Friday , 29 September 2023
Home Gazeti Habari za Siasa Rais Magufuli apiga chenga wafanyakazi
Habari za SiasaTangulizi

Rais Magufuli apiga chenga wafanyakazi

Spread the love

FIKRA kwamba, Rais John Magufuli angeongeza mishahara kwa wafanyakazi wa sekta ya umma leo, zimetoka patupu. Anaripoti Regina Mkonde … (endelea).

Akihutubia katika maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani ‘Mei Mosi’ jijini Mbeya leo tarehe 1 Mei 2019, Rais Magufuli amesema, serikali inakabiliwa na changamoto ya gharama za uendeshaji ikiwemo kulipa mishahara ya watumishi, deni la taifa pamoja na kutekeleza miradi ya maendeleo.

Hata hivyo amesema, ahadi yake ya kuongeza mishahara kwa watumishi wa umma pamoja na kutatua changamoto zao iko pale pale na kwamba, kwa sasa amejikita katika kuimarisha uchumi wa nchi ili hata watakapoongezewa mishahara fedha zao ziwe na thamani.

Rais Magufuli amesema, gharama za kuendesha serikali ni kubwa na kwamba kiasi cha fedha kinachobakia ni kidogo, hivyo fedha hizo ni bora zipelekwe katika miradi ya maendeleo ili kukuza uchumi wa nchi.

“Gharama za kuendesha serikali bado ni kubwa, tunatumia takribani Sh. 580 Bil, kulipa mishahara kila mwezi, kwa bahati nzuri siku hizi tunalipa tangu tarehe 19 suala ambalo lilikuwa halipo, najua hili tungelipa hata tarehe 2 msingeshangilia,” amesema Rais Magufuli na kuongeza;

“Lakini pamoja na kwamba tunalipa kila mwezi, bado hicho kiasi kilichobaki tunatakiwa kulipa madeni ya mkopo. Tunatakiwa pia tushughulikie miradi ya maendeleo hivyo mnaweza kuona wenyewe tunatumia kiasi gani, na kinachobaki tumekuwa tukijiuliza tukipeleke wapi.”

Kwenye maadhimisho hayo Rais Magufuli amesema, “hapo ndipo tumekuwa pia tukijiuliza kama mkulima mwenye mbegu anavyojiuliza wakati wa njaa, atumie kwa chakula au azitunze ili msimu wa mvua azipande zimletee chakula.”

Ametoa mfano huo huo kwa wafanyabiashara kwamba, anavyojiuliza atumie mtaji wake kutatua shida zake au atafute shughuli nyingine za kumuongezea vipato na sisi tumekuwa tukijiuliza.

“Tuliona ni busara kutumia kiasi kidogo ili kilichobaki tukiweke katika miradi ya maendeleo ili kuchochea uchumi, na kukuza uchumi kwa kasi zaidi,” amesema.

Rais Magufuli amesisitiza kuwa, ahadi yake ya kuongeza mishahara kwa watumishi wa umma kabla ya uongozi wake wa awamu ya kwanza kuisha iko palepale, na kuwataka watumishi kuwa na subira.

“Naomba muamini kwamba subira yavuta kheri, muda wangu bado haujaisha, ungeweza kusema napandisha sh. 5000 kesho bidhaa zingepanda, ni lazima tujenge uchumi imara. Ndugu zangu kupanga ni kuchagua, tungesema hakuna kuajiri hizi tunagawana posho, ninachotaka kuwaeleza ahadi yangu bado haijaisha, muda wangu wa utawala bado haujaisha,” amesema Rais Magufuli na kuongeza;

“Na kwa muelekeo unavyoenda kwa mambo yanavyoenda na mimi naamini yatafanikiwa kadiri ya uchumi wetu unavyoenda kwa sababu uchumi wetu bado unakua kwa silimia 7.

“Tanzania ni nchi miongoni mwa nchi tano Afrika ambao uchumi wake unakuwa kwa kasi, na kwa uchapakazi unaofanywa na wakulima, na wafanyabaishara tunaelekea pazuri, nimeamua niwaeleze ukweli na ukweli utabaki palepale, kwa hiyo ndugu zangu mvumilie, sikutaka kuwapaka uji kwa kusema nimepandisha.”

Aidha, Rais Magufuli amesema tangu serikali yake iiingie madarakani imetatua changamoto za watumishi wa umma ikiwemo kutoa nyongeza ya mshahara yenye thamani zaidi ya 72 bilioni, kupandisha madaraja watumishi 118989 ambapo kiasi cha Sh. Bilioni 29 zimetumika, pia amesema kwa mwaka ujao wa fedha wa 2019/20 serikali itapandisha madaraja watumishi 193,169.

Pia, amesema serikali imelipa deni ililokuwa inadaiwa na mifuko ya hifadhi ya jamii kiasi cha sh. Trilioni 1.5, imeajiri watumishi 42,735 ambao mishahara yapo ugharimu Sh. 25.8 bilioni kila mwezi, pia amesema itaajiri watumishi 45,000 mwaka ujao wa fedha.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

Serikali yawaangukia viongozi wa dini

Spread the loveSERIKALI imewaomba viongozi wa dini, waendelee kuelimisha wananchi kudumisha amani...

Habari MchanganyikoTangulizi

Afya ya akili yatajwa chanzo kuvunjika ndoa

Spread the loveCHANGAMOTO ya afya ya akili, imetajwa kuwa chanzo cha migogoro...

Habari za Siasa

Azzim Dewji aitaka Serikali iwanyooshe mafisadi

Spread the loveMFANYABIASHARA maarufu nchini, Azzim Dewji, ameitaka Serikali iwachukulie hatua wezi...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Kapinga: Usambazaji umeme vijijini mwisho Desemba 2023

Spread the love  NAIBU Waziri wa Nishati, Judith Kapinga, amesema ifikapo mwezi...

error: Content is protected !!