August 16, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Rais Magufuli azua gumzo ziarani UDSM

Spread the love

ZIARA ya Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli kukitembelea Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) leo imezua gumzo, anaandika Charles William.

Ziara hiyo yenye lengo la kuweka jiwe la msingi katika uzinduzi wa ujenzi wa maktaba ya kisasa inayojengwa kwa ufadhili wa Serikali ya China, imesababisha kufutwa kwa ratiba ya masomo chuoni hapo kuanzia saa mbili mpaka saa nane mchana ili kuwapa nafasi wanafunzi na watumishi wa chuo hicho kusikiliza hotuba yake.

Tangazo ambalo limetolewa na Profesa Florens Luoga, Makamu Mkuu wa chuo hicho – utawala, limeeleza kuwa ziara ya Rais Magufuli itasitisha ratiba zote za chuo hicho kuanzia saa mbili asubuhi leo mpaka saa nane mchana huku tangazo lililotolewa na Serikali ya Wanafunzi likiwataka wanafunzi wa chuo hicho kwenda katika eneo la uwanja wa mpira wa chuo hicho  kuanzia saa nne asubuhi ili kumsubiri Rais Magufuli ambaye atazungumza na wanafunzi hao.

Eneo la uwanja wa mpira, ni eneo kubwa zaidi la wazi katika chuo hicho lakini lipo umbali wa mita zaidi ya 600 kutoka eneo la ujenzi wa maktaba ambapo ndipo Rais Magufuli alipotarajiwa kwenda kuweka jiwe la msingi kabla ya kwenda uwanjani hapo kutoa hotuba yake.

Itakumbukwa kuwa siku moja iliyopita wanafunzi wa UDSM walifanya mgomo wa siku moja Chuoni hapo wakishinikiza kupewa fedha zao za kujikimu ambazo zilikuwa zimechelewa kwa muda wa siku zaidi takribani 5 na hivyo kusababisha serikali ya wanafunzi (DARUSO) kupitia Rais wake Erasmi Leon na Makamu wake Mshangama Shamira kutangaza mgomo.

Taarifa za ndani ambazo bado hazijathibitishwa na chanzo chochote zinadai kuwa, hapo awali ziara hiyo ya Rais ilikuwa na lengo la kuweka jiwe la msingi katika ujenzi wa maktaba tu hata hivyo Rais Magufuli aliamua kuomba muda wa kuhutubia taifa kupitia wanafunzi wa Chuo kikuu cha Dar es salaam, pamoja na kusikiliza malalamiko na maoni ya wanafunzi wa chuo hicho kuhusu mambo mbalimbali yanayoendelea ndani na nje ya chuo hicho.

Kwa habari za hivi punde tayari Rais Magufuli amefika UDSM. Taarifa zaidi kuhusu ziara hiyo zitaendelea.

error: Content is protected !!