May 26, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Rais Museveni aacha somo kwa Watanzania

Spread the love

 

RAIS wa Uganda, Yoweri Museveni, ametumia hotuba yake katika hafla ya utiaji saini mkataba hodhi wa Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP), kutoa somo la uchumi kwa Watanzania. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Leo Alhamisi tarehe 20 Mei 2021, Ikulu jijini Dar es Salaam, Serikali ya Tanzania ilitia saini mkataba huo pamoja na wawekezaji wa EACOP, Kampuni ya Total ya nchini Ufaransa na Kampuni ya Uchimbaji Mafuta ya China (CNOOC).

Hafla hiyo imeshuhudiwa na Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan na Rais Museveni, ambapo mradi huo utatekelezwa kuanzia Hoima-Uganda hadi Tanga-Tanzania.

Akizungumza katika hafla hiyo, Rais Museveni amesema hakuna Serikali iliyofanikiwa kutoa huduma bora za kijamii, pasina kujiimarisha kwenye eneo la uzalishaji mali.

Rais Museveni amesema, watu wengi huwa wanahoji ufanisi wa Serikali katika utoaji huduma za kijamii, badala ya kuhoji namna ya utafutaji fursa za uzalishaji mali, kwa ajili ya kukuza uchumi.

“Sehemu ya kwanza ambayo Waafrika wanajua sana kuhoji hasa wa Uganda, ni ya huduma. Lile jambo wanalielewa sana na wanadai huduma ya afya na elimu. Lakini kuna sehemu nyingine hawaelewi vizuri, kujua kwamba huwezi kuwa na huduma ambayo endelevu bila uzalishaji wa mali,” amesema Rais Museveni.

Rais huyo wa Uganda amesema, uzalishaji mali ndiyo msingi wa maendeleo ya nchi, ikiwemo uboreshwaji utoaji huduma za kijamii.

“Sasa watu wanaozungumzia ustawi wa jamii lazima waeleze sehemu hizo mbili, moja huduma za kijamii, elimu, afya na usalama. Lakini sehemu ya pili muhimu zaidi, tena ya msingi ni uzalishaji mali, sababu huwezi kuwa na maendeleo bila ya uzalishaji mali,” amesema Rais Museveni.

Kiongozi huyo wa Uganda amewashauri Watanzania na Wauganda kujikita katika shughuli za uzalishaji mali, hasa kilimo cha biashara, viwanda, usafirishaji na miundombinu mingine.

Rais Samia Suluhu Hassan

Kuhusu mradi huo, Rais Museveni amewataka wananchi wa pande zote mbili kuchangamkia fursa za ajira zitakazojitokeza, huku akiwahimiza kutosahau shughuli zao nyingine za kiuchumi, walizokuwa wanafanya awali.

“Wananchi wasibweteke na bomba la mafuta na kusahau sekta nyingine, sekta nyingine kama kilimo cha biashara,viwanda na zile sekta nyingine zitasaidiwa na haya mafuta,” amesema Rais Museveni.

Ujenzi wa EACOP unatekelezwa kwa muda wa miaka mitatu, kuanzia 2021 na kumalizika 2024.

error: Content is protected !!