February 28, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Rais Magufuli apingwa kila kona

John Magufuli, Rais wa Tanzania. Picha ndogo wafuasi wa Chadema wakiandamana

Spread the love

RAIS wa Jamhuri, John Pombe Magufuli, ameonya wananchi wake wanaotaka kufanya maandamano ya amani kupinga utendaji wa serikali yake, kuwa watakabiliana na jeshi la polisi. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).

Amesema, akiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hatakubali kuona wananchi wakiandamana kwa kuwa kufanya hivyo, ni kurudisha nyuma maendeleo ya serikali yake.

Ametoa kauli hiyo, kwenye sherehe ya ufunguzi wa tawi la benki ya biashara ya CRDB, nyumbani kwake, wilayani Chato, mkoani Geita, leo Ijumaa.

Amesema, “wapo watu wanaogependa nchi hii, kila siku iwe na migogoro. Hawa watu wameshindwa kufanya siasa za kweli, wanataka tushinde barabarani kuandamana. Nasema hivi, waache waandamane. Wataniona.”

Ameongeza, “…kama kuna watu wamewatuma hao wanaotaka kuandamana, basi wataenda kuwasimulia vizuri kitakachowapata.”

Kuibuka kwa Rais Magufuli kuzungumzia maandamano kumekuja katika kipindi ambacho baadhi ya wananchi wamekuwa wakihamasishana kuandamana kupinga wanachoita, “ukatili wa utawala wa awamu ya tano.”

Aidha, kuibuka kwa taarifa hizi kumekuja katika kipindi ambacho mashirika ya hiari, vyama vya siasa, wabunge, madiwani na baadhi ya viongozi wa madhehebu ya kidini, wakiendelea kushinikiza serikali kuruhusu mikutano na maandamano.

Akijibu tamko la Rais Magufuli, mara baada ya kulitoa kijijini Chato, mbunge wa Chadema katika jimbo la Arusha Mjini, Godbless Lema amesema, “maandamano ni haki ya kikatiba.”

Lema anasema, “rais anayejali anapaswa kusikiliza madai ya wananchi wake. Hosni Mubarak, Muammar Gaddafi na hivi karibuni, Hailemariam Desalegn, waziri mkuu wa Ethiopia, waliwahi kutoa kauli kali juu ya maandamano. Hata hivyo, nguvu ya umma ilishinda.”

Naye mbunge wa Ubungo, Saed Kubena akiandika katika ukurasa wake wa twitter, amekosoa hatua ya Rais Magufuli kutumia mkutano wa kibiashara kuzungumzia maandamano.

Amesema, “bada ya kutumia ufunguzi wa benki kuhamasisha wananchi kufungua akaunti ili kutunza fedha; kuchochea biashara na kuhamasisha uwekezaji, unapiga marufuku maandamano, ambayo ni haki ya kikatiba?”

Anaongeza, “…unasema, watakaoandamana watakutambua? Haya! Sasa wakiamua kuandamana, siyo watakutambua – kwa kuwa watakuwa wameshajiandaa kutokana na kitisho ulichowapa – hakika mtatambuana.”

Kubenea amesema, vitisho havijengi nchi na wala havisaidii kuondoa malalamiko ya wananchi dhidi ya serikali yao.

Badala yake, mbunge huyo machari anasema, “vitisho vinaongeza chuki na uhasama ndani ya nchi na jamii.”

error: Content is protected !!