August 16, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Rais Magufuli ameshindwa mapema

Spread the love

 

RAIS John Pombe Magufuli aweza kukwama mapema. Alichokisema miezi 10 iliyopita sicho anachokitenda sasa. Alivyoahidi ameanza kuvisahau. Anavyong’ang’aniza havitekelezeki, anaandika Saed Kubenea. 

Baadhi ya waliokuwa wamemuunga mkono katika mbio zake za kusaka urais, tayari mmoja mmoja wameanza kulalamika kuwa amewaangusha.

Akihutubia Bunge la Jamhuri, 20 Novemba 2015, Dk. Magufuli aliahidi kujenga nchi yenye uchumi wa viwanda na kutoa upendeleo maalum kwa wawekezaji wazalendo.

Alisema katika kipindi chake cha miaka mitano, atalifanya taifa hili kuwa lenye watu wenye kipato cha kati. Atapunguza tatizo la ukosefu wa ajira kwa vijana na kuimarisha utawala bora.

Akawataka wabunge kumuamini kwa kuwa yeye hutenda anachokinena. Alisema anamuogopa Mungu na anaongoza nchi kwa “kufuta Katiba.”

Dk. Magufuli alikuwa akieleza bungeni mwelekeo wa serikali yake katika kipindi cha miaka mitano ijayo.

Katika kipindi cha kuelekea uchaguzi mkuu wa rais, wabunge na madiwani, Dk. Magufuli aliahidi kila mwanafunzi anayesoma elimu ya juu kupatiwa mkopo na serikali.

Akihutubia wananchi katika viwanja vya Mashujaa mjini Moshi, Magufuli alisema, “…hakuna mwanafunzi atakayekosa mkopo, ikiwa nitafanikiwa kuwa rais.”

Alihoji, “pesa yenyewe ni mkopo, kwanini umnyime mtu wakati ni yeye atakayekuja kulipa? Nafahamu kuwa bila mikopo watoto wa maskini hawawezi kusoma.”

Alipokabidhiwa uenyekiti wa chama chake – Chama Cha Mapinduzi (CCM) – Julai mwaka huu, aliibuka na hoja mpya ya kuhamishia serikali mjini Dodoma.

Katika hotuba yake kwa wajumbe wa mkutano mkuu wa CCM, Magufuli alisema, “…kwa kutambua umuhimu wa mji huu, katika kipindi cha miaka mitano ya uongozi wangu, nitahakikisha serikali inahamia Dodoma.”

Aliahidi kulinda na kudumisha amani na utulivu. Alisema licha ya tofauti za kisiasa, dini, kabila au maeneo wanakotoka, “taifa bado limebaki kuwa kisiwa cha amani na watu wake ni wamoja.” Tujadili:

Kwanza, kile ambacho rais aliahidi bungeni – kujenga nchi yenye uchumi wa viwanda – hakiwezi kutendeka.

Hii ni kwa sababu, ili kujenga taifa la viwanda sharti kuwapo nishati ya umeme wa uhakika, maji na nguvu kazi.

Bila kuwapo umeme wa uhakika, bila maji na bila nguvu kazi iliyosheheni wataalamu, hakuna viwanda. Ni maigizo.

Pamoja na taifa kuzungukwa na maziwa makubwa, yakiwamo maziwa Viktoria, Nyasa na Tanganyika, hakuna mkakati wa kutumia maji yaliyo katika maziwa hayo kuzalisha umeme; na au kuyatumia viwandani.

Kuwapo kwa umeme wa uhakika kutavutia wawekezaji wa ndani na nje na kupunguza gharama za uendeshaji viwanda na uzalishaji bidhaa zinazoweza kuhimili ushindani wa soko.

Aidha, hakuna kokote ambako taifa limeweza kuitwa “taifa la viwanda,” bila kuwekeza katika nguvu kazi ya vijana.

Magufuli hawekezi kwa vijana. Alichoahidi kwa kauli ya “elimu bure,” bado kingali mateso. Watu wanachangishwa michango ya shule; ikiitwa ya hiari, lakini ikikusanywa kwa shuruti.

Ameshindwa kuwapatia watoto wa masikini mikopo kama alivyoahidi. Mathalani, katika mwaka huu, tayari wanafunzi zaidi ya elfu 20 wamekosa mikopo.

Watumishi wanachangishwa madawati. Taasisi za umma zinalalamika kunyofolewa mafungu yao ili fedha zielekezwe kwenye kuchangia madawati.

Baadhi ya halmashauri za miji, wilaya na manispaa, nazo zimelazimishwa kutoa fedha kinyume cha bajeti walizopitisha.

Ukosefu wa mikopo kwa wanafunzi kutachangia, kwa kiwango kikubwa, kushindwa kutekelezwa kwa ahadi ya kuwa na taifa la viwanda.

Ibara ya 8.1 (b) ya Katiba ya Jamhuri inataja lengo kuu la serikali kuwa ni maendeleo na ustawi wa wananchi.

Kwamba wananchi ndiyo msingi wa mamlaka yote; juhudi zote za serikali zitaekelezwa kwa ustawi wa wananchi.

Lakini serikali ya Magufuli inahubiri matumaini, bila kustawisha wananchi.

Kuna hili jingine. Ujenzi wa kila kiwanda kimoja, unategemea kuwapo kwa kiwanda kingine.

Kwa mfano, ili uweze kujenga kiwanda kimoja cha nguo, ni sharti kuwapo viwanda vingine vitatu – kiwanda cha kusokota nyuzi, vitambaa na dawa za viwandani.

Kukosekana kwa kiwanda kimoja kati ya hivyo, kutalazimisha serikali kuagiza malighafi kutoka nje.

Kuagiza malighafi kutoka nje, kutazifanya bidhaa zinazozalishwa na viwanda vya ndani kuuzwa kwa bei ya juu na kushindwa kuhimili ushindani.

Wala serikali haiwezi kusema itaongeza ushuru wa nguo zinazotoka nje na ikafanikiwa. Haiwezekani.

Kufanya hivyo kutasababisha kushitakiwa moja kwa moja katika Shirika la Biashara la Dunia (WTO), ambako Tanzania ni mwanachama.

Shirika hili lilianzishwa ili kuhakikisha mkataba wa biashara (Trade Facilitation Agreement) unatekelezwa. Mkataba unaelekeza kuwapo ushindani huru wa kibiashara duniani.

Hatua yeyote ya kwenda kinyume na mkataba, ni kutaka kujiingiza katika mgogoro. Ni kufukuzwa uanachama na kutengwa kimataifa. Je, serikali iko tayari kwa hilo?

Kabla ya Magufuli kuja na ndoto ya kuwa na “taifa la viwanda,” angejiuliza kilichosababisha kufa kwa viwanda vilivyokuwapo.

Angejiuliza kilichosababisha serikali kubinafsisha viwanda vyake. Kilichosababisha nguo zinazozalishwa na viwanda vya ndani kuzorota.

Serikali ilifikia uamuzi wa kuuza viwanda vyake au kuvibifsisha kwa sababu ya usimamizi mbovu.

Haikutarajiwa Dk. John Pombe Magufuli, ambaye amekuwa ndani ya serikali kwa zaidi ya miaka ishirini (20), kuibuka na ujenzi wa viwanda, bila maandalizi. Bila kupatikana mwarobaini wa kilichosababisha viwanda kuuzwa au kufungwa.

Pili, hata hili la kuhamishia watendaji wa serikali Dodoma, haliwezi kufanikiwa kwa njia ya vitisho ya kufukuza kazi watakaoshindwa kuhamia Dodoma; kuuza majengo ya serikali na kuigeuza Ikulu kuwa jengo la makumbusho.

Kuhamishia serikali Dodoma kunahitaji maandalizi. Kunahitaji fedha na uratibu kamilifu.

Huwezi kuhamishia serikali Dodoma kwa njia ya dharura. Huwezi kuhamisha makao makuu ya nchi mahali kwingine, bila kushirikirisha Bunge.

Pamoja na kuwa hili liliishaamuliwa wakati wa utawala wa Mwalimu Nyerere na kwamba yeye anatekeleza tu, utekelezaji wa njia ya pupa, utagharimu nchi.

Haingii akilini kuamuru kuhamishia serikali Dodoma, bila jambo zito kama hilo, kuwamo kwenye dira ya taifa na ilani ya uchaguzi ya chama chako.

Mpango wowote wa kuhamishia serikali Dodoma bila kuingizwa kwenye dira ya taifa ya maendeleo, ni hatari kwa ustawi wa taifa.

Ndani ya mpango wa miaka mitano wa serikali, uliowasilishwa bungeni, suala la kuhamishia serikali Dodoma halimo pia.

Hii ina maana kuwa hakuna mpango mkakati unaotumika kuongoza serikali. Bali, rais anaongoza nchi na kutaka ifike mahali ambako hata yeye hakujui.

Tatu, rais anatakiwa, tena ni kwa mujibu wa Katiba aliyoapa kuitekeleza, kuilinda na kuitetea, kuhakikisha serikali inaendeshwa kwa misingi ya utawala bora.

Anatakiwa kuhakikisha kunakuwapo na utawala unaozingatia kanuni na sheria zilizowekwa kwa mujibu wa Katiba.

Lakini ni yeye aliyeapa kulinda na kutetea Katiba ya Jamhuri, anayeongoza kwa ukikwaji wa wazi wa katiba.

Hatua yake ya kuzuia vyama vya upinzani kufanya kazi za kisiasa – akizuia mikutano na maandamano –siyo tu rais anavunja Sheria ya Vyama Vya Siasa, anavunja hata Katiba.

Ametamka waziwazi kuwa wanaotaka kufanya siasa wasubiri hadi mwaka 2020; amekuwa akirejea hilo na kuliwekea mkazo mara kwa mara.

Rais anayedai kuongoza kwa misingi ya sheria na kuheshimu Katiba, anatenda kinyume cha kile anachokieleza.

Ni yeye pakee aliyejihalalisha kuwa mwenye sababu ya kuzunguka nchi nzima – kila jimbo – kufikisha maendeleo aliyowaahidi wananchi  wote.

Amri ya rais ina maana kwamba vyama vingine ambavyo havina wabunge, madiwani na wenyeviti wa serikali za mitaa, hawataruhusiwa kufanya siasa hadi uchaguzi mkuu ujao au uchaguzi wa serikali za mitaa – mwaka 2019.

Hii ina maana kwamba vyama vya siasa vimeporwa uhuru na haki ya kufanya siasa ambavyo vinatambuliwa na Katiba ya Jamhuri ya Muungano na Sheria ya Vyama Vya Siasa.

Hatua ya Rais Magufuli inakwenda kinyume cha Ibara ya 20 (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.

Kwa mujibu wa katiba, vyama vya siasa na wanasiasa mmojammoja, wana haki ya kufanya mikutano na maandamano, kokote wanakotaka ndani ya Jamhuri ya Muungano.

Ibara hiyo inasema, “…kila mtu ana uhuru wa kukutana na watu wengine kwa hiari yake na kwa amani, kuchanganyika, kushirikiana na watu wengine; na kwa ajili hiyo kutoa mawazo yake hadharani.”

Ibara inaongeza kuwa kila mtu ana uhuru wa kuanzisha na kujiunga na vyama au mashirika yaliyoanzishwa kwa madhumuni ya kuhifadhi au kuendeleza, imani au maslahi yake au maslahi mengineyo.

Aidha, Ibara ya 18 (a) ya Katiba ya Jamhuri, inatambua uhuru wa kila mtu kuwa na maoni na kueleza fikra zake.”

Katazo la mikutano la Rais Magufuli, ni kinyume cha Kifungu cha 11 cha sheria ya vyama vya siasa ya mwaka 1992.

Kwa mujibu wa sheria hiyo suala la maandamano na mikutano kwa vyama linatambuliwa hata katika tangazo la Serikali Na. 215 la 12 Oktoba 2007.

Vilevile sura ya 258 ya kanuni za maadili ya vyama vya siasa ya mwaka 2007, inatambua na kuelekeza kuwapo uhuru wa vyama kukutana na wananchi, kufanya maandamano na mikutano.

Sehemu ya pili ya kifungu cha 4(1) cha sheria hiyo inasema, pamoja na mambo mengine, “…kila chama cha siasa kitakuwa na haki ya kutoa elimu ya uraia; na pia kutoa elimu ya uchaguzi kwa wananchi kwa kufuata sheria na kanuni za nchi.”

Lakini swali la kujiuliza ni hili: Nguvu zote hizi zinalenga nini? Jibu ni hili. Kwamba Rais Magufuli anajua kuwa ndani ya miaka mitano ya utawala wake, hawezi kujenga viwanda. Hawezi kujenga uchumi wa kati na hawezi kulifanya taifa hili kuwa la viwanda.

Anajua pia kuwa hawezi kuhamishia serikali Dodoma ndani ya kipindi hiki kifupi cha miaka minne na miezi miwili.

Magufuli anatamani kugombea tena urais mwaka 2020 na kwamba ili asihojiwe na wananchi, ni sharti atishe na kuangamiza upinzani.

Vinginevyo, atapambana na upinzani kuanzia ndani ya chama chake. Atapambana na upinzani wa wananchi.

 

Makala hii kwa mara ya kwanza imechapishwa kwenye Gazeti la MwanaHALISI Toleo No. 353 la tarehe 22-28 Agosti, 2016.

…………………………………………………………………………………………………..

Soma gazeti la MwanaHALISI kila Jumatatu kwenye simu yako kupitia, (bonyeza)> Mpaper kwa wateja wa Vodacom pia (bonyeza)> Simgazeti kwa wateja wa Vodacom, Tigo na Airtel. Pia unaweza kupakua (download) app ya Mpaper au Simgazeti kutoka kwenye playstore.

error: Content is protected !!