August 10, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Rais Magufuli achomoa mwingine

Spread the love

RAIS John Magufuli leo amemsimamisha kazi Wilson Kabwe, Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa Daraja la Kigamboni, anaandika Happiness Lidwino.

Kabwe amefutwa kazi baada ya Paul Makonda, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam kumtuhumu mbele ya Rais Magufuli kuwa, amefanya mambo kadhaa yaliosababisha hasara ya Sh. 3 bilion.

Mbele ya Rais Magufuli, Makonda alimtuhumu Kabwe kuwa tarehe 30 mwaka 2015 alisaini mkataba kwa kutumia sheria za mwaka 2009 ambapo ilikuwa inataka kila gari linalotoka Ubungo lilipe Sh. 8,000.

Na kwamba, mwaka huo huo tarehe 31 alidaiwa kusaini mkataba mwingine kwa kutumia sheria za mwaka 2004 ambapo ilikuwa inataka kila gari litokalo Ubungo lilipe Sh. 4000 ambayo ni kinyume cha sheria.

Makonda pia alisema Kabwe amepoteza Sh. 42 milioni kila mwezi kwa kuwa, makadirio yanaonesha kwamba, kuna magari 300 ambapo kila moja linalipa Sh. 4000 kila siku hivyo, miaka ambayo amesaini hadi sasa inafikia Sh. 3 bilioni.

Makonda aliendelea kumkandamiza Kabwe kuwa, ndani ya muda huo aliongeza mkataba wa maegesho ya magari kwa miezi 10 kwa kampuni ambayo imemaliza muda wake ikiwa ni pamoja na ulanguzi wa kodi za mapango kwenye Stendi ya Mabasi ya Ubungo.

Baada ya maelezo hayo, Rais Magufuli alimchukulia hatua Kabwe papo hapo kwa kumsimamisha kazi.

“Ebu jamani niambieni kwa mambo kama haya mnataka nifanyeje?” Rais Magufuli aliwauliza wananchi waliokuwa wamehudhuria uzinduzi huo.

Wananchi walijibu huku wakishangilia “mtumbueeeee hafai huyooooo” baada ya kauli ya wananchi, Rais Magufuli alisema kuwa, aliwaahidi wananchi kusimamia sheria.

Alisema naye anachuki watu wa namna hiyo na kwamba, “kuanzia sasa namsimamisha kazi.”

Akizungumza muda mfupi kabla ya kuzindua rasmi daraja hilo Rais Magufuli alipendekeza jina la daraja kuwa Mwalimu Julius Nyerere kutokana na mchango wake kwa nchi hiyo.

Aidha, Daraja la Kigamboni lilianza kutumika tarehe 16 Aprili 2016 ambapo lina urefu wa mita 680. Ujenzi wa daraja hilo ulifanywa na Kampuni ya China Railway 15 Group ikishirikiana na Kampuni ya China Bridge Engineering Group.

error: Content is protected !!