Saturday , 2 December 2023
Home Gazeti Habari za Siasa Rais Magufuli aelezea mafanikio, changamoto uenyekiti SADC
Habari za SiasaTangulizi

Rais Magufuli aelezea mafanikio, changamoto uenyekiti SADC

Spread the love

DAKTARI John Magufuli, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na Rais wa Tanzania amesema, katika miaka 40 tangu kuanzishwa kwa jumuiya hiyo (1980), imeimarika na kupiga hatua. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam…(endelea).

Amesema, jumuiya hiyo imepitia mengi na kwamba, wanachama wake wameimarika katika sekta mbalimbali ikiwemo masuala ya usalama na amani, maendeleo ya miundombinu, viwanda na biashara, kilimo na usalama wa chakula, afya, elimu, usawa na uwezeshaji vijana.

Rais Magufuli amesema hayo leo Jumatatu tarehe 17 Agosti 2020 wakati akihutubia mkutano wa 40 wa SADC kwa njia ya mtandao akiwa Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma.

Katika mkutano huo, Rais Magufuli anakabidhi uenyekiti wa SADC kwa Rais wa Msumbiji, Filipe Nyusi.

Rais Magufuli amesema, ni bahati mbaya mafanikio yaliyofikiwa na jumuiya hii, hayashuhudiwi na waasisi wake ambao tayari wametangulia mbele ya haki lakini nchi wanachama wa jumuiya hiyo sasa zipo imara kuliko wakati uliopita.

“SADC imepitia mengi tangu kuanzishwa kwake mwaka 1980. Katika miaka 40 iliyopita SADC imefanikiwa kwenye maeneo mengi ikiwa ni pamoja na masuala ya usalama na amani, miundombinu, viwanda na biashara, kilimo na usalama wa chakula, afya, elimu, usawa na uwezeshaji vijana.”

“Nchi zetu kwa sasa ziko imara kuliko kipindi kilichopita, tunafurahia matunda ya usalama na amani pengine kuliko maeneo mengine ya dunia. Biashara baina ya wanachama wa SADC zimeimarika na umasikini umepungua kipato kimeongezeka na ushandini wa kimataifa umeongezeka,” amesema.

Amewashukuru waasisi wa jumuiya hiyo akiwemo Hayati Mwalimu Julius Nyerere, Rais wa kwanza wa Tanzania na Robert Mugabe wa Zimbabwe kutokana na uamuzi wao wa kuunganisha nchi hizo kwa kuanzisha jumuiya hiyo.

“Ningependa kuwapongeza wanachama wote wa SADC katika siku hii muhimu. Pia, napenda kupongeza juhudi za muasisi wa jumuiya hii kwa kuwa, bila juhudi zao umoja huu tunaouona usingekuwepo.

“Nachukua nafasi hii kuwashukuru waasisi pamoja na viongozi waliosaidia kufikia mafaniko haya. Hata hivyo, tunahitaji tufanye juhudi zaidi ili tufikie malengo ya waasisi wa jumuiya hii,” amesema.

Amesema, angependa waasisi wa jumuiya hiyo wangekuwepo sasa ili kushuhudia matanda yaliyofikiwa na viongozi wake, lakini kwa bahari mbaya waasisi hao hawapo.

“Kwa bahati mbaya, katika shughuli hii leo waasisi wengi hatunao, Septemba mwaka jana tumepoteza mmoja wa waasisi ambaye ni Robert Mugabe, Rais wa Zimbabwe. Natoa pole kwa watu wa Zimbabwe.”

“Ningependa kutumia nafasi hii kueleza kwamba, mwaka huu tarehe 14 Oktoba itafanya maadhimisho ya miaka 21 tangu kuondokewa na Baba wa Taifa hili ambaye ni miongoni mwa waasisi wa SADC, naye ni Mwalimu Julius Nyerere. Na tarehe 13 Aprili 2022 tutasherehekea miaka 100 ya kuzaliwa kwake. Tunawaalikeni nyote,” amesema.

Katika mkutano huo, Rais Magufuli aliwaomba washiriki wamkutano huo, kusimama dakika moja kuwakumbuka viongozi mbalimbali waliopoteza maisha akiwemo Rais mstaafu wa Tanzania, Benjamin William Mpaka.

Rais Magufuli amesema, alipochaguliwa kuwa mwenyekiti wa jumuiya hiyo tarehe 17 Agosti 2019, alijiona kuwa mwenye amani lakini kwa bahati mbaya furaha yake iliingia machungu kutokana na kuingia kwa janga la corona (COVID-19).

“Naomba kutumia nafasi hii kuwapa pole wale waliopoteza ndugu zao kutokana na ugonjwa huu, pia nawatakiwa kupona kwa haraka walioathiriwa na ugonjwa huu,” amesema.

Rais Magufuli ametoa hotuba yake kwa Kiswahili akishukuru nchi wanachama walioridhia Lugha ya Kiswahili kuwa miongoni mwa lugha zinazotumika katika mikutano ya SADC.

Mwenyekiti huyo wa SADC amesema, bado nchi za jumuiya hizo zinakabiliwa na tatizo la ajira licha ya uwepo wa rasimali mbalimbali hivyo, kutoa wito kushughulikia suala hilo kwa kushirikiana kwa karibu.

Balozi wa Msumbiji nchini Tanzania, Monica Clemente amepokea uenyekiti huo kwa niaba ya Rais Nyusi.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari MchanganyikoTangulizi

Mwalimu jela miaka mitatu kwa rushwa

Spread the loveMAHAKAMA ya Hakimu Mfawidhi, wilaya ya Igunga, mkoani Tabora imemhukumu...

Habari za Siasa

Rais Samia kuzindua programu ya nishati safi ya kupikia kwa wanawake Afrika

Spread the loveRais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuzindua programu ya...

Habari za Siasa

AG aiagiza kamati ya maadili kuwashughulikia mawakili wanaokiuka maadili

Spread the loveMWANASHERIA Mkuu wa Serikali (AG), Dk. Eliezer Feleshi, ameagiza Kamati...

Habari za Siasa

Jaji avunja ukimya sakata la Mpoki kusimamishwa uwakili

Spread the loveJAJI Mkuu wa Tanzania, Prof. Ibrahim Juma, amekitaka Chama cha...

error: Content is protected !!