August 16, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Rais Magufuli atajiwa ‘Muhujumu Uchumi’

Spread the love

 

SIKU moja baada ya Rais John Magufuli kuonya wafanyabaishara wa sukari wanaoficha bidhaa hiyo, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) imemtaja muhusika, anaandika Faki Sosi.

Valentino Mlowola, Mkurugenzi wa Takukuru anamtaja Haruni Zacharia, Mkurugenzi Mtendaji wa Al-Naeem, mfanyabiashara mwenye ghala la sukari Mbagala na Tabata jijini Dar es Salaam kuwa, ameficha tani 4,579.2 za sukari.

Jana akiwa katika Jimbo la Hanang’, Katesh mkoani Manyara akielekea Arusha, Rais Magufuli alitoa onyo kwamba, wafanyabiashara wanaochezea serikali yake kwa kuficha sukari, akiwabaini hawatafanya bishara tena tena nchini.

Alisema kuwa, wafanyabiashara wanaoficha sukari ni wahujumu uchumi ambapo aliagiza vyombo vya dola kufuatilie wote walioficha sukari.

Katika taarifa iliyotolewa na Mlowola leo imeeleza kuwa, uchunguzi uliofanywa, umebaini tani 4,579.2 zilikuwa zimefichwa na Zacharia kwenye ghala lake la Tabata na Mbagala.

Amesema, Takukuru imeanza uchunguzi zaidi kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi na kwamba, wamebaini mfanyabiashara huyo kuwa miongoni mwa wafanyabiashara wakubwa nchini  anayetuhumiwa kuficha sukari hiyo iliyonunuliwa kutoka katika Kiwanda cha Kilombero.

“Uchunguzi ulibaini kuwepo kwa njama za dhati za kutouza sukari kulikofanywa na mfanyabiashara huyu…” imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.

Amesema kuwa, uchunguzi uliofanyika umebaini kuwepo kwa mikakati ya dhati iliyokuwa ikifanywa na mfanyabiasha huyu kwa kununua sukari yote kutoka viwanda vya ndani na kisha kuihifadhi.

Lakini pia kuuza bidhaa hiyo kidogo kidogo kwa wastani wa tani 250 kwa siku ingawa alikuwa na uwezo wa kuuza zaidi jambo lililochangia uhaba wa sukari katika soko.

“Kuficha bidhaa ni kosa la uhujumu uchumi na ni  kinyume na Aya ya 3 ya Jedwali la kwanza Sheria ya Uhujumu Uchumi Sura ya 200 (Chapisho la Mwaka 2002).

“Serikali haitavumilia hujuma za namna hii na itachukua hatua kali dhidi ya mfanyabiashara yeyote ataekwenda kinyume na sheria hii,” imeeleza taarifa hiyo.

error: Content is protected !!