September 27, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Rais Magufuli atuhumu AZAKI, NGO’s

Rais John Magufili, Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM)

Spread the love

RAIS John Magufuli ametuhumu baadhi ya asasi za kiraia (AZAKI) na mashirika yasiyo ya kiserikali (NGO’s), zinazofanya kazi ya ‘ukuadi.’ Anaripoti Mwandishi Wetu…(endelea).

Amesema, baadhi ya taasisi hizo zimekuwa zikifanya kazi ya kufifisha jitihada za maendeleo ya Tanzania, kwa manufaa ya mataifa ya nje.

Ametoa kauli hiyo leo tarehe 12 Desemba 2019, wakati akifungua Semina ya Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi (CCM), jijini Mwanza.

Amesema, wakati mwingine mataifa hayo hutumia baadhi ya AZAKI na NGO’s, kuhubiri demokrasia na haki za binadamu.

Na kwamba, wao huvunja misingi hiyo, kwa kujenga mifumo ya kinyonyaji, kuchochea machafuko pamoja na kuingilia uhuru wa mataifa mengine.

“Hivyo watatumia kila njia kufifisha jitijhada zetu na kupenyeza ajenda zao, wakati mwingine watatumia asasi za kiraia na mashirika yasiyo ya kiserikali na kujifanya wanatufundisha demokrasia na haki za binadamu,” amesema Rais Magufuli na kuongeza;

“Ilhali wao wenyewe wanavunja misingi hiyo, kwa kujenga mifumo ya kinyonyaji, kuchochea machafuko na kuingilia uhuru wa mataifa mengine.  Wakati mwingine watajenga mazingira ya taharuki, wanaweza wakakwambia una ebola na mengine mengi, ilimradi ionekane nchi haiko salama.”

Rais Magufuli ambaye ni Mwenyekiti wa CCM, ameeleza kuwa watu hao hawapendi kuona Tanzania inaendelea, ili iendelee kuwa tegemezi.

“Wasingependa hata tutoe elimu bure kwa watoto wetu, tupeleke umeme wa kutosha vijijini. Wangependa tuendelee kuwategemea wao, ilihali wao wanaishi kwa kutegemea rasilimali zetu,” amesema Rais Magufuli.

Rais Magufuli amewataka Watanzania kutambua ya kwamba, nchi iko katika mapito kuelekea ukombozi wa kiuchumi, hivyo wanapaswa kuwa imara na kujenga uzalendo.

“Inatupaswa kutambua haya ndio mapito yetu kuelekea ukombozi wa kiuchumi, na tusiposimama imara na kujenga uzalendo na moyo wa kujitolea kwa taifa. Hatuwezi kushinda, ni lazima tujitambue, tujue tulipo na tulipotoka,” amesisitiza Rais Magufuli.

Amesema, misaada inayotolewa na wafadhili wa nje ni ya kupumbaza “Hii miisaada tunayopata ni ya kutupambaza.”

error: Content is protected !!