Monday , 22 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Rais Magufuli: Mtoto akipata mimba asirudi shule
Habari za SiasaRipoti

Rais Magufuli: Mtoto akipata mimba asirudi shule

Rais John Magufuli
Spread the love

RAIS John Magufuli amepiga marufuku wanafunzi wa kike wanaopata ujauzito wakiwa shuleni, kurejea na kuendelea na masomo baada ya kujifungua, anaandika Saed Kubenea.

Akihutubia mamia ya wananchi katika mji wa Bagamoyo, mkoani Pwani, Alhamisi iliyopita, rais alisema ndani ya utawala wake, hakuna mwanafunzi aliyepata ujauzito atakayeruhusiwa kurudi shuleni.

Amesema, “siwezi kufanya kazi ya kusomesha wazazi. Hata kama ni mtoto wangu, siwezi kumfundisha. Hilo haliwezi kutokea ndani ya utawala wangu. Sikumpeleka mtoto shule ili apate mimba.”

Rais alikuwa akijibu taasisi zisizo za kiserikali (NGOs), zinazotaka serikali kuwaruhusu wanafunzi wanaopata mimba kurejea shuleni.

Alisema, “wakati mwingine ukizisikiliza hizo NGOs utaona zinataka kulipeleka taifa kubaya. Ndani ya utawala wangu haitotokea. Never (asilani!).

“Kama hizi NGOs zinawapenda sana hao watoto, zikafungue shule zao na kusomesha hao wazazi. Ndani ya utawala wangu, hakuna mwanafunzi yeyote mwenye mtoto atakayeruhusiwa kurudi shuleni. Serikali inatoa elimu kwa watoto, siyo kwa wazazi.”

Akiongea kwa sauti ya ukali, rais alisema, “hawa wanaotuletea haya mambo, hawatupendi ndugu zangu. Wametuletea dawa za kulevya, wameleta ushoga ambao hata ng’ombe hawana. Huku kuigaiga tutakuja kuiga mambo ambayo hata hayafai.”

Ametaka wanafunzi wanaopata mimba shuleni kujiunga na vyuo vya ufundi stadi (VETA).

Rais ametoa kauli hiyo wakati wa uzinduzi wa barabara yenye urefu wa kilomita 63 inayotoka Bagamoyo kwenda Msata. Tujadili:

Kwanza, watoto wenye umri mdogo wanapata ujauzito siyo kwa hiari. Wanatumbikizwa na vishawishi vya umasikini.

Serikali haina shule karibu na maeneo wanakoishi wazazi. Wanafunzi wengi wanalazimika kubebwa na wenye baiskeli na bodaboda, kutokana na umbali wa shule wanazosoma na wanakoishi.

Wanapita kwenye vichaka. Wanabakwa. Katika shule wanazosoma hakuna chakula. Kuna uhaba mkubwa wa vitabu vya kiada na ziada. Hakuna vifaa vya kufundishia; wanaombaomba na wenye navyo wanatumia udhaifu wao.

Hili haliwezi kuwa tatizo dogo. Ni tatizo kubwa mno. Limeelezwa katika ripoti mbalimbali za kitafiti, kuwa mimba za utotoni ni moja ya matatizo makubwa yanayosababisha wasichana wengi kushindwa kumaliza masomo yao.

Mathalani, shirika la kimataifa la Human Right Watch limeeleza katika ripoti yake ya mwaka 2016, kuwa asilimia 40 ya wanafunzi nchini hukatisha masomo yao sekondari kutokana na kupata ujauzito.

Ripoti ya shirika hilo imepewa kichwa cha maneno kisemacho: “Nilikuwa na ndoto za kumaliza shule.” Ripoti imeeleza kwa mapana kuwa katika mwaka huo, wasichana zaidi ya 8,000 (elfu nane), waliacha masomo baada ya kupata ujauzito au kuolewa kwa nguvu.

Katika mkoa wa Ruvuma pakee, ripoti imeeleza “takribani watoto 16 wa shule za msingi na 148 wa sekondari walikatisha masomo kwa sababu ya kupata ujauzito kati ya mwaka 2013 na 2014.”

Mkoani Tanga, takribani wasichana 300 waliacha shule. Mkoani Kagera watoto takribani 880 wameacha shule na mkoani Pwani wasichana 500 wamekatisha masomo kwa sababu hiyo. Haya yalitokea katika mwaka 2009 pekee.

Miongoni mwa sababu zilizotajwa ni kuongezeka kwa umasikini. Kwamba wanafunzi wanakwenda shule, lakini wakiwa hawajui watakula nini. Hawajui watakachokula warudipo nyumbani. Hawajui watakavyoweza kurejea nyumbani. Hawajui watakavyolipa ada zao za shule. Hawajui.

Hawana uhakika wakimaliza masomo yao watakwenda wapi? Nani atawalipia masomo yao ya kidato cha tano hadi sita; au chuo kikuu. Hawajui. Wanaishia kunaswa na vishawishi.

Huo ndio msingi wa kuwapo kesi nyingi za ubakaji. Serikali inajua hili na rais anafahamu kuwa serikali yake haijaweka utaratibu wa kusimamia kwa makini tatizo la ubakaji; na wala haijaweka utaratibu wa kumsaidia mwanafunzi aliyepata ujauzito shuleni – kulea mtoto na kuendelea na masomo.

Inaishia kutoa matamko yanayoweza kuangamiza maisha ya wasichana, mimba au watoto wao; na kuangamiza pia tamaa yao ya kuendelea na masomo.

Pili, kilichosemwa na rais ni tofauti na kinachohubiriwa na chama chake – Chama Cha Mapinduzi (CCM). Ni tofauti na kinachoelezwa ndani ya Ilani ya chama hicho iliyopelekwa kwa wananchi katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.

Kinachoelezwa na rais ni tofauti na kile kinachosemwa na baadhi ya viongozi wake wakuu, akiwamo makamu wa rais, Samia Suluhu; waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Ummy Mwalimu, baadhi ya naibu mawaziri na wakurugenzi katika wizara za serikali.

Kwa mfano, Ilani ya Uchaguzi ya CCM inasema kuwa “wasichana wote wa elimu ya msingi, wanaoacha shule kwa sababu ya kupata ujauzito, wataendelea na masomo yao mara wanapojifungua.” John Pombe Magufuli anasema “Hapana!”

Inasema, serikali itakayoundwa na chama hicho baada ya kumalizika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, itaweka utaratibu wa kuwezesha wanafunzi wanaopata ujauzito kuendelea na masomo. John Pombe Magufuli anasema “Hapana!”

Rais anasema, “…hakuna anayepata mimba ambaye ataruhusiwa kuendelea na masomo.” Anasema, “serikali inasomesha wanafunzi, haisomeshi wazazi.”

Hii ni tofauti na anavyoeleza makamu wake. Yeye amenukuliwa na gazeti la The Citizen la tarehe 6 Juni 2017 akisema, “…serikali inaelekeza wasichana wanaojifungua kurudi shuleni na kuendelea na masomo.” John Pombe Magufuli anasema “Hapana!”

Naye waziri Ummy amenukuliwa akisema, “…serikali imeamua kuwa wanafunzi wa kike wanaopata mimba wakiwa shuleni wasifukuzwe, bali waendelee na masomo.” John Pombe Magufuli anasema “Hapana!”

Alitoa kauli hiyo, tarehe 27 Aprili 2017 akiwa Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu (DUCE), Chang’ombe, Dar es Salaam.

Mkurugenzi wa Elimu ya Sekondari, Wizara ya Elimu, Paulina Mkonongo, ameeleza kuwa serikali imeweka dira inayowezesha wasichana kuendelea na masomo baada ya kujifungua.

Mkonongo alitoa kauli hiyo, tarehe 1 Desemba 2015 – wiki sita baada ya kumalizika uchaguzi mkuu wa rais, wabunge na madiwani. John Pombe Magufuli anasema “Hapana!”

Kwa muktadha huo, ni hoja dhaifu mno kudai kuwa mwanafunzi aliyebeba mimba akiwa shuleni, anaporuhusiwa kuendelea na masomo, hujenga picha mbaya kwa wanafunzi wenzake.

Hapa, madai kwamba mtoto anayepata mimba wakati akiwa shuleni amevunja kanuni na maadili ambayo hayaruhusu wanafunzi kujiingiza katika uhusiano wa kimapenzi, siyo sahihi.

Siyo sahihi pia kujenga ukuta kwa mwanafunzi aliyepata mimba, kwa kuwa mimba si mwisho wa maisha. Kuna maisha baada ya mwanafunzi kujifungua.

Aidha, siyo sahihi kuelekeza watoto wanaopata mimba kwenda kujiunga na vyuo vya VETA. Ni kwa sababu, katika vyuo hivyo vya ufundi hawaruhusu mtoto ambaye hajamaliza kidato cha nne.

Kwa maneno mengine, kutaka wanaopata ujauzito baadaye kujiunga na VETA, ni sawa na kuwaambia, “hamruhusiwi kupata elimu ya msingi, sekondari wala Veta.” Lakini sheria iliyounda VETA nayo haijabadilika kuruhusu kile ambacho rais anataka.

Wala haitakuwa sahihi serikali kuamini kila mtoto aliyepata ujauzito “amefanya uhuni;” au anastahili kuadhibiwa na kutengwa. Wengine hawakutaka kuwa na ujauzito. Wamelazimishwa na mazingira. Wamebakwa. Wameponzwa na umasikini walionao.

Si hivyo tu: Hatua ya serikali ya kuzuia mwanafunzi aliyejifungua kuendelea na masomo ina mfanya binti kugeuka mama lishe ili aweze kulea motto au awe ombaomba kwa kuwa mzazi mwenzie amefungwa gerezani miaka 30!

Ni vema Rais Magufuli akaacha kumwangalia binti huyu katika umri wake wa miaka 16, 17 hadi 20 aliyonayo wakati anapata mimba. Amwangalie maisha yake ya miaka 65 ijayo.

Tatu, kuzuia watoto waliopata ujauzito kuendelea na masomo baada ya kujifungua ni kukiuka mikataba ya kimataifa na Katiba ya Jamhuri.

Ibara ya 13 (2) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano, inapiga marufuku kutungwa sheria yoyote na mamlaka yoyote kuweka sharti lolote ambalo limesheheni vimelea vya “ubaguzi ama wa dhahiri au kwa taathira yake.”

Sera ya Elimu na Mafunzo” – Education and Training Policy (ETP) – ya mwaka 2014, inataka kuwapo usawa katika utoaji wa elimu nchini. Inaelekeza kila msichana kupata elimu kutokana na uwezo wake; na siyo kama serikali inavyotaka.

Muongozo wa elimu unazungumzia mfumo wa kisheria, taratibu zinazowezesha msichana wa shule aliyepata ujauzito kurudi shule baada ya kujifungua na mpango wa utekelezaji. Unataja hata mikakati ya ufuatiliaji na tathmini na kupima kile kilichokusudiwa.

Ndani ya sera hiyo, kumetungwa hata muongozo unaoweka sharti kwa serikali kuhakikisha kila msichana anayepata ujauzito anaruhusiwa kuendelea na masomo yake, mara anapojifungua. Lengo hapa ni pamoja na kuongeza mahudhurio ya wanafunzi mashuleni na kusaidia wasichana “kutimiza ndoto zao.”

Kumzuia mwanafunzi basi aliyepata ujauzito kuendelea na masomo, hakumkomoi yeye peke yake; na au hakuwezi kukomesha kile ambacho rais ameita mchezo “mtamu.”

Hii ni kwa sababu, zaidi ya asilimia 70 ya wananchi wanaishi vijijini na asilimia 39 wamo katika umaskini uliokithiri. Tunayodai kuyakataa yataendelea kuwepo tu maana kiini hakijaondolewa.

Hawajui maana ya elimu wala umuhimu wake. Hawajui madhara yake. Hawajui athari za mimba za utotoni – kupoteza fursa za maendeleo – na kumuweka katika hatari ya kuonewa au kudhalilishwa. Hawajui!

Hawajui madhara ya kupata mimba katika umri mdogo. Matatizo ya kiafya, yakiwamo magonjwa ya zinaa na vifo. Mengine, ni mhusika kujiingiza katika matumizi ya dawa ya kulevya, kupata mihemko, mfadhaiko na kujihisi kutokuwa na thamani.

Yapo hata matatizo ya kudharaulika kiakili; kudumaza maendeleo na wazimu usiotibika unaotokana na mhusika kujiona anaonewa au anatengwa.

Kuna madhara mengi kwa mtoto wa kike kupata mimba akiwa na umri mdogo; na au bila kupanga. Haya pekee ni mzigo mkubwa na mzito kwa mtoto wa kike.

Hakuna haja ya kumwongezea mzigo na huzuni. Wakati sheria na taratibu zinaimarishwa kuzuia mtoto wa kike kubakwa; yule ambaye tayari ni mateka aibuliwe kutoka mazingira magumu ambamo amesokomezwa.

Mtoto wa kike aliyejifungua arudi darasani. Asiporudi darasani hawi mzigo kwake peke yake, bali kwa taifa zima. Hivyo ndivyo ilivyo; tutake tusitake.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Mipango na uwekezaji kutumia bilioni 121.3, mradi wa Bagamoyo wapewa kipaumbele

Spread the loveWIZARA ya Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, imeliomba Bunge...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Mbunge ataka kasi uzalishaji walimu ipunguzwe akidai hakuna ajira

Spread the loveMBUNGE wa Mlalo (CCM), Rashid Shangazi, ameishauri Serikali ipunguze kasi...

ElimuHabari za Siasa

MbungeCCM ataka kasi uzalishaji walimu ipunguzwe akidai hakuna ajira

Spread the love  MBUNGE wa Mlalo (CCM), Rashid Shangazi, ameishauri Serikali ipunguze...

Habari za Siasa

Makamba ataja maeneo ya kuboresha mambo ya nje

Spread the love  WAZIRI wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika...

error: Content is protected !!