July 29, 2021

Uhuru hauna Mipaka

‘Rais Magufuli ni mchochezi’

Spread the love

RAIS John Magufuli anatajwa kuwa ni rais mchochezi na anayefanya mambo yake ili kuonesha anaendesha mapambano dhidi ya wapinzani wake, anaandika Happyness Lidwino.

Dk. Azaveli Lwaitama, Mhadhiri wa Josiah Kibira University College (JOKUCO) amesema, yapo baadhi ya mambo ambayo Rais Magufuli amekuwa akiyafanya ili kukomoa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).

“Mfano, siku chache baada ya kumteua Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda aliongea kauli tata akaendelea na kauli hizo tata.

“Kuteuliwa kwa Makonda inatafsiri mpambano utakaokuwepo baina ya Meya mpya na yeye (Makonda) kwa kuwa, wanaoteuliwa na rais siku zote huwa wanajiona kuwa juu,” amesema Dk. Lwaitama.

“Hata Makonda nimemuacha Dar es Salaam ili wabaya wake wamuone akipanda cheo, wenye chuki wajinyonge zaidi,” amenukuliwa Rais Magufuli wakati akiweka jiwe la msingi la ujenzi wa kituo cha kufua umeme cha Kinyerezi namba mbili.

Amesema Dk. Lwaitama, Rais Magufuli anatakiwa kufanya kazi bila upendeleo kwa kuwa lengo ni kuwatumikia wananchi na si vinginevyo.

Dk. Lwaitama anasema hayo wakati Chama Cha Mapinduzi (CCM) kikilitumbikiza taifa kwenye sintofahamu ya kisiasa na kwamba, ni wakati wa wananchi kukataa utumwa,

Dk. Lwaitama anasema, wananachi wanapaswa kuondoka kwenye minyororo ya utumwa na kusimama katika kuhakikisha wanapigania haki pale inapoonekana kupokwa na watawala.

Anatoleo mfano ushindi wa vyama vinavyoundwana ukawa kuchukua Umeya wa Jiji la Dar es Salaam ambapo ndio Mji Mkuu wa Kibiashara Tanzania na kwamba, hatua hiyo inaanza kufungua minyororo.

“Wananchi wanatakiwa kujiandaa kimabadiliko na kuukataa utumwa kwani kwa muda mrefu walikuwa utumwani kwa kuongozwa na chama kimoja,” anasema Dk. Lwaitama.

Anasema, wananchi wa Dar es Salaam amekuwa wakijiuliza sababu za kughairishwa uchaguzi huo mara kwa mara “yote hii ni kwa sababu CCM inang’ang’ania madaraka.”

Akizungumza na mtandao huu leo Dk. Lwaitama anasema jeuri ya watawala wa nchi hii inatokana na ubovu wa Katiba na kwamba, udhaifu huo unakwenda mbali ikiwa ni pamoja na kuteua viongozi wabovu.

Miongoni mwa viongozi anaowaona kutokuwa na mantiki ya kuwepo kwao licha ya rais kuwa na mamlaka ya kuwateua ni pamoja na Wakuu wa Mikoa.

“Binafsi sioni kama kunahaja ya kuwa na wakuu wa mikoa wala wakuu wa wilaya kwani hao wanaonekana kuwepo kwa ajili ya kujitengenezea ulaji tu.

“Lakini kazi kubwa inatakiwa ifanywe na Meya wa Jiji ambaye ni mchaguliwa wa wananchi kwa kupitia madiwani.”

Dk. Lwaitama anasema, “Inatakiwa tukubali kurudi katika Katiba ya Warioba ili kuondoa mfumo huu wa kuwa na viongozi wengi ndani ya mkoa mmoja.

“Tunatakiwa kubaki na Mkurugenzi wa Jiji na Meya wa jiji tu ambaye amebeba ndoto za wananchi na sio Mkuu wa Mkoa ambaye ameteuliwa tu.”

error: Content is protected !!