January 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Rais Kikwete “abariki” mbio za urais wa Lowassa

Rais wa Tanzania, Jakaya Kikwete (kushoto) akiwa na Waziri Mkuu mstaafu, Edward Lowassa

Rais wa Tanzania, Jakaya Kikwete (kushoto) akiwa na Waziri Mkuu mstaafu, Edward Lowassa

Spread the love

SIRI imefichuka. Mbio za Edward Lowassa, kusaka urais kwa udi na uvumba, zimebarikiwa kwa asilimia 100 na Rais Jakaya Kikwete.

Lowassa amekutana na Kikwete mara kadhaa na kufunga makubaliano ya siri yanayolenga kumsaidia yeye kuwa mgombea urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM). Anaripoti Pendo Omary … (endelea).

“Yote yanayofanywa na Edward (Lowassa), yamebarikiwa na Kikwete. Bila hivyo, Lowassa asingekuwa na ubavu wa kufanya anachokitenda,” ameeleza kiongozi mmoja mwandamizi ndani ya serikali.

Kikwete ndiye Mwenyekiti wa Taifa wa CCM na Rais wa Jamhuri.

Kuibuka kwa taarifa kuwa Lowassa amefunga makubaliano na Kikwete, kumekuja katika kipindi ambacho mwanasiasa huyo aliyeapa kufia katika vita ya kuwania madaraka, ameanza kupokea makundi ya wananchi akidai wanamuomba kugombea urais.

Mtoa taarifa wa gazeti hili anasema, “Kikwete na Lowassa wanakutana sana, tena kwa siri. Wamejadili mengi, ikiwamo kinyang’anyiro cha urais. Itakuwa ajabu, bwana huyu kutokuwa mgombea kupitia CCM.”

Waziri mkuu huyo aliyejiuzulu kwa kashfa ya mkataba tata wa kufua umeme, kati ya serikali na kampuni ya Richmond, tayari amefungulia anaowaita “wafuasi wake,” kushawishi baadhi ya watu kwa lengo la kutafuta kila upenyo kuhakikisha anapata nafasi ya kushika utawala Oktoba mwaka huu.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa watu walio karibu na mwanasiasa huyo, makubaliano yake na Kikwete ndiyo yanayomfanya kuwa “mbogo” hadi kuikuka taratibu za chama chake.

Uchaguzi mkuu unatarajiwa kufanyika mwishoni mwa Oktoba mwaka huu – kuchagua rais, wabunge na madiwani.

Hata hivyo, mtoa taarifa wa MwanaHALISI Online anasema, pamoja na kuwapo makubaliano hayo, bado Lowassa hawezi kujihakikishia nafasi ya kuwa mgombea.

Anasema, Lowassa anakabiliwa na kibarua kigumu kutoka kwa makundi ya yaliyopachikwa jina la “wahafidhina” ndani ya chama chake.

Kundi hilo ambalo limeapa kuhakikisha Lowassa hawezi kupitishwa kuwa mgombea wa CCM, linaongozwa na Benard Membe, waziri wa mambo ya nje na ushirikiano wa kimataifa.

“Bado anakabiliwa na kazi ngumu mbele yake. Ajenda ya kumzuia kuwa mgombea, inasukwa kwa ustadi mkubwa na watu kutoka Idara ya Usalama wa Taifa (TISS), ambao wengi wao wanamuunga mkono Membe,” anaeleza.

Anasema, “…baadhi ya mahafidhina, baada ya kushawishiwa na idara ya usalama, walitaka waongeze adhabu dhidi ya Lowassa na wenzake ili ifikie hadi Februari mwakani. Hii itamfanya yeye na wenzake kutogombea urais.”

Staili ambayo Lowassa ameamua kuitumia, ndiyo ambayo ilitumiwa na Kikwete kuingia Ikulu mwaka 2005. Wakati huo Kikwete na genge lake, waliunda kilichoitwa, “mtandao wa Kikwete mwaka 2005.”

Mtandao wa Kikwete ulitumia vyombo vya habari; kukusanya watu na kuwalipa.

Mbio za Lowassa sasa zimefikia mahali ambako, rais na mwenyekiti wa chama anakotoka, analazimika kutumia, siyo tu busara, bali hekima na uamuzi wa “utu uzima.”

Lowassa na viongozi wengine watano ndani ya CCM, “walitiwa hatiani” 18 Februari mwaka jana, kwa makosa ya kujihusisha na kampeni za uchaguzi kabla ya wakati; kujenga mtandao wa kutafuta urais kinyume cha maelekezo ya chama na kuanza kupenyeza fedha.

Wengine waliotiwa “hatiani” ni pamoja na Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye; Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Benard Membe; Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Stephen Wasira; Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba na aliyewahi kuwa waziri wa nishati na madini, William Ngeleja.

Mpaka sasa bado wako kwenye kifungo baada ya kutiwa hatiani kwa makosa ya kuanza kampeni kabla ya wakati.

error: Content is protected !!