November 29, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Rais Museven awaomba msamaha Wakenya

Rais wa Uganda, Yoweri Museveni

Spread the love

RAIS wa Uganda, Yoweri Museveni amewaomba radhi wakenya kwa machapisho ya mtoto wake aliyoyatoa wiki hii kupitia mtandao wa twitter. Katika kaarifa yake aliyoitoa leo Jumatano tarehe 5 Oktoba, 2022 kwenye ukurasa wake wa twitter Rais Museveni, amesema anasikitika huku  akiwaomba Wakenya msamaha. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).

Museven ameandika kwamba maafisa wa umma, wawe wa kiraia au wa kijeshi, haipaswi kuingilia masuala ya taifa ndugu.

“Nawaomba ndugu zetu wa Kenya watusamehe kwa alichoandika kwenye twitter, aliyekuwa Mkuu wa Majeshi ya Nchi Kavu hapa, Jenerali Muhoozi. Si sahihi kwa maafisa wa Umma, wawe wa kiraia au wa kijeshi, kutoa maoni yao au kuingilia kwa njia yoyote ile, katika mambo ya ndani ya nchi ndugu,” imesema sehemu ya taarifa hiyo.

Mtoto huyo mkubwa wa Museveni, Luteni Jenerali Muhoozi Kainerugaba, Jenerali Kainerugaba alituma jumbe ‘tata’ kwenye mtandao wa Twitter siku ya Jumatatu, na kuibua hasira ya Wakenya wengi mtandaoni.

Katika moja ya ujumbe Kainerugaba alisema kwamba itamchukua yeye na jeshi lake wiki mbili kuuteka mji mkuu wa Nairobi. Kauli iliyoibua hasira kwa Kenya na mjadala mkubwa katika nchi za Afrika Mashariki.

Katika ujumbe mwingine, alisema alisikitishwa na aliyekuwa Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta kwa kutowania muhula mwingine wa urais, wakati angeweza kushinda uchaguzi mwingine kirahisi.

Serikali ya nchi hiyo ilijitenga na kauli yake hiyo iliyoashiria ‘uvamizi’ kupitia taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Uganda.

Taarifa hiyo ilisema kuwa serikali haifanyi sera za kigeni kwenye mitandao ya kijamii, na kwamba Uganda inathamini uhusiano mkubwa uliopo kati ya nchi hizo mbili na Kenya.

Siku ya Jumanne, Rais Museveni alimfuta kazi Jenerali Kainerugaba kama kamanda wa vikosi vya nchi kavu lakini akampandisha cheo cha juu zaidi cha jeshi nchini humo.

Katika taarifa yake ya Jumatano, Museveni alieleza kwamba amempandisha cheo kwa sababu ya michango mingi mizuri ambayo Jenerali Kainerugaba alikuwa ameitoa na bado angeweza kufanya hivyo.

error: Content is protected !!