August 10, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Rais Magufuli asipotoshwe mali za Waislamu

Spread the love

RAIS John Pombe Magufuli, ameahidi kuwa serikali itarejesha “mali zote za waislamu” anazodai zimeporwa na wajanja wachache, anaandika Saed Kubenea.

Amesema kwa muda mrefu Waislamu wamelalamika kwamba mali zao zimeporwa na kwamba wote walioshiriki dhuluma hizo, atahakikisha wanazirejesha mali hizo.

Dk. Magufuli amesema alianza kuyafahamu matatizo ya Waislamu kuporwa mali zao wakati alipokuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.

Baadhi ya viongozi wa Bakwata walifika ofisini kwake kulalamikia uporaji huo. Amewashauri viongozi hao, kwa kutumia mawakili wao, kuhakikisha mali za Waislamu zinarejeshwa.

Kauli ya Dk. Magufuli kuwa atarejesha mali za Waislamu ilitokana na “ombi maalum” lililowasilishwa kwake na Katibu Mkuu wa Bakwata, Suleiman Lolila.

Akisoma risala hiyo mbele ya rais, Lolila aliomba serikali kusaidia Bakwata kurejesha mali zake ilizodai zimechukuliwa kinyume cha sheria.

Katibu huyo wa Bakwata alihoji: Yawezekana vipi kiwanja cha msikiti kikajengwa kituo cha mafuta?

Aidha, Rais Magufuli ameipongeza Bakwata, kwa kuwaunganisha Waislamu na kupanua wigo wa kutoa huduma kwa jamii.

Amesema kitendo cha Bakwata kuwaunganisha Waislamu wote katika Baraza la Eid el-Fitir, kinafungua ukurasa mpya kwa waumini wa dini hiyo na madhehebu mengine.

Kwa mujibu wa Rais Magufuli, hatua ya Waislamu kuungana katika baraza la Eid ni kielelezo cha kuimarika kwa umoja wao na mshikamano miongoni mwao.

Dk. Magufuli alitoa kauli hiyo Jumatano iliyopita, alipohutubia Baraza la EId el Fitr, katika viwanja vya Karimjee, jijini Dar es Salaam.

Mkutano wa Baraza la Eid uliotumiwa na rais kuahidi “kurejesha mali za Waislamu,” uliandaliwa na Bakwata. Ulihudhuriwa na watu mbalimbali, akiwamo Kassim Majaliwa, waziri mkuu.

Hata hivyo, kile ambacho rais amekieleza juu ya anachoita “kuporwa kwa mali za Waislamu,” ni tofauti na ukweli ambao jamii ya Kiislamu inaufahamu. Tujadili.

Kwanza, mali nyingi za Waislamu zinazodaiwa ama kuporwa, kuuzwa, kutapanywa au kugawanywa, zimefikishwa huko na viongozi wa Bakwata.

Hakuna kokote ambako kunaweza kusemwa kuwa mali hizi zimeuzwa na Wakristo, Wapagani, Wahindu au Wayahudi. Hakuna.

Baadhi ya mali hizo, zimeuzwa kwa wafanyabiashara wakubwa wanaotajwa kuwa waumini wa madhehebu ya Kiislamu. Ushahidi upo.

Kama rais alikuwa halifahamu jambo hili vizuri au ameelezwa tofauti, basi sasa anapaswa kuelezwa. Anapaswa kuambiwa kuwa mali za Waislamu zimeuzwa na madalali walioko ndani ya Bakwata.

Ni kwamba mali za Waislamu zilizokuwa chini ya taasisi ya East Africa Muslim Welfare Society (EAMWS), zimeuzwa na Bakwata kinyume na matakwa ya Waislamu.

Taasisi hii, iliyoundwa wakati wa Jumuia ya Afrika Mashariki iliyovunjika, ilikuwa ikimiliki nyumba, viwanja na mashamba na maeneo kadhaa ndani na nje ya nchi.

Kuuzwa kwa mali hizi kulitokana na hatua ya serikali kuamuru kuvunjwa kwa taasisi hii muhimu kwa Waislamu na kwa maslahi Yao.

Ni serikali iliyounda, kwa mlango wa nyumba, chombo kingine na kukipachika jina la “Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata).”

Taasisi ya EAMWS ilipigwa marufuku kwa tangazo la serikali, lililotolewa 19 Desemba 1968.

Viongozi wakuu wa EAMWS waliitwa mbele ya Kabidhi Mkuu Wasii wa Serikali ambaye alikabidhiwa na serikali, jukumu la kusimamia ufungaji wa taasisi hiyo na kukabidhi mali za EAMWS kwa Bakwata.

Serikali haikuishia kuwaundia Waislamu chombo cha kuwasimamia; ilikabidhi mali zao bila utashi wa viongozi wa EAMWS na bila kuwapo maandalizi.

Bakwata iliyokabidhiwa kazi ya kulinda na kuendeleza kazi na mali za Waislamu, haikuwa na mipango yoyote ya kusimamia na kuendesha mali ilizokabidhiwa.

Mipango yote ya kuendesha elimu, kusimamia afya na huduma nyingine za jamii, ikafifia na hatimaye kufa.

Waislamu waliokuwa mbioni kukamilisha ujenzi wa vyuo vikuu chini ya EAMWS, sasa kupitia Bakwata wameishia kumiliki shule za msingi, zahanati, vituo vya afya na shule za sekondari.

Shule nyingi za Bakwata zinaongoza kwa matokeo mabaya. Wakati Waislamu chini ya Bakwata wakiendelea kudorora kimaendeleo, madhehebu mengine ya kidini yanazidi kujiimarisha.

Baadhi yao tayari yanamiliki shule za sekondari zenye mafanikio makubwa; vyuo vikuu na hata hospitali za rufaa, ikiwamo Bugando iliyoko jijini Mwanza na KCMC iliyoko mkoani Kilimanjaro.

Pale walipojitokeza baadhi ya Waislamu kupinga Bakwata kukabidhiwa mali zao kwa mlango wa nyuma, serikali ilijiapiza kukabiliana na yeyote anayehubiri kurejeshwa kwa mali hizo.

Serikali ikakabiliana na wale wote waliokuwa wakidai mali za Waislamu zimekabidhiwa kwa Bakwata na kuuzwa kinyume cha matwaka yao.

Hicho ndicho chanzo cha mali za Waislamu kupotea. Ndiyo chanzo cha baadhi ya Waislamu kulalamikia Bakwata na kuituhumu kutetea dhuluma dhidi ya Waislamu.

Ndiyo chanzo cha tuhuma na shutuma kuwa serikali imegeuza Bakwata kuwa tawi lake. Hivyo basi, kuzirejesha mali hizo kwa madalali walewale, ni kutaka kuibua migogoro mipya ndani na nje ya baraza hilo.

Pili, hata pongezi alizomwaga rais juu ya Bakwata, kwamba “imewaunganisha Waislamu wote katika Baraza la Eid el-Fitr,” nazo hazikustahili.

Tangu baraza hili limeundwa, takribani miaka 50 iliyopita, halijaweza kuwaunganisha Waislamu. Limeishia kuwa baraza la kuwagawa Waislamu mmojammoja na kwa madhehebu yao.

Limeendelea kutuhumiwa kugombanisha baadhi ya Waislamu na serikali yao; baadhi ya Waislamu na viongozi wao wa kidini; na baadhi ya taasisi nyingine za dini na serikali yao.

Kwa maneno mengine, Bakwata imekuwa muhuri wa serikali, badala ya kuwa chombo kikuu cha Waislamu.

Mathalan, Bakwata imekuwa iikiunga mkono kila jambo ambalo linatendwa na serikali, hata kama linapingwa na jamii.

Mfano mmojawapo ni hatua ya baraza hili kufanya kazi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kubariki uchaguzi wa marudio Visiwani.

Bakwata na viongozi wake wameshindwa kukemea ukiukwaji wa sheria na katiba kwa kufuta uchaguzi mkuu huru na haki wa 25 Oktoba 2015. Walipongeza.

Wamebariki kitendo cha serikali na CCM cha kuchakachua maoni ya wananchi yaliyokusanywa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba chini ya Jaji Joseph Sinde Warioba. Ni tofauti na msimamo wa taasisi nyingine za kidini. Ushahidi upo.

Lakini ukiacha hilo, kuna hili jingine. Rais anayeahidi kurejesha mali za Waislamu hajaeleza hatua alizochukua kushughulikia malalamiko ya Waislamu yaliyofikishwa mezani kwake wakati akiwa waziri wa ujenzi.

Ameishia kusema, “nawashauri Bakwata kuwatumia mawakili mlionao pamoja na viongozi wa madhehebu mengine, kuhakikisha mnakomboa mali za taasisi zenu….”Basi!

Wala hakuna rekodi yeyote inayoeleza kuwa akiwa waziri wa ujenzi, Dk. Magufuli aliwahi kushughulikia mgogoro unaohusu mali za Waislamu. Hakuna.

Wala hakuna mahali kulikoelezwa, kwamba juhudi za rais za kukwamua mali za Waislamu zilikwamishwa na aliyekuwa bosi wake, Jakaya Mrisho Kikwete. Hakuna.

Kile ambacho wananchi wanakiona, ni hatua ya rais ya kupuuza misingi yote mikuu iliyopandikizwa na kulelewa na viongozi wote wakuu wa taifa, ikiwamo misingi ya uwiano wa Muungano, ukabila, jinsia, dini na maeneo wanakotoka watu.

Tatu, kama Rais Magufuli ni mpenda haki asiishie kurejesha mali za Waislamu pekee yao. Arejeshe shule za madhehebu ya Kikristo.

Dk. Magufuli anajua kuwa mwaka 1971, serikali ilitaifisha kwa nguvu shule, vyuo, hospitali na taasisi za mashirika ya dini nchini kote. Madhehebu ya Kikristo ndiyo yaliathirika sana kwa kuwa yalikuwa na mali na taasisi nyingi zaidi.

Dhuluma hii ilifanywa na serikali bila kuwapo kwa sheria ya kuruhusu kufanyika hilo. Sheria ya ubinafishaji wa mali za madhebu ya kidini ilitungwa baada ya mali hizo kutaifishwa.

Kwa miaka mingi makanisa yamedai chini ya marais Wakristo kwa Waislam, lakini serikali haijeweza kureshea mali zao.

Madhehebu hayo hayakuuza mali zao kwa serikali. Serikali ilichukua kwa kuwa ilijiona ina mamlaka kwenye mali zisizo zake.

Ikiwa ni kweli kwamba Rais Magufuli ana uchungu sana na mali za Bakwata zilizouzwa na madalali wenyewe wa baraza hilo, uchungu huohuo, utumike kurejesha mali za madhehebu ya Kikristo zilizotaifishwa kwa nguvu na serikali.

Kwa kutenda hilo, rais ataonekana anachukia dhuluma kwa vitendo. Ataweza kujitofautisha na hata watangulizi wake wanaotuhumiwa kudhulumu na kusaidia kutapanywa kwa mali ya madhehebu ya kidini na jamii nyingine.

Akimaliza kusaidia kurejeshwa kwa mali za Waislamu na Wakristo, ageukie kwenye dhuluma nyigine kubwa iliyofanywa na chama chake – Chama Cha Mapinduzi (CCM) – dhidi ya wananchi.

Magufuli anajua kwamba wananchi walijenga viwanja vya michezo makao makuu ya wilaya au mikoa. Walimiliki viwanja na vitega uchumi lukuki.

Lakini CCM ilijimilikisha mali zote kwa nguvu. Hii ni dhuluma bila kujali nani alikuwa kiongozi wakati huo. Rais Magufuli amesikika mara kadhaa akisisitiza kuwa, ikiwa serikali ilifanya makosa huko nyuma hapana budi yarekebishwe.

Tumemwona Rais Magufuli akitengua baadhi ya mambo anayoamini kuwa yalifanyika kimakosa. Ni vema asije kula ng’ombe ukamshinda mkia.

Rais asimamie haki kwa kuondoa dhuluma kila kona ya nchi, ili taifa liweze kushamiri kwa haki.

Hakala hii imeandikwa katika Gazeti la MwanaHALISI toleo No. 347 la tarehe 11-17 Julai mwaka huu.

error: Content is protected !!