RAIS John Mafufuli ametoa siri yake ya moyoni, namna alivyonusurika kuuawa kwa kunyweshwa sumu, wakati akiwa Naibu Waziri wa Ujenzi wakati wa utawala wa Rais Mstaafu, Benjamin Mkapa. Anaripoti Martin Kamote … (endelea).
Amesema, kilichomponza ni sifa alizomwagiwa na Rais Mkapa kutokana na uchapa kazi wake, na kwamba jambo hilo hawezi kulisahau.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kitabu cha maisha ya Rais Mkapa kiituwacho ‘Maisha Yangu, Kusudio Langu’ leo tarehe 12 Novemba 2019, katika Ukumbi wa Mikutano wa Julius Nyerere (JNICC), jijini Dar es Salaam amesema, baada ya mkasa huo aliomba kujiuzulu.
Tukio la kunyweshwa sumu lilitokea baada ya Rais Mkapa kumtamka kuwa, Rais Magufuli (wakati akiwa waziri) ndiye askari mwavuli wake namba moja.
“Licha ya dhamira njema ya Mzee Mkapa, suala hilo liliniletea mimi matatizo binafsi. Nilianza kuona dalili za baadhi ya mawaziri, tena wengine wa ngazi za juu kabisa kuanza kunichukia.
“Na muda si mrefu, baada ya hapo nikanyweshwa sumu Dodoma, ambayo almanusura iondoe uhai wangu. Lakini kwa neema za Mweneyzi Mungu, nikakiepuka kifo,” amesema Rais Magufuli.
Kutokana na tukio hilo, amesema alikwenda kwa Mzee Mkapa kuomba kujiuzulu “nakumbuka siku hiyo aliniangalia jicho la baba kwa mwana, akinihurumia,” amesema na kuongeza;
“Lakini baada ya dakika chache akaniambia, nanukuu ‘John kafanye kazi, kamtangulize Mungu,’ baada ya hapo nikapewa ulinzi, nikaendelea kuchapa kazi.”
Rais Magufuli amesema, katika tukio hili, alimuona Mzee Mkapa ni mtu anayempa matumaini hata kama mtu amekata tamaa.
“Nimejifunza kutowasifu wateule wangu mimi, hatakama wanafanya kazi vizuri kwasababu yasije yakawapata yale yaliyonipata mimi baada ya wewe kunisifu. Nimeona niliseme hili kwa sababu halijazungumzwa popote,” amesema.
Leave a comment