October 3, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Rais Magufuli aagiza wanaochunguza masuala nyeti walindwe

Spread the love

RAIS John Magufuli ameagiza vyombo vya dola kulinda watumishi wa Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali wanaochunguza masuala mazito, ili wasiingiliwe katika utekelezaji wa majukumu yao. Anaripoti Regina Mkonde … (endelea).

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Gerson Msigwa, Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Rais Magufuli ametoa agizo hilo leo tarehe 20 Agosti 2019 alipotembelea ofisi hiyo iliyoko jijini Dar es Salaam, kwa ajili ya kuangalia utendaji kazi wake.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa, Rais Magufuli amevitaka vyombo vya ulinzi na usalama kuhakikisha watumishi hao wanakuwa salama na hawaingiliwi kwenye majukumu yao.

Wakati huo huo, Rais Magufuli amewataka wafanyakazi wa Mamlaka ya Mkemia Mkuu wa Serikali kufanya kazi kwa uadilifu pasina kujihusisha na vitendo vya rushwa pamoja na kutoa siri za wateja wao.

Katika ziara yake hiyo,  Rais Magufuli amejionea namna mitambo ya uchunguzi wa kisasa ya ofisi hiyo inavyofanya kazi ikiwemo kuchunguza vinasaba vya miili ya watu waliopoteza maisha katika ajali ya moto mkoani Morogoro, iliyotokea hivi karibuni.

“Katika maabara hiyo, Rais Magufuli amejionea mitambo mipya ya uchunguzi wa vinasaba vya binadamu, sumu, dawa za kulevya na kemikali,” inaeleza taarifa ya Msigwa.

Aidha, Rais Magufuli amemuagiza Profesa Ester Jason, Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka hiyo na Dk. Fidelis Mafumiko, Mkemia Mkuu wa Serikali, kusimamia vizuri matumizi ya fedha za kununulia mahitaji mbalimbali ikiwemo vitenganishi vya maabara.

error: Content is protected !!