March 6, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Rais Magufuli aikalia kooni Acacia

Spread the love

RAIS John Magufuli ameapa kuibana kampuni ya uchimbaji madini ya Acacia ili ikamilishe ujenzi wa  mradi wa maji unaojengwa wilayani Tarime mkoa wa Mara unaogharimu kiasi cha Sh. 700 milioni. Anaripoti Regina Kelvin…(endelea).

Wakati akizungumza na Wananchi katika kijiji cha Nyamongo wilayani Tarime mkoa wa Mara leo tarehe 7 Septemba, 2018, Rais Magufuli amesema haiwezekani kampuni hiyo ikapata faida kutokana na uchimbaji madini, halafu ikashindwa kutoa sehemu ya faida hiyo kwa ajili ya kusaidia wananchi husika katika kutatua kero ya maji.

Rais Magufuli amesema kuwa “…Wanachimba hiyo dhahabu kwa sababu ya imani yetu, tukiamua hapa wote hakuna hata gari kuingia, haitaingia. Hata polisi wakija hapa hawataweza kupiga risasi wote, lakini msifanye hivyo.”

Sambamba na hilo, Rais Magufuli amemuagiza Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Profesa Makame Mbarawa kuzungumza na kampuni ya Acacia kuhusu utekelezwaji wa mradi huo.

“Huu mradi wa milioni 700 ambao walisema wataleta na hawajaleta, mimi mwenyewe nitadili nao, kwa sababu hakuna mwekezaji aliyekuja kutangaza dini huku.

“Wote wamekuja kuwekeza kwa sababu ya kutafuta faida, sasa hawawezi wakataka faida, hata ile faida kidogo tunayoitaka na yenyewe waichukue, kwa sababu milioni 700 ni kiasi gani kwa mgodi mkubwa unaochukua matrilioni ya fedha? Maji tukose, wao wanakunywa maji ya chupa, hawataki kutupa maji miaka yote wanachukua dhahabu sisi kutupa maji hapana, nasema hili tutalisimamia,” amesema na kuongeza Rais Magufuli.

“Lakini bahati nzuri sasa hivi tumepitisha sheria nzuri ya madini, palikuwa na sheria ya hovyo hovyo ndiyo maana nikasema, tumelaliwa vya kutosha ngoja na sisi tuwalalie, wametugeuza vya kutosha ngoja na sisi tuwageuzie, wametuchezea vya kutosha na sisi lazima tuwachezee.

“Hii mali tumepewa na Mungu na Mungu ndiye alitaka hii mali iwe nyamongo kwa hiyo wale walitakiwa kuyafanya nataka kuwambia watayafanya, kwa hiyo huu mradi wa maji kwa vile ulikuwa ni mradi wao, nitamtuma waziri wa maji akazungumze nao.”

 Rais Magufuli amefikia hatua hiyo baada ya Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Tarime Apoo Tindwa kumueleza kuwa, walikataa kupokea mradi huo kutoka kwa Acacia kutokana na kuwa na mapungufu.

Tindwa alieleza kuwa, mradi huo walipokabidhiwa awali ulikuwa hautoi maji, vile vile uliwekewa umeme wa jua (solar) na kwamba kutokana na hali hiyo walikataa kuupokea hadi pale watakapoweka umeme wa kawaida.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam Malima alisema kwamba, mkoa huo una changamoto ya utekelezaji wa miradi ya maji, na kueleza kuwa mradi huo wa Acacia unachunguzwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (TAKUKURU).

error: Content is protected !!