RAIS John Magufuli amemteua Mhandisi, Julius Ndyamukama kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA). Anaripoti Regina Mkonde … (endelea).
Taarifa ya uteuzi huo imetolewa leo tarehe 26 Machi 2019 na Gerson Msigwa, Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu.
Taarifa ya Msigwa inaeleza kuwa, Mhandisi Ndyamukama anachukua nafasi ya Richard Mayongela ambaye uteuzi wake umetenguliwa na Rais Magufuli, na kutakiwa kuripoti Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mwasiliano ambako atapangiwa kazi nyingine.
“Uteuzi wa Mhandisi Ndyamukama unaanza leo tarehe 26 Machi 2019,” inaeleza sehemu ya taarifa ya Msigwa.
Kabla ya uteuzi huo Mhandisi Ndyamukama alikuwa Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) mkoani Dar es Salaam.
“Ndiye alikuwa msimamizi mkuu wa ujenzi wa majengo namba 3 (Terminal 3) ya uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam ambayo yapo hatua za mwisho kukamilika,” inaeleza zaidi taarifa hiyo ya Msigwa.
Leave a comment