Wednesday , 6 December 2023
Home Habari Mchanganyiko Rais Magufuli: Mkapa aligoma kuzikwa Dodoma 
Habari Mchanganyiko

Rais Magufuli: Mkapa aligoma kuzikwa Dodoma 

Spread the love

RAIS wa Tanzania, John Pombe Magufuli amesema Hayati Benjamin William Mkapa, Rais mstaafu wa awamu ya tatu wa Tanzania, alikataa kuzikwa katika eneo la makaburi ya viongozi wa Serikali lililopo jijini Dodoma. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam…(endelea).

Rais Magufuli amesema hayo leo Jumatano tarehe 29 Julai 2020, katika mazishi ya mwili wa Mkapa, kijijini Lupaso mkoani Mtwara.

Mzee Mkapa alifariki dunia kwa mshtuko wa moyo Alhamisi tarehe 23 Julai 2020 saa 3:30 usiku jijini Dar es Salaam na mwili wake uliagwa kwa siku tatu mfululizo kwenye Uwanja wa Uhuru  jijini humo, kuanzia Jumapili hadi Jumanne tarehe 28 Julai 2020.

Akizungumza katika mazishi hayo, Rais Magufuli amesema, Serikali ilipanga sehemu ya maziko ya viongozi kuwa jijini Dodoma kwa kuwa ndio makao makuu ya nchi.

Hata hivyo, Rais Magufuli anasema Mzee Mkapa alikataa kuzikwa huko na kuagiza atakapofariki azikwe kijijini kwao Lupaso mkoani Mtwara.

“Nataka niseme kitu kimoja, Serikali ilipanga mahali pa maziko kwa viongozi na tulipangiwa kuwa tunazikwa Dodoma sababu ndio makao makuu ya nchi, miaka miwili mitatu Mzee Mkapa akaniuliza mlipanga maziko yawe Dodoma?” amesema Rais Magufuli.

Rais Magufuli ameeleza zaidi, “Mzee Mkapa alisema mimi msinizike Dodoma, nikasema wewe unataka uzikwe wapi akasema Lupaso.”

Rais Magufuli amesema, hata Rais mstaafu wa awamu ya nne wa Tanzania alipomuuliza juu ya suala hilo, alisema anataka kuzikwa kijijini kwao Msoga mkoani Pwani.

“Nikamuuliza Mzee Kikwete akasema mimi Msoga, nikaogopa kumuuliza Mzee Ali Hassan Mwinyi sababu alikuwa na miaka 90 na kitu, nikaona nikimuuliza likatokea la kutokea itaonekana uchuro, lakini dhamira yangu nikasema nitazikwa Chato,” amesema Rais Magufuli.

Akizungumzia mazishi ya Mzee Mkapa, Rais Magufuli amewashukuru viongozi wa dini, Serikali na Watanzania kwa kushiriki kikamilifu kuupumzisha mwili wa kiongozi huyo mstaafu katika makazi yake ya milele.

“Tumekuja hapa kwa kazi moja ya kumuaga Mzee wetu Benjamin Mkapa ambaye ametimiza kazi yake kwa miaka 82, nipende kwa mara nyingine kuwashukuru Watanzania wote mahali pote walipo, lakini kuwashukuru sana viongozi wetu wa dini zote,” amesema Rais Magufuli

“Ambao wameshiriki kikamilifu katika kumuombea Mzee Mkapa ili aweze kumpumzika kwa amani, niwashukuru waombolezaji wote na walioshiriki kutoka maeneo mbalimbali kumsindikiza safari yake.”

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari Mchanganyiko

Shura ya Maimamu kukata rufaa kupinga Sheikh kufungwa miaka 7

Spread the loveSHURA ya Maimamu Tanzania, inakusudia kukata rufaa dhidi ya hukumu...

Habari Mchanganyiko

TMA yaagizwa kutangaza mafanikio yao kikanda, kimataifa

Spread the love  KATIBU Mkuu Wizara ya Uchukuzi, Prof. Godius Kahyarara ameiagiza...

Habari Mchanganyiko

NMB yasaidia waathirika wa mafuriko, maporomoko Hanang

Spread the loveWaathirika wa maporomoko ya tope Wilayani Hanang, mkoani Manyara, waliopoteza...

Habari Mchanganyiko

TPF-NET Arusha yaonya jamii ya wafugaji zinazoendeleza ukatili wa watoto na wanawake

Spread the love  MTANDAO wa Polisi wanawake wa Arusha kuelekea siku 12...

error: Content is protected !!