LICHA ya kuwepo kwa shinikizo kutoka ndani na nje ya nchi kumtaka Dk. John Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuingilia na kutatua mgogoro wa kisiasa visiwani Zanzibar, amegoma kufanya hivyo, anaandika Regina Mkonde.
Msimamo huo ameutoa leo katika Ukumbi wa Diamond Jubilee jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na wazee wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) huku akisisitiza kwamba, Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) kwa mujibu wa katiba, ipo huru kama zilivyo tume zingine duniani.
“Kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar kifungu cha 112 au 115, katiba hainiruhusu kuingilia mgogoro huo, kama ilivyo kawaida kwa tume huru za uchaguzi duniani kote, tume haiwezi kuingiliwa na rais yeyote,” amesema Dk. Magufuli na kuongeza;
“Kuna watu wanasema kwamba niingilie mgogoro wa Zanzibar, sitaingilia na nitaendelea kukaa kimya. Kama kuna mtu atakayetaka tafsiri sahihi ya sheria hii na haki, aende mahakamani.”
Amesisitiza kwamba atakapoingilia mgogoro huo, atakuwa ameingilia kazi ya ZEC na kwamba atakuwa anavunja sheria kwa kuingilia kazi yake ambapo Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) haikuingiliwa katika kazi zake “haiwezekani upande mmoja kuwa huru na kwingine kutokuwa huru.”
Wakati Rais Magufuli akinadi kutoingilia mkwamo huo visiwani Zanzibar, taasisi, wanasiasa, wachumi na watu wa kada nyingine wamekuwa wakionya kutokea kwa vurugu visiwani Zanzibar hasa baada ya Chama cha Wananchi (CUF) kugomea kuingia kwenye uchaguzi wa marudio uliotangazwa na ZEC kufanyika tarehe 20 Machi mwaka huu.
Jumuiya za kimataifa ikiwemo Umoja wa Ulaya (EU) na Marekani tarehe 31 Januari mwaka huu zilitoa taarifa ya kupinga kurejewa kwa uchaguzi visiwani humo wakieleza kuwa, uchaguzi uliofanyika tarehe 25 Oktoba mwaka jana haukuwa na kasoro na hata kufikia hatua ya kurudiwa.
Kutokana na kuwepo kwa hofu ya kutokea vurugu, Rais Magufuli ametisha kwamba wale watakaoanzisha fyokofyoko watakiona.
“Mimi kama Amiri Jeshi Mkuu wa nchi, nawahakikishia usalama wa Zanzibar na Bara, kwa yeyote atakayeleta fyokofyoko ataona,” amesema na kuongeza;
“Iwe Ukerewe, Nachingwea, Dodoma, Pemba, Zanzibar popote pale, wajue vyombo vya usalama vipo kwa ajili ya kuwashughulikia.”
Akizungumzia utendaji wa serikali yake amesema kuwa, imefanya kazi na kujifunza mengi na kwamba, maeneo mengi nchini yameoza katika utendaji.
“Waziri Mkuu alienda bandarini kuangalia mafuta yanayoingia nchini na kubaini hayapimwi kutokana na kifaa kinachotumika kupima mafuta kuharibika kwa miaka mitano,” amesema na kuongeza kwamba ndio maana wananchi wanaona vituo vya mafuta vingi katika barabara ya kutoka Dar es Salaam kwenda Chalinze.
Amesema fedha zilizopotea kwa uzembe huo, zingetengeneza barabara, kuboresha elimu na kufanya mambo mengine mengi na kwamba “hii ndiyo Tanzania tuliyoikuta awamu ya tano.”
Akizungumzia safari yake ya Hospitali ya Taifa ya Muhimbili aliyoifanya juzi, Rais Magufuli amesema akina mama walimwita ili akawatembelee lakini wasaidizi wake walimkataza.
Hata hivyo amesema kuwa, alikataa kusikiliza ushauri wa wasaidizi wake na kuamua kwenda.
“Sikujua kukoje. Niliyoyakuta huko ni maajabu, wodi namba 39 maji yalikuwa yanavuja kutoka chooni yakisambaa kwenye sakafu. Kwenye vyumba vya akina mama nilikuta magodoro wanayolalia yakiwa yamewekwa chini,” amesema Rais Magufuli.
Akizungumzia ujenzi wa barabara za juu Rais Magufuli amesema, mwezi ujao serikali itaweka jiwe la msingi kuashiria kuanza kwa ujenzi huo katika barabara mbalimbali Dar es Salaam.
Miongoni mwa barabara alizozitaja kwamba zipo kwenye mpango wa barabara za juu ni pamoja Dar mpaka Chalinze ambayo pia itakuwa na barabara sita. Pia ametaja njia panda za Tazara, Ubungo.
Amesema Barabara ya Dar es Salaam kwenda Chalinze upembuzi na michoro yake imekamilika huku akibainisha kwamba tayari kampuni 12 zimejitokeza kuomba kazi hiyo.
Amesema, kwa Barabara za Dar es Salaam zimetengwa jumla ya Sh. 260 Bilioni kwa ajili ya ujenzi ikiwa ni pamoja na daraja la Coco Beach hadi Agakhan.
Amesema kuwa, lengo la serikali yake ni kuhakikisha kwamba Watanzania wanakuwa na maisha bora na kwamba “tuliahidi na lazima tutekeleze kwa nguvu zote.”
Hata hivyo, amewataka Watanzania kuwa na utaratibu wa kuomba stakabadhi kwa kuwa, pesa inayopatikana kutokana na bidhaa iliyonunuliwa inatumika katika kuboresha maisha yao.
Inashangaza sana, mtu anayedai kuwa tume za uchaguzi Tanzania ni huru na kwamba Rais hawezi kuingilia maamuzi yake; ndiye huyo huyo anayesisitiza kuwa Tanzania itaongozwa na CCM tu eti kwa sababu vyama vingine vya siasa ni vya ovyo ovyo. Sasa hicho kinachojiita chama hasa cha siasa kinawezaje kujihakikishia ushindi daima ikiwa kweli hakina mkono kwenye tume ya uchaguzi?
Jambo jingine. Gazeti la Mawio lilikuwa likifichua maovu mbalimbali vikiwemo uhujumu uchumi na uozo katika kushughulikia masuala ya uchaguzi kiasi cha kuiweka amani na umoja wa taifa rehani. Uozo huu uliwaudhi Mawio, Watanzania pamoja na Rais. cha ajabu, serikali iliwaona Mawio kama watu wanaoandika mambo mabaya tu ya Tanzania na kuamua kulifuta gazeti hilo. Wakati huo huo, kuna magazeti mengine ambayo yanaandika uozo mbali mbali ndani ya serikali na ndani ya Tanzania, lakini yanasifiwa, kana kwamba kuna uozo mbaya na mzuri.
Ni lini Watanzania watachiwa mamlaka yao ya kuamua nani awaongoze? Ni lini mihimili ya dola itafanya kazi bila mhimili mmoja kuingilia mwingine? “msema kweli mpenzi wa Mungu” Hivi kweli kila Mwenyekiti wa tume anapoongea, tume inakuwa imeongea! Ina maana hapa Tanzania tume ya uchaguzi ni mtu na siyo taasisi! Inashangaza sana kwamba huu ni ukweli.
Barabara, shule na hospitali, hata zikiwa nzuri kiasi gani, zitakuwa na faida gani ikiwa wananchi hawana tena namna ya kuamua nani awaongoze na awaongoze vipi? Yaani wanachi wamenyang’anywa mamlaka kiasi cha kuwafanya watawala kutamba kuwa eti hakuna mwingine wa kutawala isipokuwa wao! Hata Libya walikuwa na neema ya kila kitu, isipokuwa uhuru wa maoni na mamlaka ya kuamua nani awaongoze na awongoze lini na namna gani. Leo Libya ni shida.