January 19, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Rais Kikwete aungana na mamia kuombeleza msiba wa Komba

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete akisaini kitabu cha maombelezo

Spread the love

MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Jakaya Mrisho Kikwete, ameungana na mamia ya wananchi kuombeleza msiba wa John Damian Komba. Anaripoti Saed Kubenea…(endelea).

Kikwete alifika nyumbani kwa Komba asubuhi ya leo, akiongozana na mkewe, Mama Salma Kikwete.

Mbunge huyo wa Mbinga Magharibi (CCM), alifariki dunia jana majira ya saa 1o jioni wakati akipelekwa katika hospitali ya TMJ, jijini Dar es Salaam.

Wengine waliofika nyumbani kwa Komba, kutoa mkono wa pole, ni pamoja na Spika wa Bunge, Anne Makinda, Mbunge wa Arumeru Mashariki (Chadema), Joshua Nassari, Edward Lowassa, Bernard Membe, Asha-Rose Migiro na Emmanuel Nchimbi.

Wapo pia, Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema, mbunge wa Mbeya Mjini (Chadema), Joseph Mbilinyi (Sugu), Wiliiam Lukuvi, mbunge wa Ismani (CCM) na mtuhumiwa mkuu wa ugaidi nchini, Mwigulu Lameck Madelu Nchemba.

Komba amejipatia umaarufu kupitia kikundi cha uhamasishaji cha Tanzania One Theatre (TOT) na tuhuma za ngono zilizokuwa zikisambazwa katika mitandao ya kijamii.

Mwanajsehi mstaafu wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), alikuwa mmiliki wa kundi la TOT, ambalo amelipora kutoka CCM.

Aidha, Komba alikuwa miongoni mwa wabunge waliokuwa mstari wa mbele kupinga Katiba Mpya yenye maoni ya wananchi

Wakati mjadala wa Katiba ukipamba moto bungeni, Komba alisema, “Katiba Mpya yenye Muundo wa Serikali Tatu ikipita, nitaingia msituni.”

Ndani ya Bunge Maalum la Katiba, Komba alimtuhumu Waziri mkuu mstaafu, Jaji Joseph Sinde Warioba, kuwa ni kibaraka wa nchi za magharibi.

Jaji Warioba, alikuwa mwenyekiti wa Tume ya Rais ya Mabadiliko ya Katiba.

Vilevile, msanii huyo mashuhuri alijiapiza kuwa “Chadema haiwezi kushika madaraka nikiwa bado ni hai.”

Mwanajeshi huyo aliyestaafu akiwa na cheo cha kepteni, anakumbukwa kwa kukubali kutumika. Alikuwa jasiri na asiyeyumba katika msimamo wake wa kutetea yule anayemtuma.

Komba alianza kupata umaarufu akiwa na kikundi cha burudani cha JWTZ wakati huo akiwa hajastaafu jeshi.

Alizunguka na kikundi hicho kila sehemu ya nchi akiwa mwimbaji kiongozi wa kwaya ya kikundi hicho, ambacho pia kilikuwa na sanaa za sarakasi, maigizo na taarab.

Lakini wakati nchi iliporejea kwenye mfumo wa vyama vingi mwaka 1995, kikundi hicho kiliondolewa jeshini na kuingiza moja kwa moja CCM na baadaye kikabatizwa jina la Tanzania One Theatre (TOT).

error: Content is protected !!