RAIS wa Tanzania, John Magufuli ameanza kuunda Serikali atakayoiongoza kwa miaka mitano ijayo 2020-2025 kwa kumteua Profesa Adelardus Kilangi kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG). Anaripoti Kelvin Mwaipungu…(endelea).
Uteuzi huo umefanyika leo Alhamisi tarehe 5 Novemba 2020 saa chache kupita tangu Dk. Magufuli alipoapishwa na Jaji Mkuu, Profesa Ibrahim Juma kuwa Rais wa Tanzania.
Dk. Magufuli na makamu wake, wameapishwa kwa pamoja Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma.
“Profesa Kilangi ameteuliwa kushika wadhifa huo kwa kipindi cha pili baada ya uteuzi wa kipindi cha kwanza kumalizika leo tarehe 05 Novemba, 2020,” imeeleza taarifa ya Gerson Msigwa, Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu.
Kabla ya uteuzi huo, Profesa Kilangi alikuwa AG, wadhifa alioteuliwa tarehe 1 Februari 2018 na Rais Magufuli ili kuchukua nafasi ya George Masaju ambaye alimteua kuwa Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania.
Itakumbukwa, mara baada ya Rais Magufuli kuingia Ikulu kwa mara ya kwanza tarehe 5 Novemba 2015, alimteua Masaju kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).
Masaju alishika wadhifa huo wa AG kuanzia tarehe 3 Januari 2015 alipoteuliwa na Rais wa wakati huo, Jakaya Mrisho Kikwete ili kuchukua nafasi ya Fredrick Werema.
Baada ya Rais Magufuli kuingia madarakani, aliendelea na Masaju kwa kumteua kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) nafasi aliyohudumu hadi tarehe 1 Februari 2018 alipomteua Profesa Kilangi.
Kabla ya uteuzi huo wa Profesa Kilangi kuwa AG, alikuwa Mkurugenzi wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino (St. Augustine University) kituo cha Arusha na pia Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Udhibiti wa Shughuli za Mkondo wa Juu wa Mafuta (Tanzania Petroleum Upstream Regulatory Authority – PURA).
Leave a comment