October 7, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Rais Magufuli aonya pokeapokea vifaa ya corona, watakaobainika

John Magufuli, Rais wa Tanzania

Spread the love

JOHN Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, amewaonya watu watakaopokea misaada ya vifaa vya kupambana na janga la virusi vya Corona (Covid-19), vyenye dosari. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).

 Akizungumza mara baada ya kumaliza kuwaapisha viongozi sita aliowateua hivi karibuni Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma, leo Alhamisi tarehe 21 Mei 2020, Rais Magufuli amesema mtu atakayekubali kupokea vifaa hivyo na kubainika kuwa na virusi vya corona, atafunguliwa kesi ya mauaji.

Mkuu huyo wa nchi ameitaka wizara ya afya nchini humo, kuvikagua vifaa hivyo kabla ya kutumika, ili kujua kama viko salama kwa matumizi ya Watanzania.

“Nawaomba wizara ya afya kalisimamieni hili, na mtu atakayepewa mavifaa ya kuzuia Corona halafu mkayapima yakakutwa yana Corona,  huyu mpeleke kwenye kesi ya jinai hata ya mauaji kama wauaji wengine, “ amesema Rais Magufuli.

Rais Magufuli amewataka watendaji wa Serikali kujiepusha na misaada isiyothibitishwa na mamlaka husika.

 “Kwa hiyo, watendaji  wajiepushe kupokea pokea, ndio maana nimemuona waziri (Prof. Palamagamba Kabudi, Waziri Mambo ya Nje)  anazungumza tunataka hela. Tutatengeneza barakoa zetu wenyewe, tutanunua vifaa ambavyo tunajua vimekaguliwa, na kujua vinafaa kwa ajili ya matumizi ya Watanzania,” amesema Rais Magufuli.

 Wakati huo huo, Rais Magufuli amesema kasi ya maambukizi ya homa kali ya mapafu  inayosababishwa na virusi hivyo (Covid-19), inapungua, na kuwataka Watanzania kuwa makini ili maambukizi hayo yasiongezeke tena.

“Nawaomba Watanzania kwenye hili tuchukue tahadhari, kubwa Corona inashuka chini inaelekea kuisha, lakini tusije tukapandikiziwa Corona kwa uzembe wetu,” amesema Rais Magufuli.

Rais Magufuli amesema, Tanzania inapenda kupokea misaada, lakini iko makini katika kufuatilia misaada hiyo, kwa kuwa janga la Corona ni vita.

“Vya dezo vinaua, tunahitaji misaada na tunashukuru sana wanaoamua kutusaidia. Huu ni wakati wa vita kama zilivyo vita vingine. Huu ugonjwa ni vita na katika vita kuna mbinu nyingi,” amesema Rais Magufuli

“Katika michango inaweza ukaletewa barakoa yenye Corona, na hasa kwa sababu mwenendo wetu unaenda vizuri kutokana na hatua tunazochukua, yako mengi tunachukua lakini hatuyatangazi, vya bure ni vibaya.”

Kwa mara ya kwanza, nchi ya Tanzania iliripoti mgonjwa wa kwanza cha ugonjwa wa Covid-19, tarehe 16 Machi 2020, ambapo ilianza kuchukua hatua mbalimbali kukabiliana na maambukizi ya ugonjwa huo, ikiwemo kuzuia shughuli zenye mikusanyiko ya watu wengi.

Baada ya miezi miwili na nusu kupita, Tanzania imeanza kurejesha baadhi ya shughuli zenye mikusanyiko, ikiwemo vyuo vikuu na michezo kuanzia tarehe 1 Juni, 2020.

error: Content is protected !!