July 6, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Rais Kikwete abebeshwa mzigo ajali ya Mafinga

Alliance For Democratic Center (ADC), Said Miraji Abdulla (kushoto)

Spread the love

CHAMA cha Alliance For Democratic Center (ADC), kimeitaka serikali kuwachukulia hatua kali za kinidhamu askari wote wa usalama barabarani, waliokuwa zamu kwenye eneo la barabara ya Mafinga, Mkoani Iringa, kulikotokea ajali iliyoua watu zaidi ya 45. Anaandika Sarafina Lidwino…(endelea).

Akizungumza na waandishi wa habari, makao makuu ya chama hicho, Buguruni, jijini Dar es Salaam, mwenyekiti wa ADC, taifa, Bw. Said Miraji Abdulla amesema, jeshi la Polisi limeshindwa kulinda raia na mali zao.

Kwa mujibu wa kamanda wa Polisi mkoa wa Iringa, ajali hiyo ilisababishwa na uzito mkubwa wa watu na mizigo, mwendo kasi wa dereva, pamoja na ubovu wa barabara.

Lakini Miraji anasema, “Sasa sitaki kuamini kama tangu mwanzo wa safari hiyo kutoka Mbeya hadi Mafinga, hakuna askari wa usalama barabarani, na kubaini tatizo hilo. Huu ni uzembe na lazima wahusika wawajibishwe.”

Amebainisha kuwa, siyo ajali hiyo tu ambayo husababishwa na uzembe wa jeshi la polisi, bali kuna ajali nyingi za barabarani zilitokana na uzembe wa polisi.

“ Serikali imekuwa ikinyamazia ajali hizi kila siku, kuanzia zile majini, moto na mauaji ya kikatili dhidi ya walemavu wa ngozi albino,” ameeleza Miraji.

Amesema, kutokana na uzembe huo unaofanywa na jeshi la polisi kushindwa kufanya kazi zao ipasavyo, wananchi wanalazimika kujichukulia sheria mkononi ili kujilinda.

Amesema, hatua hiyo imesababisha kutokea mauaji ya raia dhidi ya polisi na raia dhidi ya raia wengine.

“Haya yanafanyika bila kuwapo uthibitisho kutoka mahakamani. Lakini ukiuliza, wanasema ameuawa na wananchi wenye hasira kali.”

Aidha, mwanasiasa huyo amemtaka Rais Jakaya Kikwete, kubaini matatizo ya wananchi wake na kuyafanyia kazi mapema, badala ya kusubiri matatizo yanapotokea ndio achukue hatua.

Amemtolea mfano mvua kubwa ya mawe iliyonyesha mkoani Shinyanga wiki iliyopita, ambapo watu 38 walifariki dunia na wengine 60 kujeruhiwa.

“Mvua ile ya Shinyanga, imepoteza watu wengi na kuacha mamia majeruhi. Baada ya tatizo kutokea, ndipo viongozi wanajitokeza kutoa pole. Ukiwauliza muda wote walikua wapi? Kwa nini wasingedhibiti mitalo mapema? Au leo ndiyo wanasikika wakitaka wananchi wahame mabondeni. Serikali isifanye mzaha katika maisha ya watu,” anasema Miraji.

error: Content is protected !!