August 13, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Rais Magufuli kumvua nguo Kikwete

Spread the love

SERIKALI ya Rais John Magufuli muda wowote kuanzia sasa inaweza kukamata maofisa waliofanya kazi na Rais Jakaya Kikwete na kuwaburuza kortini, anaandika Happyness Lidwino.

Mkakati huo unaelekea kukamilika baada ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kufanya ukaguzi na kujiridhisha kwamba maofisa 156 wanapaswa kufikishwa mahakamani.

Kati ya maofisa hao 156 kesi kubwa zinatajwa kuwa 98 ambapo majalada 17 tayari yamepelekwa Biswalo Mganga, Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DPP) ili kupata kibali cha kuwaburuza mahakamani.

Takukuru kwa sasa wanasubiri kibali kutoka katika Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka ili kuchukua hatua hiyo. Maofisa hao ni wale waliofanya kazi na Rais Kikwete.

Kabla ya kubaini idadi ya maofisa hao wanaopaswa kufikishwa mahakamani, Takukuru ilifanya ukaguzi 296 ambapo jumla ya majalada 252 yaliyofikishwa kwa DPP huku maofisa 156 pekee ndio walioonekana kuwa na sababu ya kufikishwa mahakamani.

Hatua hiyo imebainika katika Kikao cha Kamati ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kilichokaliwa tarehe 16 Machi mwaka huu ambapo Valentino Mlowola, Mkurugenzi wa Takukuru alieleza kuwa, kinachosubiriwa kwa sasa ni vibali.

Ukaguzi huo umefanyika katika kipindi cha miezi saba kuanzia Julai mwaka jana hadi Januari mwaka huu.

Taarifa ya Mlowola kwa kamati hiyo ambayo mtandao huu inayo inaeleza kuwa, tayari kesi mpya zimefunguliwa 208 katika mahakama mbalimbali nchini huku kesi 113 watuhumiwa wake walipatikana na hatia.

Rais Magufuli wakati na baada ya kampeni za Uchaguzi Mkuu wa tarehe 25 Oktoba mwaka jana amekuwa akihubiri kuwachukuliwa hatua wabadhirifu wa fedha.

Tayari maofisa kadhaa waliofanya kazi na Rais Kikwete ama kuteuliwa wamefikishwa mahakamani kutokana na tuhuma za ufisadi hata hivyo, mkakati zaidi uliopo ni kuhakikisha maofisa wengine wanapelekwa kujibu tuhuma hizo ikiwa ni sehemu ya ahadi ya Rais Magufuli kwa wananchi wake.

error: Content is protected !!