Tuesday , 21 March 2023
Home Gazeti Habari za Siasa Rais Magufuli amkomoa Nape, kisa kamgusa Makonda
Habari za SiasaTangulizi

Rais Magufuli amkomoa Nape, kisa kamgusa Makonda

Nape Nnauye, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo
Spread the love

CHINI saa 24 tangu Nape Nnauye atoe ahadi ya “kumshughulikia” Paul Makonda amekomolewa yeye, anaandika Hamisi Mguta.

Nape katika nafasi ya uwaziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, juzi aliunda kamati ya kuchunguza kilichotokea katika tukio la Ijumaa usiku tarehe 17 Machi ambalo Makonda, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, anatajwa kuvamia kituo cha Clouds Media akitumia askari wa serikali wenye bunduki na kutishia watangazaji warushe kipindi cha Shilawadu kwa namna atakavyo.

Jana mchana Nape alikabidhiwa ripoti ya uchunguzi huo uliothibitisha Makonda amefanya uvamizi huo na alilofuatwa na kamati hiyo kutoa maelezo alikimbia ofisini.

Nape alisema akishapitia ripoti iliyofungamanishwa na vielelezo vya picha na sauti, atapeleka mapendekezo kwa mamlaka za juu yake akitaja waziri mkuu, makamu wa rais na rais.

Lakini kwa hatua aloichukua Rais Magufuli asubuhi hii ya kumtangaza Dk. Harrison Mwakyembe kushika uwaziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, ina maana amezuia mapendekezo kufika kwenye mamlaka za juu.

Rais Magufuli katika taarifa iliyoenezwa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu, amemteua Prof. Palamagamba Kabudi kuwa Waziri wa Katiba na Sheria badala ya Dk. Mwakyembe.

Wakati Nape, mwenye shahada ya kwanza ya mawasiliano aliyoisomea nchini India, anaunda kamati ya kuchunguza uvamizi wa Clouds Media alisema tasnia ya habari anayosimamia imeguswa.

Hapohapo, Rais Magufuli yeye siku hiyo ya Jumatatu alimwambia Makonda achape kazi yeye ndio amemteua kuliko kushughulishwa na maneno yanayoandikwa mitandaoni na magazetini.

Alikuwa akihutubia hafla ya uzinduzi wa ujenzi wa barabara ya juu ya kupita kwenye makutano ya barabara za Morogoro, Sam Nujoma na Mandela, eneo la Ubungo jijini Dar es Salaam.

Kufuatia uvamizi wa Clouds Media Group uliofanywa na Makonda, taasisi za wanahabari zikiwemo vyombo vya habari vimetangaza kutoshirikiana na Makonda kihabari.

Jana ilikuwa zamu ya Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) na Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Dar es Salaam kutangaza kuanza kumnyima Makonda ushirikiano wa kihabari.

Kwa miezi miwili sasa Makonda amekuwa katika kipindi cha kukabiliwa na joto la kutajwa kuwa ametumia vyeti bandia ili kupata fursa ya kujiendeleza kielimu.

Wakati jina alopewa na wazazi alipozaliwa imethibitishwa kuwa ni Daudi Albert Bashite, aliingia chuo cha uvuvi Nyegezi kwa jina la Paul Christian Makonda.

Uchunguzi umebaini Paul Christian ni jina la mtu waliyesoma naye ambaye alifaulu mtihani wa taifa wa kidato cha nne. Daudi Albert Bashite yeye alifeli.

Ingawa tuhuma za kuwa Makonda ana vyeti vya kughushi ziliwahi kuripotiwa gazetini mwaka 2013, na hadi sasa mwenyewe amejizuia kuzisemea kwa ufasaha, zimepata kutajwa kwa nguvu kubwa ndani ya mitandao ya jamii na vyombo vya habari baada ya kuanzisha kampeni ya kudhibiti biashara na matumizi ya dawa za kulevya Februari 2 mwaka huu kwa mfumo wa kutangaza hadharani majina ya alowashuku.

Katika hatua yake hiyo anayoitekeleza kwa kutumia fursa ya matangazo live ya televisheni na redio, alianza na orodha ya wasanii na wanamitindo maarufu na baadae wanasiasa na wafanyabiashara.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

Rais Samia aagiza iundwe kamati ya pamoja ya Mawaziri mradi wa BBT

Spread the love  RAIS Dk. Samia Suluhu Hassan, amewaagiza mawaziri kuunda kamati...

Habari za Siasa

Rais Samia apangua makatibu tawala mikoa, ateua Kamishna DCEA

Spread the loveALIYEKUWA Kamishna wa Mamlaka ya Kudhibiti Dawa za Kulevya, Gerald...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

M/kiti bodi ya wadhamini Chadema afariki dunia

Spread the loveMWENYEKITI wa Bodi ya Wadhamini ya Chama cha Demokrasia na...

Habari za Siasa

Zitto: Nikifa Ado atavaa viatu vyangu

Spread the love  KIONGOZI Mkuu wa Chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe...

error: Content is protected !!