May 6, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Rais Magufuli: Niombeeni nisiwe na kiburi, jeuri

Rais John Magufuli

Spread the love

RAIS wa John Magufuli amewataka Watanzania kutodharau dawa za kienyeji katika kukabiliana na maradhi mbalimbali. Anaripoti Mwandishi Wetu…(endelea).

Kiongozi huyo wa Tanzania ametoa wito huo leo Alhamisi tarehe 11 Juni 2020, wakati akizungumza katika hafla ya uwekaji jiwe la msingi la ujenzi wa barabara ya lami kwenye mji wa Serikali, ulioko Mtumba jijini Dodoma.

Rais Magufuli amesema miti inayotengeneza dawa za kienyeji imeumbwa na Mungu kwa ajili ya kusaidia wanadamu.

Kauli hiyo ya Rais Magufuli ya kuwataka watu kutodharau dawa za kienyeji, imetokana na mchangao mkubwa wa dawa hizo katika kukabiliana na mlipuko wa ugonjwa ya homa kali ya mapafu, inayosababishwa na virusi vya corona (Covid-19).

“Tunamshukuru Mungu kwa kutuepusha na ugonjwa huu wa Corona kwani sasa hivi mambo yanaenda vizuri, natoa rai kwa Wananchi kutodharau dawa za kienyeji kwani miti yote iliumbwa na Mungu kwa ajili ya kutusaidia sisi,” amesema Rais Magufuli.

Rais Magufuli amesema kujifukiza kwa kutumia dawa za kienyeji kumesaidia wananchi kukabiliana na mlipuko huo, ambao kwa sasa kasi ya mamabukizi yake imepungua kwa kasi.

“Kujifukiza kumesaidia sana, Corona haijaisha sana lakini imepungua sana. Tuendelee kuchukua tahadhari, wale waliokuwa wanasema tutakufa sana na kwamba barabarani kutakuwa na maiti wameshindwa na wakalegee,” amesema Rais Magufuli.

Hata hivyo, Rais Magufuli ameendelea kuwahimiza Watanzania waendelee kujilinda ili wasiambukizwe Covid-19.

“Corona bado haijaisha lakini imepungua sana, hivyo tuendelee kuchukua tahadhari na watu waliodhani tutafariki wengi wameshindwa. Mungu wetu anatupenda na tuendelee kumtegemea yeye,” amesema Rais Magufuli.

Wakati huo huo, Rais Magufuli ameagiza wizara ya afya kukiendelea kitengo cha dawa za asili, kwa kukitengea bajeti yake.

“Nimetoa maelekezo kwa wizara husika kuwa kitengo cha dawa za asili kiendelezwe, na bajeti yake iongezwe ili watu wanapotengeneza dawa zao tusiwadharau, dawa hizo ni tiba kama zilivyo dawa zingine. Niwaombe Watanzania tubadilike,” amesema Rais Magufuli.

Rais Magufuli ametumia fursa hiyo kuwaomba Watanzania kuendelea kumwombea ili awe mtumishi mwema asiyebagua watu.

“Nami kama kiongozi wenu, nitaomba tu muendelee kuniombea nisije kuwa na kiburi, nisije kuwa na jeuri, nikawe mtumishi wa kweli kwa Watanzania wote bila kuwabagua kwa rangi zao au dini zao au makabila yao.”

“Nikatimize wajibu wangu katika kipindi ambacho kimepangwa kwenye katiba ili kusudi baada ya hapo, tuwaachie wengine watakaokuja watimize wajibu wao,” amesema Rais Magufuli

Amesema, “Nataka kuwahakikishia Watanzania, nawapenda na niwahakikishie kazi hii ni ngumu sana, ina mateso, inahitaji sala, dua na nguvu za mwenyezi Mungu katika kuwatumikia Watanzania wote.”

error: Content is protected !!