August 13, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Rais Magufuli mambo hadharani

Spread the love

 

KASHFA zimeanza kumiminika baada ya Dk. John Magufuli wakati akiwa Waziri wa Ujenzi katika Serikali ya Awamu ya Nne kudaiwa kuridhia ununuzi wa Kivuko cha Mv. Dar es Salaam feki na kibovu, anaandika Faki Sosi.

Manunuzi ya kivuko hicho kibovu, feki yalifanywa na Wakala wa Ufundi Umeme (TAMESA) na kugharimu Dola za Marekani 4,980,000 sawa na Sh. 7.916 Bil.

James Mbatia, Msemaji wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni katika Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano amesema hayo wakati akisoma hotuba yake jana bungeni. Ifuatayo ni sehemu ya hotuba hiyo;

UFISADI KATIKA VIVUKO NA MADARAJA NCHINI

3.2.1.Ununuzi wa Kivuko Kibovu cha Dar es Salaam -Bagamoyo

Mheshimiwa Spika, Kivuko kutoka Dar es Salaam kwenda Bagamoyo ni jipu ambalo limeiva kwa viwango vyote na sasa linatakiwa litumbuliwe mara moja.

Ni dhahiri kuwa Kivuko cha Dar es Salaam kwenda Bagamoyo kilichonunuliwa na TEMESA chini ya uongozi wa waziri wa Ujenzi wa serikali ya awamu ya nne ambaye ndiye Rais wa Tanzania wa sasa.

Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) katika Hesabu za Serikali kuu akikagua Taarifa za fedha kwa mwaka ulioishia tarehe 30 Juni 2015 iliyotolewa mwezi Machi 2016 (Ukurasa wa 132 na 133), alibaini ununuzi wa boti feki na mbovu uliofanywa na TEMESA na kugharimu Dola za Marekani 4,980,000 sawa na shilingi 7,916,955,000 kupitia mkataba namba AE/006/2012-13/HQ/G/CN-39 uliosainiwa tarehe 25 April 2013 kati ya TEMESA kwa niaba ya Serikali na Mzabuni M/s Johs.Gram-Hanssen Bergensgade.

Mheshimiwa Spika, CAG alibaini masuala makuu mawili kuhusu ununuzi huo wa kivuko feki na kibovu cha Dar es Salaam – Bagamoyo.

Jambo la kwanza CAG alibaini kasi ya kivuko hicho ni tofauti na kasi iliyotakiwa kuwepo, jambo la pili ni kuwa cheti cha kukikubali kivuko hicho kilikuwa hakijatolewa kinyume na Kanuni ya 247 ya Manunuzi ya Umma.

Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inahoji, tabibu wa kutumbua jipu hili yuko wapi? Au msemo usemao kuwa“mganga hajigangi” unatumika hapa?

 

error: Content is protected !!