September 26, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Rais Magufuli ateta na vigogo wa CCM Ikulu

Spread the love

MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi, Rais John Pombe Magufuli amefanya kikao na viongozi waandamizi wa chama hicho akiwemo Rais wa Zanzibar, Ali Mohamed Shein. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam…(endelea).

Kikao hicho kimefanyikia Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma leo Jumatano tarehe 3 Juni 2020.

Katika kikao hicho, mbali na Shein ambaye ni Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi na Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar kimehudhuriwa na Makamu Mwenyekiti CCM Bara, Philip Mangula na Katibu Mkuu wa chama hicho, Bashiru Ally.

Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu ya Tanzania, Gerson Msigwa imesema, “viongozi hao wamezungumzia masuala ya CCM.”

Baada ya kikao hicho, Rais Shein amekwenda kuweka udongo katika jiwe la msingi la ujenzi wa Ofisi za Ikulu na kukagua maendeleo ya kazi ya ujenzi wa ofisi hizo inayofanywa na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kupitia shirika lake la Suma JKT.

Rais Shein amemshukuru Rais Magufuli kwa kumpa fursa ya kwenda kuweka udongo ikiwa ni kumbukumbu ya ujenzi wa ofisi hizo na amebainisha kujengwa kwa ofisi hiyo ni heshima kwa Taifa na tafsiri sahihi ya kujitawala.

“Huko ndio kujitawala, kutawaliwa sio kuzuri, mtawala anafanya anavyotaka yeye, anafanya kwa utashi wake pale anapotaka yeye kufanya, tunapochukua hatua ya kujitawala wenyewe tunafanya mambo makubwa kama haya kwa ajili ya wananchi, hii ofisi ni ya wananchi wa Tanzania,” amesema Rais Shein.

Rais Shein amewasalimu vijana wa JKT wanaofanya kazi za ujenzi wa ofisi hizo, amewapongeza kwa kazi nzuri wanayoifanya na amewataka kujivunia fursa hiyo adhimu ya kujenga ofisi ya Ikulu za nchi yao, badala ya kazi hiyo kufanywa na kampuni za nje ya nchi kama ambavyo hufanyika katika maeneo mengi.

error: Content is protected !!