August 13, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Rais Magufuli atumbua TCRA

Spread the love

RAIS John Magufuli amevunja Bodi ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) na kumsimamisha kazi Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo Dk. Ally Yahaya Simba kwa madai ya kushindwa kusimamia ipasavyo mkataba wa utekelezaji wa Mfumo wa Usimamizi Mfuko wa Mawasiliano (TTMS), anaandika Happiness Lidwino.

Katika taarifa iliyotolewa leo Jijini Dar es Salaam na Gerson Msigwa, Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu imeeleza kuwa, kushindwa kusimamia vizuri TTMS kunaiingizia nchi hasara ya zaidi ya Sh. 400 milioni kwa mwaka.

Rais Magufuli amechukua hatua hiyo baada ya kufanya kikao cha kazi kati ya viongozi na wataalamu kutoka Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi; Wizara ya Fedha na Mipango na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (Takukuru) .

Kikao kimebaini kuwa, tarehe 22 Machi 2013 TCRA iliingia mkataba na Kampuni ya SGS juu ya uwekaji na uendeshaji wa mapato ya simu ambapo kampuni hiyo ilipaswa kutekeleza vipengele vitano lakini mpaka sasa bado haijaanza.

Kampuni hiyo ilitakiwa kuanza na kipengele kidogo kinachohusu udhibiti wa mapato ya simu za ndani hali ambayo imesababisha serikali kukosa mapato hayo.

Rais Magufuli pamoja na kuvunja bodi hiyo inayoongozwa na Prof. Haji Semboja na kumsimamisha kazi Simba, pia amemuagiza Prof. Makame Mbarawa, Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi kumteua kaimu mkurugenzi wa mamlaka hiyo mara moja.

Rais Magufuli amewataka Waziri Mbarawa, Katibu na Naibu Katibu katika wizara hiyo kuchukua hatua mara moja ili mfumo wa ukusanyaji wa mapato ya simu za ndani uanze kufanya kazi, na nchi ipate mapoto yanayostahili kukusanywa.

“Waziri ahakikishe anachukua hatua mara moja nataka tukusanye mapato yote ya serikali yanayostahili na na sitasita kuchukua hatua dhidi ya yoyote atayekwamisha jambo hili ”amesisitiza magufuli katika taarifa hiyo.

error: Content is protected !!