August 19, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Rais Magufuli ‘adai’ pesa zake

Spread the love

SIKU mbili kabla ya Sherehe za Kilele cha Mwenge wa Uhuru kufanyika Bariadi, mkoani Simiyu, waliopokea pesa kwa ajili ya kuhudhuria sherehe hizo, wametakiwa kuzirejesha, anaandika Pendo Omary.

Agizo la kurejeshwa pesa hizo limetolewa leo na Rais John Magufuli kupitia Balozi John Kijazi, Katibu Mkuu Kiongozi.

Kwenye taarifa yake kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Gerson Msigwa, Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Balozi Kijazi amesema, hatua hiyo ni utekelezwaji wa dhamira ya Serikali ya Rais Magufuli katika kupunguza matumizi yasiyo ya lazima.

“Rais Magufuli ameagiza viongozi wote walioalikwa kuhudhuria sherehe za mbio za Mwenge zitakazofanyika tarehe 14 Oktoba 2016 Bariadi, Simiyu kutohudhuria na waliolipwa posho wazirejeshe,” imeeleza sehemu ya taarifa hiyo na kuongeza;

“Viongozi waliotakiwa kufuta safari zao ni wakuu wote wa mikoa, wilaya, wakurugenzi wote wa mamlaka za serikali za mitaa, mameya wote, wanyeviti wa halmashauri za majiji, manisapaa, miji na wilaya pamoja na watumishi wote wangeambatana nao ambao kwa idadi kufika 1500.”

Balozi Kijazi ameeleza kuwa, Rais Magufuli amewataka viongozi hao kwamba, kwa kuwa Sherehe za Kilele za Mbio za Mwenge huambatana na Maadhimisho ya Kumbukumbu ya Mwalim Julius Nyerere, viongozi hao waweke utaratibu mzuri wa kusherehekea siku hiyo.

Hata hivyo, kwenye taarifa hiyo Rais Magufuli ameagiza wilaya zote ambazo zimefanya vizuri katika shughuli za maendeleo wakati Mwenge wa Uhuru ulipokuwa katika maeneo yao, zitambuliwe kwa kutangazwa rasmi katika kilele cha mbio hizo.

Na kwamba, zawadi zitaandaliwa na kupelekwa kwa wahusika kwa utaratibu utakaoelekezwa na mamlaka husika ya kutoa zawadi.

“Kutokana na umuhimu wa Mwenge wa Uhuru kwa Taifa, viongozi wote wa serikali katika Mkoa wa Simiyu, wilaya zake pamoja na wananchi wote wa mkoa huo, wajitokeze kwa wingi na kushiriki katika sherehe za kuzimwa Mwenge siku hiyo,” imeeleza taarifa hiyo.

 

error: Content is protected !!