Thursday , 25 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Rais Magufuli: Hatuchukii kukosolewa, ila kosoeni kwa staha
Habari za SiasaTangulizi

Rais Magufuli: Hatuchukii kukosolewa, ila kosoeni kwa staha

Spread the love

 

RAIS wa Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli amesema, serikali yake haikasirishwi na vyombo vya habari vinavyoikosoa, lakini ukosoaji huo, ni sharti uwe wa staha. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Ametoa kauli hiyo, leo Alhamisi, tarehe 25 Februari 2021, katika viwanja vya Mnazi Mmoja, jijini Dar es Salaam, wakati alipokuwa akizindua jengo la kituo cha televisheni cha Chanel Ten.
Kituo hicho kwa sasa, kinamilikiwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM), baada ya waliokuwa wamiliki wa wake wa awali, kujiondoa na kukabidhi hisa zao kwa chama hicho tawala.

Alisema, “serikali haichukii wanaotupa changamoto na kutukosoa kwa staha. Kitakwimu, tumeruhusu vyombo vingi sana vya habari katika kipindi hiki, kuliko wakati wowote tangu tupate Uhuru.”

Amesema, kwa sasa ndani ya Tanzania uzalendo umepungua hivyo kumekuwa kukiandikwa kila kitu, hata yale yasiyofaa kutokana na kuwepo uhuru wa kuandika.

Amedai kuwa katika baadhi ya mataifa kumewepo na mambo ya ajabu, lakini mambo hayo huwezi kuyaona kwenye vyombo vya habari.

“Uzalendo umepungua, niwaombe Watanzania na wahabari wote, tutangulize uzalendo wa nchi yetu. Yapo mataifa yanatokea mambo ya ajabu sana katika maeneo yao, lakini huwezi kusikia yameandikwa au kuwekwa katika mitandao.

“Lakini sisi tumekuwa wepesi kwa sababu ya uhuru huu. Kila kitu, hata kile ambacho hakifai, kinaandikwa,” ameeleza.

Amesema, katika uongozi wake kumekuwepo na ongezeko kubwa la vyombo vya habari, jambo ambalo limeifanya Tanzania kuongoza Afrika Mashariki na duniani.

“Katika miaka mitano iliyopita, serikali imeimarisha ipasavyo haki na wajibu wa vyombo vya habari, na kuhakikisha vinatoa haki na kuthamini suala la kutoa haki katika mambo ya habari.

Ameongeza kuwa “mwaka 2015, kulikuwa na vituo vya redio 106 tu katika nchi nzima, lakini hadi mwezi Februari 2021, tuna vituo vya redio 193.”

Amesema, mwaka 2015, kulikuwa na televisheni 25, lakini sasa kuna vituo vya televisheni 46.

“Serikali imeshasajili redio 23 na televisheni 440, zinazotumika mtandaoni kutoka sifuri mwaka 2015. Sheria ya huduma za habari ilipopitishwa, serikali imetoa leseni za magazeti ya kila siku, kila wiki na mwezi yanayofikia 247.

Kwa mujibu wa Rais Magufuli, “rekodi hii, inaifanya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi zenye vyombo vya habari vingi zaidi katika Afrika na duniani.”

Gazeti la MwanaHALISI
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Hali Halisi Publishers, Saed Kubenea akionyesha moja ya toleo la gazeti la MwanaHALISI wakati likiwa linachapishwa

Kiongozi huyo amesema, pamoja na vyombo vya habari kuhitajika, lakini ni vizuri kutanguliza uzalendo kwa kuwa ni kitu muhimu huku akieleza kukerwa na taarifa za “kushabikia vifo.”

Amesema, “…uzalendo ni kitu muhimu sana, kitu muhimu kingine ni haki ya yule anayeandikiwa habari. Pamekuwa na habari nyingi za uzushi zinatolewa; mara fulani kafa, nani kafa, vigogo wafa, vigogo wapukutika. Ni mambo ya ajabu.

“Tumefikia sisi Watanzania tunaombeana kufa, ni upendo wa ajabu. Lakini pia katika taarifa taifa letu linachafuliwa, unakuta watu kabisa bila kujali, nao wanashabikia,” amesema.

Hata hivyo, wakati Rais Magufuli anasema, kwa ujumla vyombo vya habari vimeongezeka, lakini ni katika kipindi chake, magazeti, radio na televisheni kadhaa zimefungwa na nyingine kutozwa faini ya mamilioni ya shilingi.

Miongoni mwa magazeti yaliyofungwa, ni pamoja na gazeti la kila wiki la MwanaHALISI, ambalo pamoja na kushinda kesi mahakama ya rufaa na kumaliza adhabu yake ya miaka mitatu, bado limenyimwa leseni.

 

Magazeti mengine ambayo yamefungiwa na baadaye kwenda mahakamani kulalamika na kisha kushinda kesi, lakini mpaka sasa, bado hayajapewa leseni ya uchapishaji, ni Mseto na Mawio.

Gazeti jingine ambalo limeondolewa sokoni na serikali, ni Tanzania Daima.  Gazeti hilo la kila siku na ambalo linamilikiwa na mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, lilifungiwa tarehe 20 Juni mwaka jana.

Katika taarifa yake, serikali kupitia Idara ya Habari – Maelezo – ilisema, imepiga marufuku gazeti la Tanzania Daima kuchapishwa na kusambazwa popote nchini au nje ya nchi, kufuatia uamuzi wa kusitishwa kwa leseni yake ya uchapishaji na usambazaji.

Serikali ilidai kuwa uamuzi huo, unatokana na kile ilichoita, “kukithiri na kujirudia,” kwa makosa yanayokiuka sheria za nchi na maadili ya uandishi wa habari.

”Juhudi za kuwaonya, kuwaelekeza na kuwakumbusha wahariri wa gazeti hilo, ili waweze kufuata masharti ya leseni waliyopewa kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa, zimeshindwa kuzaa matunda kutokana na ukaidi, ubishi, dharau kwa mamlaka za nchi na wakati fulani nia ovu ya dhahiri,” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.

Barua hiyo imesema, “kwa sababu hizo, kwa mamlaka niliyopewa chini ya kifungu cha 9(b) cha sheria ya Huduma za Habari Na.12 ya mwaka 2016, Mkurugenzi wa Idara ya Habari amefuta leseni ya gazeti hilo.”

Aidha, magazeti mengine kadhaa nchini yamefungwa kutokana na kushindwa kustahamili mazingira magumu ya uendeshaji, ikiwamo vitisho vya kufungiwa; na au kufutwa kutoka kwa baadhi ya wenye mamlaka.

Baadhi ya magazeti yalijifunga wenyewe, ni pamoja na magazeti yaliyokuwa yakichapishwa na kampuni ya New Habari 2006, ambayo ni Rai, Mtanzania, The African, Bingwa na Dimba.

Mhariri mtendaji wa magazeti hayo, Dennis Msacky, hakueleza sababu za kusitishwa kwa uzalishaji huo, bali aliishia kusema, “uzalishaji utasitishwa kuanzia Jumatatu, tarehe 7 Desemba 2020.”

Msacky alisema, usitishwaji wa uzalishaji utakwenda sambamba na upunguzaji wa wafanyakazi, ambapo mwaka 2019, kampuni ilipunguza wafanyakazi wake 150.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

Kilosa yawa mfano wa kuigwa miradi ya Mwenge nchini

Spread the love  KIONGOZI wa Mbio za Mwenge Kitaifa Godfrey Mzava amezitaka...

Habari za SiasaTangulizi

Biteko ataja vipaumbele 7 bajeti nishati 2024/25

Spread the love  NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Mwekezaji amwaga bil. 39 kujenga viwanda 3 vya uchenjuaji

Spread the loveKampuni ya Mineral Access System Limited (MAST) inayoiwakilishwa kampuni ya...

Habari za SiasaTangulizi

Mpwa wa Magufuli mbaroni kwa kusambaza picha za utupu

Spread the loveJESHI la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limewakamata...

error: Content is protected !!