January 19, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Rais Magufuli aanza `kuhonga` vyeo

Spread the love

RAIS wa Tanzania, John Magufuli, amedaiwa kuanza uongozi wa nchi kwa `kuhonga` wapambe na vigogo wa Serikali wanaotuhumiwa na kashfa mbalimbali za ubadhirifu wa mali za umma katika kila kona. Anaandika Moses Mseti, Mwanza … (endelea).

Rais Magufuli ambaye aliapishwa Novemba 5 mwaka huu, kwa sasa ametimiza mwezi mmoja na siku nne tangu achaguliwe  kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Uongozi wa Rais Magufuli unatuhumiwa kuanza vibaya baada ya kuibuka madai ya `kumhonga` nafasi ya Ukurugenzi kigogo anaetuhumiwa na kashfa kibao za ubadhirifu wa mali za umma.

Uongozi wa Magufuli umeanza kwa `kumhonga` nafasi ya ukurugenzi aliyekuwa Kaimu Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza, Tito Mahinya, kuwa mkurugenzi wa Wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya.

Mahinya ambaye ameteuliwa kuwa mkurugenzi wa Mbarali, katika uchaguzi wa Oktoba 25 mwaka huu, aliahidiwa na Chama cha Mapinduzi (CCM) kwamba endapo atamtangaza Mbunge wa sasa wa Nyamagana, Stanslaus Mabula, angepata ukurugenzi jambo ambalo limedhihilishwa.

Pia Mahinya ambaye anatuhumiwa na kuwa ni `fisadi` wa kupindukia hivi karibuni alipandishwa kizimbani baada ya kudaiwa kuuza viwanja vya wananchi wa Nyamongoro Wilaya ya Nyamagana mkoani hapa vya Shilingi 60 millioni.

Pia Mahinya anatuhumiwa ubadhirifu wa mabilioni ya fedha katika Jiji la Mwanza, ni kati ya vigogo wachache katika Jiji hilo la wanaomiliki majumba ya kifahari, shule na hoteli kubwa ambayo moja inadaiwa kuwa kona ya Bwiru (jina linahidhiwa).

Hata hivyo, inadaiwa kuwa baada ya Mahinya kumtanganza mbunge huyo wa Nyamagana, kesi iliyokuwa ikimbabili katika Mahakama ya Mkoa wa Mwanza, ilitupiliwa mbali huku wananchi waliotapeliwa viwanja vyao wakiendelea kusaga maji.

Pia inaelezwa kuwa Serikali ya CCM imeamua kumteua Mahinya na kumpeleka Mbalali mkoani Mbeya kwa lengo la kumpa fadhila baada  `kumchinja` aliyekuwa mgombea wa Chadema, Ezekia Wenje, ambaye alikuwa anapewa nafasi kubwa ya kushinda.

Mahinya ambaye kabla ya kuchaguliwa kuwa mkurugenzi wilayani Mbalali, alikuwa Afisa ugavi wa Jiji la Mwanza, akitokea huko mkoani Mbeya ambaye hata huko inadaiwa aliondolewa baada kuibuka kwa kashfa ya ubadhirifu wa fedha.

Mkurugenzi huyo ambaye pia anatuhumiwa kuwa kinara wa kuandaa mipango na mikakati ya `kuibia` Serikali, mwaka jana katika ubadhilifu wa billioni 40 katika Halmashauli ya Jiji la Mwanza, kitendo chake cha ugavi ndo kilitajwa na PAC kuongoza kwa ubadhilifu.

Hata hivyo inadaiwa kuwa kitendo cha Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kumteua Mahinya kuwa Mkurugenzi, imeelezwa ni mwanzo mbaya wa uongozi wa Rais Magufuli ambaye ameanza kuongoza kwa `mbwembwe`  nafasi hiyo.

Wasomi na wataalamu wa masuala ya kisiasa waliozungumza na gazeti hili, wanadaiwa kuwa kitendo cha uongozi wa Serikali ya Rais Magufuli kuanza kwa kuhonga vigogo wanaotuhumiwa na ubadhilifu wa mali za umma, hautakuwa na tofauti na mtangulizi wake, Rais Mstaafu, Jakaya Kikwete.

Wasomi hao wanadaiwa kuwa ili uongozi wa Magufuli uwe tofauti na watangulizi wake inapaswa asiteuwe vigogo wanaotuhumiwa na wizi wa mali za umma ama wenye chembe chembe za wizi ili kujenga uchumi wa Taifa ulio imara.

Kijana msomi na Mtaalamu wa siasa, John Nyanda, yeye alidai kuwa Rais Magufuli ambaye ameanza kuongoza nchi kwa `mbwembwe` uongozi wake hautakuwa na utofauti wowote kutokana na watu waliomzunguka kuwa ni vinara wa wizi.

Nyanda alidai kuwa uteuzi wa Mahinya ambaye anatuhumiwa na kashfa kibao za wizi, umeonesha ni namna gani Rais Magufuli, alivyoshindwa kuthibiti mianya ya uteuzi mbovu uliofanywa na TAMISEMI kumteua mkurugenzi huyo.

“…, aah uteuzi wa Mahinya uliofanywa na Tamisemi mimi nadhani ni fadhila tu, kwani mtu kama huyo ambaye anatuhumiwa kwa kila kashfa katika Jiji la Mwanza lakini leo hii anateuliwa kuwa mkurugenzi (Mbarali) hiyo ni dalii mbaya kwa uongozi wa Rais (John Magufuli),” amesema Nyanda.

Mahinya aliteuliwa kuwa mkurugenzi wa Wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya baada wabunge wa Tanzania kuapishwa Novemba 12 mwaka huu, Makao Makuu ya Tanzania mjini Dodoma, ikiwa ni siku chache ya kuapishwa kwao.

error: Content is protected !!