January 25, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Rais Kikwete atisha wananchi

Spread the love

RAIS Jakaya Kikwete amewatisha wananchi wanaohamasishwa na viongozi wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) kubakia nje ya vituo ili kulinda kura zao dhidi ya kuibwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM). Anaandika Danny Tibason, Dodoma … (endelea).

Rais Kikwete amesema kila mtu anapaswa kutii sheria na kuonya kuwa serikali haitamvumilia mtu atakayevunja sheria wakati huu taifa likiwa kwenye uchaguzi wa kutafuta viongozi wa serikali mpya.

Alikuwa akihutubia jana kilele cha mbio za Mwenge wa Uhuru, maadhimisho ya Siku ya kumbukumbu kifo cha Mwalimu Julius Nyerere na Wiki ya Vijana yaliyofanyika katika Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma.

Rais Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), alisema kwa vile kazi ya kulinda kura ni kazi ya mawakala, atakayepingana na kauli ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na kulazimisha kuendelea kukaa karibu na kituo cha kupigia kura atambue vyombo vya dola havitamvumilia.

“Niwaombe siku hiyo ikifika, wananchi wakishapiga kura waondoke na kurudi majumbani kwao NEC imekwishawaeleza viongozi wa vyama vya siasa kuwa kazi ya kulinda kura itafanywa na mawakala.

“Mimi nawashangaa wanaowataka wafuasi wao kukaa mita 100 ili walinde kura, hiyo siyo kweli bali wana nia ya kuleta vurugu jambo ambalo halitakubalika,” alisema Kikwete.

Aliwakumbusha viongozi wa vyama vya siasa watambue kuwa uchaguzi mkuu unaongozwa na katiba ya nchi kwa hiyo kazi ya kusimamia uchaguzi huo itafanywa na NEC na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC).

“Viongozi hao wana lao jambo la kutaka kuwatisha baadhi wananchi wengine ili wasiweze kupiga kura, niseme atakaye kwenda kinyume na sheria za maadili ya uchaguzi wa rais, wabunge na madiwani atambue hataheshimiwa atachukuliwa hatua kwani ulinzi wa uhakika upo,” alisema Kikwete.

“Jamani wakati mwingine unaweza kuwaona watu wazima kumbe ni watu wazima ovyo… kicheko kwa wananchi na vijana wa haraiki, haya vijana endelea kuwacheka,” amesema.

Aidha, katika kumuenzi Baba wa Taifa, Rais Kikwete alisihi Watanzania wasikubali kurubuniwa na baadhi ya viongozi wanaotaka madaraka huku tangu mwanzo wa kampeni za uchaguzi wameshindwa kugusia tatizo la rushwa.

Rais Kikwete pia ametaka wananchi wasimchague mwendekeza udini, ukabila, ubaguzi wa rangi na asiye muadilifu kwani kwa kufanya hivyo, atakuja kiongozi atakayenufaisha vikundi vya watu badala ya wananchi wote.

“Mimi natamani kuwa sasa raia mwema na kujiunga na jopo la Mwinyi na Mkapa, ikifika 27 Oktoba mwaka huu mimi wabunge na madiwani utawala wetu unakoma, kama nitakuwa nimeongoza vibaya sura ya utawala itakuwa na sura yangu pamoja na baraza la mawaziri niliofanya nao kazi.

“Hivyo hakikisheni mnatafakari na kufanya uchaguzi sahihi wa kuwapata viongozi wawajibikaji,” amesema.

Waziri Habari, Vijana na Utamaduni, Dk. Fenella Mukangara amesema mbio za mwaka huu zimewezesha miradi zaidi ya 1,000 yenye thamani ya Sh. 400 bilioni imefunguliwa.

Naye mkuu wa mkoa wa Dodoma Luteni Mstaafu Chiku Gallawa amesema mbio hizo mkoani kwake zimewezesha kuzinduliwa kwa miradi 39 yenye thamani ya zaidi ya Sh. 9 bilioni.

error: Content is protected !!