January 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Rais Kikwete atambia kufunga magazeti

Rais mstaafu wa Tanzania Jakaya Kikwete

Spread the love

RAIS Jakaya Kikwete ameshikilia dhana yake ya kutosheka na kiwango cha uhuru wa vyombo vya habari nchini kwa kuzingatia takwimu za idadi ya magazeti na vituo vya redio na televisheni vilivyopo. Anaandika Jabir Idrissa … (endelea).

Akihutubia kwa mara ya mwisho bunge kabla ya kulivunja rasmi mjini Dodoma leo jioni, Rais Kikwete alisema hawezi kusema hakuna uhuru wa kutosha wa vyombo vya habari nchini.

Alijenga hoja yake kwa kutaja idadi ya magazeti yaliyopo nchini, yanayochapishwa kila siku na kila wiki, na vituo vya vyombo vya kielektroniki – redio na televisheni; na kusifia kuwa Tanzania inaongoza katika nchi nyingi kwa idadi kubwa ya vyombo vya habari.

Rais Kikwete alitaja kwa majina baadhi ya magazeti, na ikatokea yote yapo chini ya umiliki wa kampuni moja ya kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Eric Shigongo ambaye ameshawahi kugombea ubunge kupitia chama hicho jimbo la Buchosa.

Wakati akitaja magazeti ya Shigongo anayemiliki kampuni ya Global Publishers Ltd (GPL), ilitoka sauti ukumbini ikitaja gazeti la MAWIO, lakini Rais Kikwete alijibu kwa kushangaa, “Mawio?” hakuendelea na hoja hiyo.

MAWIO ni gazeti linalomilikiwa na kampuni ya Victoria Media Services (VMS) na ambalo linachapishwa kila wiki chini ya uongozi wa waandishi waliokuwa na Hali Halisi Publishers Ltd (HHPL) ambayo gazeti lake maarufu la MwanaHALISI limefungiwa tangu Julai 2012 kwa muda usiojulikana.

Serikali ya CCM kupitia kwa waziri wake wa habari, utamaduni na michezo, Dk. Fenella Mkangara, imelifungia gazeti hilo kwa madai ya kuchapisha habari na makala za uchochezi. Pia serikali imefungia vituo vya redio.

Rais Kikwete alisema serikali imekuwa na dhamira ya kupanua uhuru wa vyombo vya habari na tayari imeandaa miswada miwili ambayo imeshasomwa bungeni kwa mara ya kwanza, inayohusu huduma za vyombo vya habari na haki ya kupata habari.

Hiyo ni miswada iliyopingwa na wadau wa habari na masuala ya haki za binadamu kwa sababu imejazwa mapendekezo hasi kwa dhamira inayodaiwa kuwepo upande wa serikali.

Wadau wanalalamika kuwa yale mapendekezo ya kujenga msingi imara wa umuhimu wa haki ya kupata habari na kuimarisha uhuru wa vyombo vya habari yaliyoandaliwa na wadau wenyewe, yamewekwa kando na serikali ikachomeka mapendekezo yanayoipa mamlaka makubwa ya kuvidhibiti vyombo vya habari na kuwashurutisha waandishi wa habari.

Malalamiko na jitihada za wadau vikiwemo vyama na asasi za waandishi na wafanyakazi wa vyombo wa habari na mashirika yanayopigania haki za binadamu, yamefanikisha kuikwamisha miswada hiyo kuwasilishwa bungeni.

Wakati Rais Kikwete amekuwa akijinasibu kuwa serikali yake imekuwa ikiheshimu uhuru wa vyombo vya habari, hali inaonesha tofauti kwani katika awamu yake ya uongozi magazeti manne yamefungiwa kwa vipindi tofauti likiwemo la MwanaHALISI ambalo bado liko kifungoni na taarifa kutoka ndani ya watendaji wa serikali yake zinasema halitafunguliwa akiwepo Ikulu.

MwanaHALISI lilijijengea sifa kubwa ya ujasiri kwa kuchapisha habari zilizokuwa zinafichua ufisadi na ubadhirifu wa raslimali za taifa, zikiwemo kashfa zilizowahusu mawaziri, watendaji serikalini pamoja na wafanyabiashara wakubwa walio karibu na viongozi wa kitaifa.

Kampuni ya HHPL ilifungua kesi ya kikatiba kupinga amri ya serikali ya kulifungia gazeti hilo, lakini hata baada ya kutopangiwa kwa jaji kwa zaidi ya miaka miwili, mpaka sasa haijatolewa uamuzi.

error: Content is protected !!