July 6, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Rais Kikwete atawaachia nini albino?

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa maalbno na mawaziri wake

Spread the love

RAIS Jakaya Kikwete, aliyebakiza miezi saba tu ya kustaafu uongozi, yupo kwenye mtihani mgumu wa kutakiwa kufanya uamuzi kabla hajaachia madaraka. Anaandika Jabir Idrissa… (endelea).

Katika muda huo, ana uchaguzi mmoja tu – kufanya uamuzi utakaomjengea heshima katika jamii au kujitengenezea historia ikayomuandama milele.

Anapojiandaa kung’atuka, anashuhudia mzizimo mzito wa shinikizo la kuchukua hatua inayoweza kusaidia kujaza hofu watu wanaoendesha mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi (albino) nchini.

Hatua yenyewe ni kuchukua kalamu, akamwaga wino wa kuidhinisha utekelezaji wa hukumu ya kifo kwa wahalifu waliotiwa hatiani kwa kuhusika na mauaji hayo.

Kufikia sasa, tayari watu 17 wamehukumiwa kushiriki mauaji ya walemavu wa ngozi ambayo yanazidi kushika kasi katika kipindi ambacho taifa linakabiliwa na uchaguzi mkuu wa madiwani, wabunge na rais.

Inajengeka sasa kwamba watafuta uongozi wanasukumwa kuamini kuwa wanaweza kubahatika wakitumia viungo vya albino ambavyo inasemekana hutumika kishirikina kutengeneza bahati.

Shinikizo kwa Rais Kikwete linakuja baada ya jamii yenyewe ya albino kulalamika kuwa serikali inapuuza kukomesha mauaji dhidi yao wakati tishio la mauaji zaidi linaongezeka kila siku.

Wanasiasa wamekuwa wakituhumiwa kuhusika na mipango ya kuuliwa albino ili wapate viungo kwa ajili ya kutengenezewa mambo yao na waganga wa kienyeji. Matukio mengi yanaripotiwa kutokea mikoa ya Kanda ya Ziwa.

Mshtuko mkubwa umeipata nchi kutokana na matukio mawili ya kikatili dhidi ya watoto wenye ualbino. Katika tukio moja, mtoto aitwaye Pendo Emmanuel, (miaka minne), alitekwa nyumbani kwao, wilaya ya Kwimba, mkoani Mwanza, na mpaka sasa hajapatikana.

Naye Yohana Bahati (mwaka mmoja), wa kijiji cha Ilelema, Chato mkoani Geita, alitekwa mikononi mwa mama yake aitwaye Esther, na akakutwa siku tatu baadaye amekufa, baadhi ya viungo vikiwa vimekatwa na kuchukuliwa.

Kilio kimeibuka upya baada ya matukio haya na serikali inazidi kulaumiwa kuwa haijachukua hatua zifaazo katika kukomesha mauaji ya maalbino.

Wakati sauti ya vilio ikipaa angani, washitakiwa wanne waliokuwa wakikabiliwa na kesi ya mauaji ya mwanamke mwenye ualbino, wamehukumiwa kunyongwa hadi kufa.

Nasoro Charles anayetajwa kama mume wa aliyeuliwa, pamoja na Singu Siyantemi, Masalu Kahindi na Ndahanya Lumola, walithibitika kumuua Zawadi Magindu (32) wa Nyamalulu, Kata ya Kaseme, wilayani Geita, mnamo saa 1 usiku, tarehe 11 Machi 2008.

Walitiwa hatiani na Jaji Joacquine De-Mello wa Mahakama Kuu, Kanda ya Mwanza ambaye alisema wakati akisoma hukumu kuwa ushahidi umethibitisha pasina shaka kuwa kwa pamoja na kwa makusudi walikula njama na kumuua Zawadi. Baadhi yao walikiri maelezo ya yaliyotolewa na mashahidi 12, akiwemo mtoto wa marehemu Zawadi.

Hukumu hiyo imechochea mjadala mkali unaoashiria kuibana zaidi serikali na hususan rais aidhinishe adhabu hiyo ili kuzuia mauaji hayo kuendelea.

Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, Rais ndiye pekee mwenye wajibu huo.

Lakini tangu aingie madarakani Oktoba 2005, Rais Kikwete, hajapata kutekeleza wajibu wake huo hata mara moja, ingawa waliohukumiwa kifo wanaendelea kuishi.

Kutotimiza wajibu wake huo kunakuja huku watetezi wa haki za binadamu, zikiwemo asasi za kimataifa, wakiisihi Tanzania ifute adhabu hiyo kwani “inakiuka haki za binadamu na haitoi ufumbuzi wa tatizo kwa kuwa waliokosa wananyongwa.”

Nchi kadhaa zimeondoa katika katiba zao adhabu ya kifo. Tanzania ambayo ina watetezi wanaoendeleza kampeni ya kutaka adhabu hiyo ifutwe, haijaridhia shinikizo hilo.

Kwa mfano, wakati viongozi wa shirikisho la vyama vya watu wenye ulemavu, wakiwemo wabunge Salim Barwany na Al Sheimar Kwegiir, wenye ualbino, wakitaka adhabu hiyo itekelezwe kwa waliohukumiwa, Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) cha nchini, Dk. Hellen Kijo-Bisimba, anasema japo inalenga kukomesha unyama huo, wanaohukumiwa wanapaswa kufungwa maisha ndipo watajifunza na kujutia walichokitenda.

“… Naona kifungo cha maisha kingewafaa zaidi. Naiona haja ya kifungu cha sheria kinachoruhusu mkosaji kunyongwa hadi kufa kiondolewe katika sheria zetu,” anasema, tofauti na Barwany, ambaye anasikitika kuona inakuwa jambo la kawaida sasa kwa adhabu hiyo kutolewa na mahakama nchini, lakini utekelezaji wake unakuwa mgumu hivyo kusababisha wahusika kuendelea kutenda unyama huo.

Anamsihi Rais Kikwete: “Ningemuomba kabla hajamaliza muda wake, achukue hatua hii ninayoweza kusema ni muhimu kwetu na itamfanya akumbukwe siku zote, hususani katika suala kubwa kama hili.”

Juzi, viongozi wa chama cha maalbino walikwenda Ikulu kuonana na Rais Kikwete ambaye pamoja na mambo mengine, walimhimiza kuchukua hatua kali dhidi ya wanaoua wenzao.

Rais Kikwete aliwaambia kuwa si sahihi wanapodhani serikali haiumii kuhusu tatizo hilo, na kuwahakikishia inajitahidi kuchukua hatua na kwamba ipo tayari kushirikiana nao kusimamia hatua makini.

error: Content is protected !!