wa kuchangamsha uchumi kwa kufanya miundombinu na tulilenga pia kushirikisha kampuni za wazawa za ndani ili kuwe na mzunguko wa fedha na tulitumia zaidi ya Sh. 200 bilioni katika kufanya miradi kwenye sekta za huduma na uchumi,” amesema Rais Mwinyi.

Mwenyekiti huyo wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar, amesema kwa sasa Wizara ya Uchumi wa Buluu visiwani humo, inaendelea na uimarishaji wa sekta hiyo, ikiwemo kuhamasisha wawekezaji kujenga viwanda vya kuchakata samaki, pamoja na kujenga bandari maalum kwa ajili ya uvuvi na kwamba masuala hayo yanatakiwa kukamilika 2026.

Amesema kwa sasa Serikali yake imefanikiwa kuboresha sekta ya uvuvi, kwa kugawa maboti ya kisasa hatua iliyoongeza kiwango cha samaki wanaovuliwa kutoka kilo 4 hadi 40. Pia, imejenga soko la kisasa la samaki Malindi, ambalo lina uwezo wa kutunza tani 250 na kuhudumia watu 6,500kwa siku.

Katika hatua nyingine, Rais Mwinyi amesema serikali yake inaweka mkazo katika sekta ya utalii, ili kuongeza mchango wake katika pato la taifa, ikiwemo kuhamasisha sekta binafsi kuwekeza katika ujenzi wa kumbi za mikutano za kimataifa. Kwa sasa utalii unachangia asilimia 30 ya pato la Zanzibar.

“Mwaka jana watalii walikuwa 548,000, mwaka huu walikuwa 713,000 na tunatarajia kufikia 2025 tuwe tumefifikia watalii 1,000,000 kwa mwaka. Kwa sasa utalii Zanzibar uko maeneo mawili makuu, fukwe za bahari na utalii wa historia kwenye Mji Mkongwe. Kama tunavyozungumza lazima serikali tujipange wakija waweze kutumia fedha zaidi,” amesema Rais Mwinyi.

Mbali na kuimarisha utalii, Rais Mwinyi amesema Serikali yake inaendelea kuweka mikakati itakayosaidia kuboresha kilimo ili mazao yawe na tija, huku akiweka mkazo wa uzalishaji mazao yenye thamani kubwa sokoni hususan viungo.

 

“Kutokana na udogo wa ardhi yetu, tumeamua tujikite katika eneo maalum, kuna zao la chakula kikuu mpunga, tumepata fedha kutoka Korea tukaweka miundombinu ya umwagiliaji, badala ya wakulima kuvuna mara moja watavuna mara mbili au zaidi. Pia tumeamua tujikite katika mazao yenye thamani kubwa, mfano vanilla, karafuu, pilipili manga, ambavyo thamani yake ni kubwa,” amesema Rais Mwinyi.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

Biteko: Samia ni muumini wa maridhiano sio kwa kuigiza

Spread the loveNaibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko...

Habari za SiasaTangulizi

Dk. Mpango: Sitakufa bali nitaishi

Spread the loveMAKAMU  wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk....

Habari za SiasaTangulizi

Mbowe: Miaka 62 ya uhuru tujenge upya mioyo yetu

Spread the loveWAKATI Tanganyika ikiadhimisha miaka 62 tangu kupata uhuru, Mwenyekiti wa...

Habari za Siasa

Rais Samia asamehe wafungwa 2,244

Spread the loveRAIS Dk. Samia Suluhu Hassan, amewasamehe wafungwa 2,244, huku akiwabadilishia...

error: Content is protected !!