July 5, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Rais Magufuli akabidhiwa Uenyekiti SADC, awatoa hofu wanachama

Rais wa Namibia, Dk. Hage Geingob (kulia) akimkabidhi Uenyekiti wa Jumuiya ya SADC Rais John Magufuli wa Tanzania

Spread the love

RAIS John Magufuli leo tarehe 17 Agosti 2019 amekabidhiwa rasmi uenyekiti wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika SADC. Anaripoti Regina Mkonde … (endelea).

Dk. Magufuli amekabidhiwa kijiti hicho na Rais wa Namibia, Dk. Hage Geingob, Mwenyekiti wa SADC aliyemaliza muda wake, katika mkutano wa 39 wa jumuiya hiyo unaondelea katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam.

Sambamba na kumkabidhi uenyekiti wa SADC Rais Magufuli, Dk. Geingob aliitangaza lugha ya Kiswahili kuwa miongoni mwa lugha nne zinazotumika katika Jumuiya ya SADC.

Akizungumza baada ya kukabidhiwa uenyekiti wa SADC, Rais Magufuli amewatoa hofu wanachama wa jumuiya hiyo akisema kwamba katika uongozi wake atahakikisha anakidhi matarajio ya wanachama wake.

“Najua hii si kazi ndogo na inakuja na matarajio makubwa sana, lakini niwaahidi nitajitahidi sana kufikia matarajio yenu, na kwa manufaa ya Jumuiya yetu,” ameahidi Rais Magufuli.

Rais Magufuli amesema licha ya mafanikio yaliyofikiwa na nchi wanachama wa SADC, bado wanachama wa jumuiya hiyo wanatakiwa kushirikiana kuondoa changamoto zilizopo.

 “Licha ya mafanikio ya ukanda wetu, bado jumuiya yetu ina changamoto. Inatakiwa tufanye kazi kwa pamoja kushughulikia changamoto hizo. Nchi zetu zinatakiwa kuhakikisha zinajiondoa katika migogoro,” amesema Rais Magufuli.

Katika hotuba yake hiyo, Rais Magufuli aliangazia changamoto ya nchi wanachama wa SADC kutotumia vyema rasilimali zake katika kujikwamua kiuchumi ikiwemo kwa kutoanzisha viwanda vya mazao ya kimkakati.

“Hizi ni rasilimali ambazo tukiungana na kuzitumia vyema kwa pamoja kwa manufaa ya wananchi wetu, uchumi wetu utakua, watu wetu hawatokuwa masikini, lakini pia tutakuwa na miundombinu bora ya kushughulika na majanga ya asili,” amesema Rais Magufuli.

Rais Magufuli ameeleza kuwa, kitendo cha nchi za jumuiya hiyo kupeleka malighafi zake nje ya nchi kwa ajili ya kuongezewa thamani kutokana na ukosefu wa viwanda,  kinadidimiza maendeleo ya kiuchumi pamoja na kuminya fursa za ajira.

Wakati huo huo, Rais Magufuli amezitaka nchi za SADC kwa pamoja kupaza sauti zao kuziomba jumuiya za kimataifa ziondoe vikwazo vyake dhidi ya nchi ya Zimbabwe, akisema kwamba vikwazo hivyo vinaathiri maendeleo ya taifa hilo.

“Kama tunavyofahamu, ndugu zetu wa Zimbabwe wamewekewa vikwazo kwa muda mrefu, hili haliiathiri Zimbabwe pekee, linatuathiri sisi majirani pia. Naomba kutumia nafasi kuziasa jumuiya za kimataifa kuiondolea vikwazo Zimbabwe,” amesema Rais Magufuli.

Aidha, Rais Magufuli amesema katika kipindi cha uongozi wake, atahakikisha anafuata nyayo za watangulizi wake, akiwemo Baba wa Taifa, Hayati Julius Nyerere, Marais wastaafu, Al Hassan Mwinyi, Benjamin Mkapa na Dk. Jakaya Kikwete, kuhakikisha kwamba Tanzania inasalia kama alivyoikuta.

“Napenda kuwahakikishia kwamba katika uongozi wangu wa hii nchi, Tanzania mnayoijua itakua kama ilivyo, nawaahidi kufuata nyayo za watangulizi wangu, Mwalimu Julius Nyerere, Mheshimiwa Mwinyi, Mkapa na Jakaya ambao mmewaona hapa,” amesema Rais Magufuli.

Wakati akihutubia kabla ya kukabidhi uenyekiti wa SADC kwa Rais Magufuli, Dk. Geingob ameeleza kufurahishwa na uhusiano mzuri wa marais wastaafu wa Tanzania, akisema kwamba kitendo hicho ni funzo na kwamba Afrika mpya inatakiwa kuwa namna hiyo.

“Nawaona marais wastaafu, Tanzania inatufundisha namna ya kufanya vitu, kuona marais watatu wastaafu wameketi pamoja na kuungana na sisi.  Ni njia ambayo tunataka Afrika iwe,tunajivunia kwenu Tanzania,” amesema Dk. Geingob.

Dk. Stergomena Lawrence Tax, Katibu Mkuu wa SADC amesema nchi wanachama wa jumuiya hiyo zinafanya vizuri katika ukuaji uchumi na kukidhi vigezo vya ukuaji uchumi vya SADC. Huku akiipongeza Tanzania kwa kuwa kinara katika kipengele hicho.

“Nimetoa takwimu jinsi ya nchi wanachama zilivyokidhi vigezo vya uchumi mpana wa SADC. Tuna vigezo vyetu, takwimu zimeonesha nchi wanachama zinafanya vizuri ikiwemo Tanzania, na kwa kipekee kabisa imeweza kufikia kigezo cha asilimia 7 cha ukuaji uchumi,” amesema Dk. Tax.

Hafla ya makabidhiano hayo ilishuhudiwa na marais 11 kati ya 16 wa nchi mwanachama wa SADC, wakiongozwa na Dk. Geingob wa Namibia, wengine ni Cyril Ramaphosa (Afrika Kusini), Danny Faure (Visiwa vya Shelisheli),  Joao Manuel Goncalves (Angola), Edgar Lungu (Zambia), Felix Tshisekedi (DRC).

Marais wengine ni Andry Rajoelina (Madagascar) Emerson Mnangagwa (Zimbabwe) na Phillipe Nyusi (Msumbiji).

Pamoja na marais hao, nchi kadhaa zilituma wawakilishi wake ikiwemno Eswatini iliwakilishwa na Waziri wake Mkuu, Ambrose Dlamini, Lesotho iliwakilishwa na Waziri wake Mkuu, Motsahai Thabane.

error: Content is protected !!