October 2, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Rais Magufuli ateua RC, Katibu mkuu na DC Dodoma

Rais John Magufuli

Spread the love

RAIS wa Tanzania, John Pombe Magufuli amefanya uteuzi wa viongozi mbalimbali kama ifuatavyo akiwemo mkuu wa mkoa (RC), katibu mkuu na mkuu wa wilaya (DC). Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam…(endelea).

Taarifa iliyotolewa leo Ijumaa tarehe 17 Julai 2020 na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Gerson Msigwa imesema wateuliwa wote wataapishwa Jumatatu tarehe 20 Julai 2020 Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma.

Walioteuliwa, Kwanza, Rais Magufuli amemteua Dk. Jumanne Fhika kuwa Mkuu wa Mkoa wa Njombe.

Kabla ya uteuzi huo, Dk. Fhika alikuwa Ofisi ya Rais na anachukua nafasi ya Christopher Ole Sendeka.

Pili, Rais Magufuli amemteua Dk. Aloyce Nzuki kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii.

Kabla ya uteuzi huo, Dk. Nzuki alikuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii na anachukua nafasi ya Profesa Adolf Mkenda.

Tatu, Rais Magufuli amemteua Mhandisi Anthony Sanga kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji.

Kabla ya uteuzi huo, Mhandisi Sanga alikuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji na anachukua nafasi ya Profesa Kitila Alexander Mkumbo.

Soma zaidi hapa

Rais Magufuli awaapisha warithi wa Makonda, Mnyeti

Nne, Rais Magufuli amemteua Dk. Allan Kijazi kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii.

Dk. Kijazi anachukua nafasi ya Dk. Aloyce Nzuki aliyeteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, na pia Dk. Allan Kijazi ataendelea kuwa Kamishna wa Uhifadhi wa Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA).

Tano, Rais Magufuli amemteua Mhandisi Nadhifa Kemikimba kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji.

Kabla ya uteuzi huo, Mhandisi Nadhifa Kemikimba alikuwa Mkurugenzi katika Wizara ya Maji na anachukua nafasi ya Mhandisi Anthony Sanga ambaye ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji.

Soma zaidi hapa

JPM: Sijamtuma mtu akagombee, awapa ujumbe wanaCCM

Sita, Rais Magufuli amemteua Fadhili Mohamed Juma kuwa Mkuu wa Wilaya ya Geita Mkoani Geita.

Kabla ya uteuzi huo, Fadhili Mohamed Juma alikuwa Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Lindi na anachukua nafasi ya Josephat Paulo Maganga ambaye amehamishwa kituo cha kazi na kuwa Mkuu wa Wilaya ya Dodoma.

Josephat Paulo Maganga anachukua nafasi ya Patrobas Katambi.

error: Content is protected !!