January 23, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Rais Kikwete kukutana na Albino

Maalbino wakiandamana

Spread the love

RAIS Jakaya Kikwete, wiki ijayo anakutana na baadhi ya viongozi na wanachama wa Chama cha Watu Wenye Ulemavu wa Ngozi (Albino) ili kuweka “mkakati ya pamoja” wa kukabili vitendo vya mauaji dhidi yao. Anaandika Mwandishi wetu…(endelea).

Hatua hiyo inakuja baada ya viongozi hao “kutishia” kuongoza maandamano ya wanachama wao hadi Ikulu kwa Kikwete, kushinikiza serikali iwalinde.

“Nimekubali maombi yao ya kukutana nao ili niweze kusikiliza maoni yao na tubadilishane mawazo juu ya namna bora ya kumaliza tatizo hili. Mimi naamini kuwa ushirikiano wa karibu kati ya Serikali na jamii utatuwezesha kutokomeza mauaji ya ndugu zetu wenye ulemavu wa ngozi na kuliondolea taifa letu aibu hii,” amesema Kikwete kupitia hotuba yake ya mwisho wa mwezi.

Pia, ameeleza kusikitishwa sana na taarifa kuwa mauaji ya albino yameibuka upya baada ya hali kuwa tulivu mwaka 2011.

“Mwaka 2014 yalitokea matukio matatu katika mikoa ya Mwanza, Tabora na Simiyu na mwaka huu limetokea tukio moja mkoani Geita.

“Lazima tulaani vikali mauaji ya ndugu zetu albino. Ni vitendo vya kinyama ambavyo havitegemewi kufanywa au kutokea katika jamii yeyote ya watu waliostaarabika, ya watu wanaomuabudu Mungu,”anasema.

Rais Kikwete anaongeza kuwa; “walemavu hao ni wanadamu wenzetu, wenye haki sawa ya kuishi na kupata hifadhi ya maisha yao kama walivyo wanadamu wengine”.

Amesema kuwa hawastahili kufanyiwa wanayofanyiwa. Hawapaswi kuishi kwa hofu katika kijiji chao, mtaa wao au katika nchi yao.

Ametoa wito kwa jamii nzima kwamba “sisi sote mmoja mmoja na katika umoja wetu”, wanao wajibu wa kuhakikisha usalama wa maisha yao na mali zao kama ilivyo kwa watu wengine wote.

Kwa mujibu wa rais, “mauaji ya albino ni jambo linalofedhehesha na kulidhalilisha taifa”. Ni vitendo visivyovumilika. Kwamba hawana budi wote kushikamana na kuhakikisha kuwa wanapambana na wahalifu hao na kuwashinda.

“Tangu mwaka 2006 mpaka 2015, watuhumiwa 139 wametiwa nguvuni, miongoni mwao wako watuhumiwa 16 wa matukio ya Desemba na Januari mwaka huu.

Mashauri 35 yamefunguliwa mahakamani na kati ya hayo 10 bado yanaendelea na yapo katika hatua mbalimbali. Watuhumiwa 73 wameachiliwa na 15 wamepatikana na hatia. Kati ya hao waliopatikana na hatia 13 wamehukumiwa kifo na wawili wamepata kifungo cha miezi 6. Watuhumiwa kwa matukio sita bado wanasakwa,” amaesema rais.

error: Content is protected !!