January 23, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Rais Kikwete akutana na Maalim, ngoma mbichi

Spread the love

MAALIM Seif Shariff Hamad, mwanasiasa anayepigania haki yake ya kushika uongozi wa Zanzibar baada ya kutamka kuwa amechaguliwa na wananchi, amekutana na Rais Jakaya Kikwete ndani ya Ikulu ya jijini Dar es Salaam. Anaandika Jabir Idrissa, Zanzibar … (endelea).

Taarifa za kuaminika zilizoifikia MwanaHALISI Online mapema leo, zimesema viongozi wao wa kitaifa walikutana jana, kufuatia ombi rasmi la Maalim Seif kwa Rais Kikwete kutaka wakutane kuzungumzia mgogoro mpya wa uchaguzi mkuu Zanzibar.

Hakuna taarifa iliyotolewa na upande hata mmoja wa viongozi hao, lakini mtoa taarifa wa gazeti hili, amesema kikao cha viongozi hao kilifanyika katika hali ya “utulivu, undugu na urafiki.”

Maalim Seif ambaye Oktoba 26 alitangaza kuwa alikuwa anaonesha kuwa na kura nyingi kumzidi Dk. Ali Mohamed Shein anayepigania kuendelea kushika wadhifa wa urais Zanzibar, alilalamika wiki iliyopita kuwa amekuwa hapati simu ya Rais Kikwete.

Kauli yake iliibua mjadala na Ikulu ikajibu kwamba kitu kama hicho hakipo kwa sababu Rais Kikwete yupo nchini na hajakataa kukutana na mtu yeyote.

Jumatatu Maalim Seif alipokutana na waandishi wa habari alisema amemuandikia barua Rais Kikwete kumtaka wakutane kuzungumzia mgogoro ulioibuka na kwamba kiongozi huyo anawajibu wa kuchukua hatua kuutatua.

“Na huu ni mgogoro usiohitaji utatuzi wa kiulinzi, bali wa kisiasa utakaozingatia Sheria na Katiba. Tume ifanya kazi yake kwa mujibu wa sheria na kumtangaza mshindi wa uchaguzi,” alisema na kusisitiza kuwa yeye na wenzake katika Chama cha Wananchi (CUF) wapo tayari kushirikiana kuunda serikali ya umoja wa kitaifa kama Katiba ya Zanzibar inavyoelekeza.

Maalim Seif pia amesema hana dhamira hata chembe ya kuongoza kwa kulipiza visasi kwa kuwa anaamini wakati wa kufanya hivyo ulizikwa baada ya kufikia maridhiano na Rais mstaafu Amani Abeid Karume mwaka 2009.

error: Content is protected !!