April 17, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Rais Magufuli ampa kazi Rostam Aziz

Spread the love

RAIS John Magufuli amempa kazi Rostam Aziz, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Taifa Gas Tanzania Limited, kutafuta wawekezaji. Anaripoti Regina Mkonde … (endelea).

Amempa kibarua hicho leo tarehe 25 Juni 2019 wakati akizindua ghala na mitambo ya gesi ya kupikia (LPG), inayomilikiwa na kampuni hiyo  iliyoko Vijibweni, Kigamboni jijini Dar es Salaam.

Akizungumza katika uzinduzi huo, Rais Magufuli amesema, hapendi wawekezaji wa maneno bali wanaotekeleza kwa vitendo, na kumwambia Rostam atafutie wawekezaji wa aina hiyo kama 10 au 20.

 “Mimi huwa sipendi wawekezaji wa maneno maneno tu. Umeonesha njia, imenipa nguvu sana, tafuta wawekezaji wengine hata 10 au 20 wenye moyo wa kuwekeza, tuje tuwape sapoti serikali na sisi tutawapa sapoti, tunahitaji wawekezaji wa ukweli,” amesema Rais Magufuli.

Aidha, Rais Magufuli amewataka wawekezaji kutosikiliza maneno ya watu aliowataja kuwa hawaitakii mema nchi, huku akisisitiza kwamba, serikali yake iko tayari kuwapa ushirikiano.

“Wawekezaji wa ukweli waje wasisikilize maneno ya wale ambao hawatutakii mema. Waje wawekeze tutawasaidia, lakini tunataka wanapowekeza serikali nayo kupitia wananchi wake wapate.”

Akizungumza kuhusu uwekezaji wa Kampuni ya Taifa Gas, Rais Magufuli amesema uwekezaji huo uliogharimu kiasi cha Sh. 150 Bilioni ikiwemo ujenzi wa mitambo ya kuhifadhi gesi kwenye mikoa 20, imeongeza uwezo wa nchi kuhifadhi gesi kutoka tani 8,050 mwaka 2016 hadi kufikia tani 15,600.

“Miongoni mwa kampuni zinazofanya biashara ya gesi ya mitungi ni yaani LPG,  Taifa Gas Tanzania Limited ambayo zamani ilijulikana Mihan Gas. Kampuni hii kama mlivyosikia imewekeza kiasi cha bil 150 ikihusisha ujenzi wa magala na mitambo ya kuhifadhi gesi kwenye mikoa 20 mojawapo ni hili ninalolizindua leo ambalo lina uwezo wa kuhifadhi tani 7,650,” amesema Rais Magufuli na kuongeza.

 “Ghala hili kubwa kwa nchi za Afrika Mashariki limeifanya Taifa Gas kuongoza kwa kuwa na uwezo wa kuhifadhi gesi nchini.  Rostam ninakupongeza sana pamoja na Watanzania wengine kwa uwekezaji huu mkubwa ambao mmeufanya kutengeneza ajira 260 na ajira nyingine kufikia 3,000.”

Wakati huo huo, Rais Magufuli ametoa wito kwa wasambazaji wa gesi za mitungi kupanua huduma zao hususani katika maeneo ya vijijini.

error: Content is protected !!