Thursday , 30 March 2023
Home Gazeti Habari za Siasa Rais Magufuli akerwa na wizara ya Dk. Mwigulu
Habari za Siasa

Rais Magufuli akerwa na wizara ya Dk. Mwigulu

Spread the love

 

RAIS wa Tanzania, John Magufuli ameonesha kukerwa na hatua ya Wizara ya Katiba na Sheria, inayoongozwa na Waziri, Dk. Mwigulu Nchemba kwa kushindwa kuajiri watumishi wapya 200 licha ya kupewa kibali tangu mwaka 2020. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).

“Watu 200 wafanyakazi wa mahakama mwaka umepita hawajaajiriwa, lazima tujiulize wizara kuna tatizo,” amesema Rais Magufuli.

Ametoa kauli hiyo leo Jumanne tarehe 2 Februari 2021, jijini Dodoma wakati akijibu ombi la Prof. Ibrahim Juma, Jaji Mkuu wa Tanzania la kuongeza watumishi wa mahakama.

Rais Magufuli amesema, wizara nyingine zimeajiri watumishi wake mara baada ya kutoa vibali vya ajira, lakini wizara hiyo haikutekeleza suala hilo.

“Kuna mambo mengine yanasikitisha, nimekuwa nikitoa vibali kwa watu kuajiriwa katika wizara mbalimbali, mwaka jana nilitoa vibali kwa madaktari 1,000 waliajiriwa, walimu 8,000 haikuchukua miezi mwili zikatangazwa nafasi za ajira, wakaajiriwa,” amesema Rais Magufuli.

Amemuagiza Waziri Dk. Nchemba na wasaidizi wake kulifanyia kazi suala hilo mara moja.

“Nikishasema ndio nimemaliza, mbona wizara nyingine zinafanya? lakini wizara hii wafanyakazi wa mahakama hawajaariwa mwaka umepita, katibu mkuu upo, waziri upo, AG (Mwanasheria Mkuu wa Serikali ) yupo, hii kasoro muirekebishe.”

“Kibali kimetolewa mwaka mzima umepita hawajaajiriwa, kashughulikieni hili,” ameagiza Rais Magufuli huku Waziri Mwigulu aliyekuwepo kwenye hafla hiyo, akisimama kuonyesha kuitikia agizo hilo.

Awali, Prof. Juma alimuomba Rais Magufuli aongeze watumishi wa mahakama, ili kuondoa changamoto ya mlundikano wa mashauri mahakamani hasa katika Mahakama Kuu na Mahakama za Rufaa.

Alitoa ombi hilo wakati wa kuapishwa aliyekuwa Jaji wa Mahakama Kuu, Kanda ya Musoma, Zepharine Galeba aliyepandishwa cheo na Rais Magufuli kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufaa.

Ni baada ya kutumia Lugha ya Kiswahili katika Kesi ya mapitio Namba 23/2020 ya North Mara Gold Mine dhidi ya Gerald Nzumbi.

Rais Magufuli amejibu ombi hilo kwa kuahidi kwamba, atafanya haraka kuajiri watumishi wapya wa mahakama.

“Nafahamu changamoto kubwa ya majaji wa rufaa pamoja na majaji wa Mahakama Kuu, nimeshaanza kuifanyia kazi wala msiwe na wasiwasi.”

“Nitalifanya haraka sana ili kusudi majaji wa mahakama ya rufaa na Mahakama Kuu wapatikane mapema,” ameahidi Rais Magufuli.

Kuhusu Jaji Galeba aliyeapishwa leo, Rais Magufuli amemuagiza kufanya kazi yake kwa ukamilifu.

“Jaji mpya wa Mahakama ya Rufaa uende ukafanye kazi, umeipata nafasi kwa mpango wa Mungu, mimi hata sura nilikuwa sikujui, nasema kwa dhati.”

“Lakini nilichukua kile kitendo ulichofanya cha ujasiri, nenda kasimamie ujasiri huo wa kutenda haki na kumtanguliza Mungu sababu ndio alikupa hiki cheo,” amesema Rais Magufuli.

Jaji Galeba, amemuahidi Rais Magufuli kwamba, atafanya kazi kwa uaminifu “nakushukuru kwa kuniheshimisha kunipa nafasi ya juu katika mahakama, mimi sina maneno ya kueleza namna ambavyo nimepokea hii nafasi.”

“Labda niseme kwa ufupi, nakuahidi kukutumikia na wananchi kwa kutenda haki vile ambavyo Mungu anataka tutende haki hapa duniani,” amesema Jaji Galeba.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

TEMESA iliyokarabati Kivuko kwa Bil 7.5 yapata hati chafu

Spread the love  MDHIBITI na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG),...

Habari za Siasa

ACT-Wazalendo yakusanya Mil 8.5/- kodi ya zuio na kutokomea nazo

Spread the love  MDHIBITI na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG),...

Habari za Siasa

DC Kasilda Mgeni ahamasisha chakula shuleni

Spread the love  MKUU wa Wilaya ya Same, mkoani Kilimanjaro, Kasilda Mgeni...

Habari za Siasa

Bilioni 223.9 zapelekwa Tunduru ndani ya miaka 2 ya SSH

Spread the love  ZAIDI ya Sh. bilioni 223.9 zimepelekwa Wilaya ya Tunduru...

error: Content is protected !!