October 2, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Rais Magufuli awapa ujumbe wanaotaka kugombea uchaguzi mkuu

Spread the love

MWENYEKITI wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Rais John Pombe Magufuli, amewataka wanachama wa chama hicho, wenye nia ya kugombea nafasi mbalimbali za uongozi katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 2020, kujitathmini na kujiridhisha kama wanatosha kugombea nafasi wanazoomba. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea)

Rais Magufuli ameyasema hayo leo Jumatatu tarehe 1 Juni 2020 wakati akikagua maandalizi ya kumbi za mikutano na vikao vya chama vinavyotarajiwa kufanyika hivi karibuni.

Katika ukaguzi huo, Rais Magufuli ameongozana na Makamu Mwenyekiti wa CCM (Bara), Philip Mangula na Katibu Mkuu wa chama hicho, Bashiru Ally kukagua kumbi za Kituo cha Mikutano Dodoma (Jakaya Kikwete Hall) ambako utafanyika Mkutano Mkuu wa CCM na jengo la Ofisi za Makao Makuu ya CCM (White House).

Amesema, pamoja na kufanyika kwa mchakato wa uchaguzi ndani ya chama, Uchaguzi Mkuu lazima utakuwepo hivyo amewataka wanachama wote wenye nia ya kugombea nafasi mbalimbali za uongozi kujitathmini na kujiridhisha kama wanatosha kugombea nafasi wanazoomba.

Ameonya kuelekea katika mchakato huo, wanachama hawana budi kuweka mbele maslahi ya chama badala ya maslahi yao binafsi na pia kutofanya vitendo vya kuwagombanisha na fujo ambazo vitakavyokiumiza chama.

“Chama chetu kinayo demokrasia ya kutosha, lakini demokrasia hii ndani ya chama isije ikatumika kuleta fujo, kutugombanisha na kukiumiza chama, tuweke maslahi ya chama mbele na tutumie nafasi hii kukiimarisha chama chetu” amesema Rais Magufuli.

Rais Magufuli amewataka wana CCM kote nchini kutembea kifua mbele na kuyasema mambo yote ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM kwa wananchi, badala ya kuacha jukumu hilo kwa viongozi wachache.

error: Content is protected !!